ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 16, 2011

Jahazi yazama, tisa wanusurika


Jahazi ijulikanayo kwa jina la Asaa Robo yenye namba za usajili 328 iliyokuwa ikitokea Tanga kuelekea Wete Pemba ilizama jana asubuhi nje kidogo ya Bandari ya Tanga.
Jahazi hiyo iliyokuwa na wafanyakazi tisa akiwemo Nahodha, wote waliokolewa na boti ya kijeshi ya Tanzania Bara iliyokuwa katika doria.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo baada ya kuwasiliana na Kamanda wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Yahya Rashid Bugi, Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Zanzibar, Issa Haji Gavu, alisema jahazi hiyo ilichukuwa mizigo ya vyakula na magodoro na kwamba inamilikiwa na Mkubwa Omari Saleh.

Alisema ilizama baada ya kugonga mwamba na baadaye kutoboka, hali ambayo ilisababisha kujaa maji na baadaye kuzama.
Gavu aliwataja walionusurika katika ajali hiyo kuwa ni pamoja na nahodha, Issa Sharifu Issa. Mabaharia ni Hussein Saleh Omar, Ali Rashidi Ali, Ahmed Bakari Saleh, Ali Bakari Saleh, Hamad Rashid Ali na Abrahmani Bakari Othman.
Wengine ni Khamis Hamad Seif na Ali Sharif Ali. Wote hivi sasa wamehifadhiwa katika gati kongwe ya kiwanda cha mbolea Tanga na hali zao zinaendelea vizuri.
Kutokana na ajali hiyo Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano imelazimika kuitisha kikao kati yao na wamiliki wa majahazi Jumatatu ijayo, kwa lengo la kuweka mikakati na kudhibiti hali kama hiyo isitokee.
Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Jafari Mohamed, alisema ajali hiyo lilitokea jana majira ya saa 12.00 asubuhi.
Jafari alisema mizigo iliyokuwa imepakiwa katika jahazi hilo mingi ni aina ya vyakula ambapo mzigo wote ulikuwa na thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 16.3.
Akizungumzia tukio hilo mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo aliyelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, Alli Bakari (60) almaarufu kama Shake, alisema kuwa jahazi hilo liligonga gati lililokuwa limezibwa na maji na kusababisha chombo hicho kupasuka.
Bakari alisema baada ya kupasuka kwa chombo hicho ndipo nahodha alifanya maamuzi ya kutaka kurudi walipotoka, lakini ilishindikana kwani maji yalishaanza kujaa chomboni.
“Tulipofika katika gati ya zamani ya mbolea pale nahodha hakuliona lilikuwa limefunikwa na maji sasa kwa sababu lile ni la chuma na chombo kimetengenezwa kwa mbao kilipasuka na kuanza kujaa maji pamoja na jitihada za kutaka kulirudisha, lakini ziligonga mwamba na hali ikawa ni mbaya kwani tulizama kabisa,” alisema majeruhi huyo.
Miongoni mwa mali zilizokuwemo katika jahazi hilo ni pamoja na magunia ya mchele,unga wa sembe,viazi,mafuta ya kula,maharage,mtama, nyanya,iliki, vitunguu na kamba za katani.
Naye Dadi Hamadi (35), mmoja wa walionusurika katika ajali hiyo, alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni vyuma vilivyokuwa vimefunikwa na maji na kuziomba mamlaka husika kuchukua hatua za kuvitoa au kuweka alama nyingine ili kunusuru watumiaji wa usafiri wa majini.
CHANZO: NIPASHE

No comments: