
Magoli mawili, moja kila kipindi, kutoka kwa Mzambia Davis Mwape na Rashid Gumbo jana yaliizindua Yanga kutoka usingizini na kuipa ushindi wa kwanza katika mechi tisa wakati walipoibwaga kwa taabu timu ya African Lyon kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Chamazi pembeni ya jiji la Dar es Salaam.
Yanga iliyozungukwa na migogoro, ambayo ilishindwa kupata ushindi katika mechi zake zote nane za kwanza msimu huu tangu ilipotwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), ilitangulia kupata bao jana katika dakika ya 39 kupitia kwa Mwape aliyeunganisha krosi ya Shamte Ali.
Dakika moja kabla ya mapumziko, Lyon walijibu mapigo kwa goli kali kutoka kwa Hamisi Shengo aliyefunga bao la kusawazisha kwa kutumia mpira wa 'fri-kiki' iliyokwenda moja kwa moja wavuni na kumuacha kipa bora wa msimu uliopita, Mghana Yaw Berko akiwa hoi.
Mabingwa Yanga walianza kipindi cha pili kwa kuwaingiza washambuliaji Gumbo na Mghana Kenneth Asamoah badala ya Shamte na Kigi Makasi mabadiliko ambayo yaliinufaisha klabu hiyo ya Jangwani.
Gumbo aliyejiunga na Yanga msimu huu akitokea kwa mahasimu wao Simba waliomtema kwa madai ya kushuka kiwango, aliipa Yanga ushindi wao wa kwanza msimu huu kwa goli zuri la shuti kali la mbali kutokea nje ya 18 katika dakika ya 63.
Kwa ushindi huo, Yanga imeondoka katika nafasi yao iliyoing'ang'ania kwa muda mrefu ya mkiani na kupaa hadi nafasi ya nane kati ya timu 12 za ligi hiyo kwa kufikisha pointi sita baada ya mechi tano wakati Lyon wameshuka kwa sehemu moja tu kutoka nafasi ya nne hadi ya tano.
Licha ya ushindi huo, kocha wa Yanga, Mganda Sam Timbe alikataa kuzungumza na waandishi akisema "nendeni mkaandike mnavyojua."
Mahasimu wao Simba wanaendelea "kujinafasi" kileleni wakiwa na pointi 13 baada ya mechi tano.
Wakati huo huo, uingozi wa Yanga umesema kuwa sasa hautamvumilia mshambuliaji wake, Khamisi Kiiza, ambaye mara kwa mara amekuwa akichelewa kujiunga na timu yake mara anapomaliza majukumu ya kuitumikia nchi yake.
Kiiza aliyejiunga na Yanga wakati wa mashindano ya Kombe la Kagame mwaka huu, hivi karibuni alikuwa Maputo, Msumbiji na timu ya vijana ya umri chini ya miaka 23 ya Uganda kwenye Michezo ya Afrika 'All-Africa Games' lakini tangu kikosi chao kilipotolewa katika mashindano hayo tangu Jumapili hajarejea nchini.
Akizungumza na gazeti hili jana, Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema kwamba umefika wakati sasa mchezaji huyo atekeleze majukumu yake yaliyoelekezwa kwenye mkataba na si kila siku hadi apigiwe simu ili kujua atarejea lini klabuni.
Sendeu alisema kwamba Yanga inafahamu kuwa timu ya Uganda iliyaaga mashindano hayo tangu Jumapili lakini wanashangaa kuona hadi jana asubuhi Kiiza alikuwa hajarejea nchini au kutoa taarifa zozote zinazomuhusu yeye baada ya kumaliza kuitumikia nchi yake.
"Sasa sijui atasema nini kwa sababu mwenzake Okwi (Emmanuel) alikuwa nae na amerejea na juzi aliichezea Simba ilipocheza na Polisi Dodoma, sasa tutachukua hatua kwa sababu alishaelezwa anachotakiwa kukifanya kwa mujibu wa mkataba wake," aliongeza Sendeu.
Kiiza aliwahi kuchelewa wakati kikosi hicho kikijiandaa na msimu
huu wa ligi na kukaririwa na baadhi ya magazeti kwamba anautaka uongozi wa mabingwa hao wa Kombe la Kagame wammalizie malipo yake ya uhamisho ya Dola za Marekani 15,000 anazowadai, lakini alipozungumza 'live' na kituo kimoja cha radio alikuzisoma taarifa hizo magazetini tu na alidai kushangazwa na waandishi walikozitoa taarifa hizo.
Katika hatua nyingine, mechi ya Ligi Kuu ya Bara iliyochezwa juzi kati ya Simba na Polisi Dodoma kwenye uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam imeingiza Sh. milioni 16.8.
Kutokana na mapato hayo kila timu imeambulia Sh. milioni 3.5 baada ya fedha nyingine kukatwa kodi ambapo idara husika imepata Sh. milioni 2.5.
Tofauti na hofu ambayo Shirikisho la Soka Nchini (TFF) waliingia nayo kuhusiana na idadi ya mashabiki wanaotakiwa kuingia kwenye uwanja huo wa Chamazi, juzi jumla ya mashabiki 2,257 waliingia kushuhudia mchezo huo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment