ANGALIA LIVE NEWS
Saturday, August 6, 2011
Yanga yazuia nyota wake kujiunga Stars
Sweetbert Lukonge na Jessca Nangawe
WAKATI timu ya Taifa 'Taifa Stars', ikijiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan, uongozi wa klabu ya Yanga umelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuwasamehe juu ya wachezaji wake kujiunga na timu hiyo.
Yanga ina wachezaji nane katika kikosi cha Stars kilichoitwa na kocha Jan Poulsen hivi karibuni, ambao ni Shabani Kado, Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub'Canavaro', Chacha Marwa, Julius Mrope, Juma Seif, Nurdin Bakari pamoja na Godfrery Taita.
Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati wataondoka leo kuelekea Sudan walipopata mwaliko wa kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya El Merreikh na Al Halil wiki ijayo michezo itayoingiliana na ile ya timu za taifa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Ofisa habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema TFF wanapaswa kuwasamehe kwa hilo kwa sababu klabu hiyo pia inaenda kuiwakilisha Tanzania kwenye mechi hizo mbili za kirafiki itakazocheza nchini humo.
"Hakuna sababu ya kuanza kulumbana juu ya hili, TFF wanapaswa kutusamehee kwani walikuwa wanafahamu fika kuwa tutakuwa na ziara nchini Sudan na tayari tumeingia gharama mbalimbali za safari juu ya wachezaji hao.
"Tunawaomba TFF watumie busara zao katika hili kwani Yanga, pia inaenda Sudan kuiwakilisha Tanzania," alisema Sendeu.
Timu hiyo inaondoka na wachezaji 18 na viongozi saba, ambapo katika muda wote watakaokuwa nchini humo watacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Al Hilal pamoja na El Meriekh kabla ya kurejea nchini Agosti 10.
Katika hatua nyingine kocha mkuu wa timu hiyo, Sam Timbe alisema kuwa mechi hizo atazitumia ipasavyo ili kupata kikosi cha kwanza cha timu hiyo kabla ya kuanza michuano ya Ligi Kuu.
Wakati Yanga ikisisitiza kuondoka na wachezaji Shirikisho la soka Tanzania TFF limesema klabu hiyo inatambua ratiba za Fifa na endapo itakiuka taratibu hizo itahukumiwa kwa mujibu wa taratibu za FIFA.
Akifafanua suala hilo Ofisa habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mechi hiyo ilikuwa ikijulikana tangu awali na Yanga walifahamu hivyo, hivyo wanapaswa kuangalia lipi muhimu kati yao ama timu ya Taifa.
"Kanuni zipo wazi na sisi tutazifuata kulingana na taratibu, hii mechi sio ya kustukizwa waliifahamu tangu awali, lakini tunachofahamu hili suala lipo kiufundi zaidi hivyo ni vyema makocha wa pande zote mbili (Yanga na Taifa Stars) kukubaliana na kufikia muafaka,"alisema Wambura.
Aidha aliongeza kuwa endapo makocha wa pande zote mbili watafikia muafaka wao kama shirikisho hawana tatizo kwani suala hilo lipo kiufundi zaidi.
Aidha kwa upande wa Simba kupitia kwa Ofisa wao wa habari , Ezekiel Kamwaga alisema tayari wamewaruhusu wachezaji wao walioitwa katika kikosi cha Taifa kuanza kambi na wenzao na hawatawatumia katika tamasha lao la Simba Day litakalofanyika Jumatatu Mkoani Arusha.
Simba tayari ipo mkoani humo kujindaa na tamasha hiloambalo litafanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment