Advertisements

Tuesday, August 9, 2011

Vigogo CCM wanyukana


 Vita ya Zungu na Mtemvu dhidi ya Masaburi yaiva
Mstahiki Meya wa Jiji, Dk. Didas Masaburi
Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, wametoa siku saba kwa Mstahiki Meya wa Jiji, Dk. Didas Masaburi, kuwaomba radhi kwa kuwadhalilisha, asipofanya hivyo watamburuza mahakamani ili akathibitishe tuhuma alizowapa.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa wabunge hao, Abbas Mtemvu, ambaye pia ni Mbunge wa Temeke (CCM), wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema matusi waliyotukanwa kuwa wanafikiri kwa kutumia makalio badala ya kichwa yamewadhalilisha katika chama chao, jamii, wapiga kura wao, wabunge wenzao pamoja na familia zao.

“Nampa siku saba Dk. Masaburi kuomba radhi la sivyo tutamburuza mahakamani ili atoe vielelezo vya tuhuma za ufisadi wa mikataba mibovu na DDC Keko, hao hao anaowatukana hivyo ndio tulimwezesha kuwa Mbunge wa Afrika Mashariki,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Hiki ni kipindi cha pili nachaguliwa kuwa Mwenyekiti DDC kwa nini ananivunjia heshima yangu kwa kunitangazia masuala ya hatari ambayo yatasababisha wananchi wetu kufikiri kwamba wamechagua watu wasiokuwa na akili timamu ... kwa kweli kama ana vielelezo vya hayo aliyoyasema aonyeshe hadharani badala ya kuongea na vyombo vya habari ambavyo vinaandika upande wake bila kuhakikisha wanachokitoa kwenye jamii,” alisema Mtemvu.
Alisema ameshangazwa na kuhusishwa na mikataba mibovu ya Mlimani City, nyumba ya DDC na heka 5,000 zilizoko Ruvu mkoani Pwani bila kutoa uthibitisho wa tuhuma hizo.
Naye Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu, alisema kitendo cha kuhusishwa na tuhuma za kuingia mikataba mibovu ya Machinga Complex sio za kweli na kwamba Masaburi kama ana ushahidi wa mikataba hiyo atoe hadharani vielelezo kuonyesha mahali aliposaini.
Alisema alipokuwa mwenyekiti wa bodi ya Machinga Complex, bodi hiyo ilikuwa ya mpito na haikuwa na nguvu za kisheria za kuingia mkataba na mtu yeyote, kazi yake ilikuwa ni kusimamia vyama vya wafanyabiashara kuingia katika jengo hilo na sio kuingia mikataba na mtu yeyote.
“Amenichafulia heshima yangu kwa wapiga kura wangu, familia, jamii na chama changu pia mimi mtu maarufu 'Top in Dar' nikipita kwa nini anatumia vyombo vya habari kutuchafua badala ya kutumia sheria?” alihoji mbunge huyo.
Alisema matusi aliyoyatoa kwao hayakustahili kwani wamefanya mambo mengi hadi kumwezesha kuwa mbunge wa Afrika Mashariki.
“Mimi ni kiongozi na mtu maarufu siwezi kujibishana naye, hana haki ya kuharibu sifa yangu imenifedhehesha sana, hizo bilioni mbili anazonituhumu aonyeshe nilisaini wapi kuingia mikataba ili ukweli uwe wazi kwa kuwa sikuwa na mamlaka ya kuingia mkataba wowote na mtu yeyote, mzabuni aliyeweka vizimba aliwekwa na Halmashauri na sio bodi iliyokuwa chini yangu, mimi ni mtu na heshima zangu ziwezi kujivunjia heshima niliyopewa na watu wa Ilala, hata 2015 nikiwa hai nitashinda hakuna wa kuniharibia,” alisema Zungu.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu Dk. Masaburi alisema hawezi kuomba radhi kwa kuwa hakutukana wala kumtaja mtu kwamba anatumia makalio kufikiri.
Alisema kama kuna mtu yeyote anahisi ametukanwa aende mahakamani ili aseme ni wapi na siku gani alitoa lugha ya matusi dhidi yake.
“Nasema hivi sijawahi kumtukana mtu wala kumtaja mtu kwa hiyo siwezi kuomba radhi kwa mtu ambaye sijamkosea... anayehisi nimemtukana sina la kusema aende mahakamani ili atoe ushahidi wa malalamiko yake," alisema Masaburi.
Aliongeza: "Sijamsema Mtemvu wala Zungu kwamba mwizi au fisadi bali nimesema sehemu wanazoongoza kuna harufu za rushwa kwa hiyo nimemaliza la UDA, sasa nahamia Machinga Complex na DDC, mashamba ya Ruvu pamoja na mikataba ya Mlimani City, waniache nifanye kazi kwa manufaa ya umma ni haki ya Watanzania," alisema Dk. Masaburi kwa njia ya simu.
Alisema kama kusingekuwa na harufu ya ufisadi kwenye mikataba hiyo, Jiji lingepata gawio, lakini kwa miaka mingi DDC haijatoa gawio.
“Badala ya kunipa siku saba za kuomba radhi, wanipe muda, waniache nikague, suala la UDA kwangu limekwisha, liko serikalini sasa wasubiri kamati iliyoundwa itasema nani ni fisadi sijamsema Zungu wala Mtemvu," alisema Dk. Masaburi.
Akizungumzia kuhusu kumsaidia kupata nafasi ya ubunge wa Afrika Mashariki, Dk. Masaburi alisema si kweli kwani walimpinga na hata katika nafasi ya umeya hawakuwa upande wake.
CHANZO: NIPASHE

No comments: