ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 10, 2011

Unampenda sawa, upo moyoni mwake?

NINAMSHUKURU Mwenyezi Mungu Subhana Wataalah kwa kunipa afya njema na nguvu ya kuendelea kuandika. Ni kweli, yeye ndiye kila kitu katika maisha yangu. Nikiacha kusema neno la shukrani kwake, nitakuwa sina busara hata kidogo.

Safu ya All About Love, ipo kwa ajili yako ikiwa na lengo la kufundisha mambo mbalimbali ya maisha. Ukiwa mdau wa kona hii, utaishi maisha ya furaha siku zote, hakika hutajutia kupoteza muda wako!


Huu ni Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, mwezi ambao tunapaswa kutulia na kumrudia Mola wetu, kumtaka radhi kwa dhambi ambazo tumezifanya. Nawapongeza wanaofunga, rafiki zangu ambao hawajafunga nawapa pole kwa sababu wanajiumiza wenyewe bila kujua.

Kufunga katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni moja kati ya nguzo tano za Uislamu, sasa ili uwe muumini kamili, lazima utimize nguzo hii kubwa na muhimu. Kama una sababu za msingi, mathalani maradhi au hudhuru wa lazima, hakuna tatizo ila unapaswa kujitahidi kuwafuturisha Waislamu wenzako, hata maji ya kufungulia wakati wa futuru.

Sasa turudi katika kile kilichotukutanisha. Nazungumzia uhusiano ambao hauna uhakika wa penzi la dhati. Sawa, upo kwenye uhusiano na mwezi ambaye moyo wako umeridhika naye, je, naye anakupenda? Hili ndilo swali la msingi unalopaswa kujiuliza.

Mada hii imezaliwa baada ya kupokea simu kutoka kwa msomaji wangu ambaye anasumbuliwa na msichana anayempenda. Alisema kuwa anapompigia simu, huzungumza naye kawaida, akimtumia waraka pepe humrudishia majibu, lakini huu ni mwaka wa tatu sasa msichana huyo amekuwa hampi jibu linaloeleweka.

Katika hali ya kushangaza, anasema binti huyo amekuwa akimuomba amuamshe kila siku asubuhi ili awahi kazini, ndivyo anavyofanya rafiki yetu huyo. Pamoja na yote hayo, hataki kumwambia kama anampenda au la, kila siku anampiga danadana.

Hilo ndilo tatizo kubwa katika maisha ya rafiki yetu kutoka Moshi, Kilimanjaro. Moyo wake unahisi kumpenda, ingawa sasa amechoka na yupo katika hatua za mwisho za kujilazimisha kuachana naye!

Nasema kujilazimisha kwa sababu anampenda sana, pia ni vigumu moyo kukubali moja kwa moja kuachana naye. Kwa jumla msichana huyo haoneshi kama anampenda. Nilizungumza naye kwa muda mrefu sana nikimshauri, lakini naamini siyo yeye peke yake mwenye tatizo hilo. Huenda hata wewe upo katika kundi hilo.

Nilimpa dawa ya kufahamu kama msichana huyo anampenda, dawa ambayo nitawapa nanyi pia wasomaji wangu wa safu hii maridhawa. Je, uliyenaye au unayehangaika kwa ajili yake anakupenda? Hebu twende tukaone.

DAWA YA UTAMBUZI
Usichanganywe na maneno hayo, mwingine anaweza akajiuliza, hivi jamani Shaluwa anaweza kuwa na dawa ya penzi la dhati? Naam, ipo! Mapenzi kama alivyo binadamu, yanaugua na hupata ajali pia, kama ndivyo, hata dawa zake pia zipo.

Ukiweza kutumia dawa hiyo kwa umakini, utajua kama mpenzi wako yupo na wewe au anakufanya Kadi ya Benki. Tunaangalia penzi la dhati, kimsingi hupaswi kuishi na mwanamke ambaye hakupendi. Nguzo ya kwanza ya kuwa na mume mwema na kamili ni yule anayekupenda. Soma kipengele kinachofuata.

ONYESHA MAPENZI YAKO YOTE
Hata kama anaonesha hakupendi, lakini kwa siku hii ya kwanza, onesha kuwa unampenda kwa mapenzi yako yote. Msogeze karibu kihisia kila wakati, asubuhi mwamshe kwa kumpigia simu, mwambie hivi: “Kumekucha sasa, ni wakati wa kuamka na kuanza siku mpya vyema! Jiandae uwahi kazini, nafanya haya yote kwa sababu nakupenda mpenzi wangu.”

Ni kauli itakayomuacha hoi, itakuwa nzuri zaidi kwake ikiwa kama utakuwa umemuwahi wakati wa kuamka! Mchangamshe siku nzima kwa kumtumia meseji nyingi za mapenzi kadiri uwezavyo. Mwambie unampenda, maisha yako hayawezi kukamilika bila yeye, mwambie yeye ni muhimu sana kwako, onesha mapenzi yako kwake siku nzima.

Mchana mtakie mlo mwema, majira ya jioni mkumbushe apate kimiminika cha moto kwa ajili ya kunyoosha utumbo. Fanya kila unaloweza kumuonesha unampenda. Mfanye acheke kila wakati na akufikirie wewe. Mteke, kuwa kiongozi wa siku yake.

Kwa kufanya hayo, kama mgonjwa alikuwa hawezi hata kula, sasa ataomba maji ya kunywa. Naamini nimesomeka, panapo majaliwa wiki ijayo tutaendelea na sehemu ya pili.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love. Kwa makala zaidi, tembelea www.globalpublisherstz.com

3 comments:

Anonymous said...

Mmmmh kama mtu anakupenda hawezi kukuzungusha na utajua tu anayekupenda anakuhitaji anataka kuwa nawe mara zote ukiona vikwazo ujue hamna mapenzi mapenzi hayachoshi,hayakinaishi yapo level ileile miaka na miaka labda mkerane haswaaa na mkikerana mara kwa mara na aibu nyingi hayo si mapenzi shukrani.

profa said...

Naomba kukupongeza mhandishi wa makala hii ambayo inatoa mafunzo katika jamii yetu ila ningetoa mapendekezo kidogo kuhusu picha,tafuta ya mwanamke wa kiafrika asilia mwenye meno meupe na weusi ule wa maji ya kunde.Nasema hivi kwasababu katika kuandika habari au makala fulani tuiweke katika mazingira ya kiafrika zaidi siyo tufikirie kama wazungu ambao wanaamini kwamba urembo wa mwanamke lazima awe mweupe,mwembaba,mwenye macho rangi ya bluu yote hiyo ni kumtawala mwafrika kisaikologia.
Asante

Anonymous said...

Picha shurti iende sambamba na maneno mwanamke mzuri dawa. Mwandishi hajafanya kosa hata kidogo amenizisuuza nyoyo zetu.