
Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Thomas Mihayo, jana aliukana uvumi ulioenea kuwa, kiongozi mmoja mkubwa wa serikali aliwashinikiza majaji ili watoe hukumu ya kifungo cha maisha kwa mwanamuziki mashuhuri nchini, Nguza Viking maarufu kama Babu Seya na watoto wake.
“Hakika si kweli…Niliupitia mwenendo wa kesi hiyo na kubaini kwamba kilichokuwa kinasemwa mitaani kilikuwa ni uvumi usiokuwa na chembe ya ukweli,” alisema Jaji Mihayo alipokuwa akizindua rasmi Ripoti ya Ufuatiliaji wa Vyombo vya Habari vya magazeti (Julai 2010-Juni 2011) ya Baraza la Habari la Tanzania (MCT) jana jijini Dar es Salaam.
“Na cha kushangaza, vyombo vya habari vilikuwa vikiutangaza uvumi huu,” aliwaambia waandishi wa habari.
Jaji Mihayo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya MCT, alisema aliusoma kwa kina mwenendo wa kesi ya kulawiti dhidi ya Babu Seya na wanawe kama ulivyoandaliwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu kabla ya kutoa hukumu ya mwisho.
Alisema kwa kuwa Mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kuamua kuhusiana na shauri hilo, ilipokea ukweli wa mwanzo wa shauri hilo na ikauwasilisha Mahakama Kuu.
“Kwa kweli ni mimi ndiye nilikuwa mwenyekiti wa kesi hiyo kama Jaji wa Mahakama Kuu na ndiye niliyetoa hukumu ya mwisho (ya kumhukumu Babu Seya na wanaye kifungo cha maisha),” alisema.
Alisema wakati akizisoma nyaraka na mwenendo wa kesi toka katika mahakama hiyo ya chini (Mahakama ya Kisutu), aligundua kwamba kilichokuwa kikisemwa na watu mitaani ulikuwa ni uvumi tu.
“Si kweli kwamba kulikuwa na ofisa mmoja mkubwa katika duru za serikali ambaye alitoa shinikizo kwa Majaji lililowafanya wafikie kwenye tamati hiyo ya kumhukumu Babu Seya na wanaye kifungo cha maisha,” alisema.
Jaji Mihayo alisema alitenga muda wa kuongea na watoto wasichana waliodaiwa kubakwa na Babu Seya na wanawe na akagundua kwamba watoto hao walikuwa wamelawitiwa na kwamba tendo hilo lilikuwa limefanywa kwa kipindi cha miezi kadhaa.
Alisema aliwasikiliza watoto hao na akapata picha kamili ya kilichoendelea katika matukio hayo na pia aligundua kwamba wazazi wa watoto hao hawakuwa wanajua mwenendo wa watoto wao.
Alifafanua kwamba baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa vikitoa ripoti isiyo sahihi ya kesi hiyo na akasema kwamba kama waandishi wangefanya uandishi wa kiuchunguzi, wangeweza kupata ukweli wa tukio hilo.
“Kibaya ni kwamba waandishi hawakulichunguza tukio hilo kiundani, vinginevyo wangeweza kupata ukweli wenyewe,” alisema Jaji Mihayo.
Alisema uandishi wa kiuchunguzi unakosekana Tanzania na akawaomba wanachama wa vyombo vya habari nchini kusoma hiyo ripoti mpya ya ufuatiliaji wa vyombo vya habari vya magazeti iliyozinduliwa na MCT kwa nia ya kubaini mapungufu yao katika eneo la kuripoti habari za uchunguzi na kuyasahihisha.
Pamoja na hayo, Jaji Mihayo, aliipongeza MCT kwa kufuatilia kwa kina mwenendo wa kitaalamu wa wataalamu wa vyombo vya habari na kuja na ripoti pana na ya kina inayojumuisha masomo mengi…uhuru wa vyombo vya habari, masuala ya kijinsia, walemavu, maadili ya waandishi wa habari, mchakato wa mapitio ya katiba na kadhalika.
“Ninawaasa wataalamu wa vyombo vya habari kuwasaidia watu wanaoishi vijijini, walemavu na wale walio katika makundi ya pembezoni ili waweze kushiriki kwa ukamilifu katika mchakato wa mapitio ya katiba,” alisema. Hivi sasa Babu Seya na mwanaye mmoja, wanatumikia kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kuwalawiti watoto wanafunzi wa kike.
Hata hivyo, washtakiwa wawili waliachiwa huru na Mahakama ya Rufani.
Kwa upande wake, John Mirenyi ambaye ni Meneja wa MCT anayeshughulika na uchapaji, utafiti na nyaraka, alisema kimsingi ufuatiliaji wa vyombo vya habari ni tathmini ya weledi na ufanisi wa maadili wa vyombo hivyo.
Alisema matokeo ya ufuatiliaji huo yatashirikisha wadau wa nje kwa lengo la kuchambua uzito wa ufanisi na mapungufu yake toka kwenye jicho la wataalamu wenyewe.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
SASA NDUGU JAJI,KAMA ULIONGEA NA WATOTO HAO NA KUONA KAMA WALIKUWA WAMELAWITIWA,UKAAMUA KUWAFUNGA WOTE KIFUNGO CHA MAISHA KWANINI MMEWAACHIA WAWILI HURU,NA PAPII NA BABA YAKE BADO WANATUMIKIA KIFUNGO HICHO?
Post a Comment