ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, September 11, 2011

JK amtumia Dk.Shein rambirambi

Rais Dkt.Jakaya Kikwete na Mkewe Mama Salma Kikwete wakimfariji mtoto Said Gerald katika Hosipitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar baada ya kunusurika na ajali ya meli iliyotokea Unguja usiku wa kuamkia Jumamosi Sept 10,2011,aliyempakata mtoto Said ni mama yake mdogo Mariam Hemed(picha kwa hisani ya MICHUZI BLOG)
Kufuatia ajali hiyo mbaya, Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kuomboleza msiba mkubwa wa vifo vya mamia ya watu waliopoteza maisha yao katika ajali hiyo.
“Nimepokea kwa mshtuko, masikitiko na huzuni kubwa taarifa ya ajali na kuzama kwa meli ya Mv Spice Islander, usiku wa kuamkia leo (jana), Septemba 10, 2011. Kutokana na kuzama huko, abiria wengi wamepoteza maisha na wale walionusurika wamepata athari mbalimbali zifanyazo afya zao kuhitaji uangalizi wa karibu. Aidha mali nyingi zimeteketea.


“Haya ni maafa makubwa kwa nchi yetu na Watanzania wote wako pamoja na ndugu zao wa Unguja na Pemba katika kipindi hiki kigumu. Kwa niaba yao nakutumia salamu za mkono wa pole na kupitia kwako naomba unifikishie salamu za rambirambi kwa ndugu zetu waliopoteza ndugu na jamaa zao.
Nawaomba wafahamu kuwa msiba wao ni msiba wetu sote, majonzi yao ni majonzi yetu na uchungu wao ni uchungu wetu sote. Tunawaombea wawe na moyo wa subira na uvumilivu na tunaungana nao kuwaombea marehemu wetu kwa Mola awape mapumziko mema, awasamehe madhambi yao na kuwajaalia pepo,” alisema.
Aidha, Rais Kikwete amewapa pole ndugu walionusurika katika ajali hiyo, na kuwapa pole kwa msukosuko mkubwa walioupata.
“Tunaungana nao kumshukuru Mwenyezi Mungu kuokoa maisha yao na tunawaombea wapone upesi ili waweze kuendelea na juhudi za kujiletea maendeleo yao na kuijenga nchi yetu.”
Alisema kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anamhakikishia ushirikiano Dk Shein katika hatua zote za kukabiliana na janga hili na athari zake. “Tutakupa kila aina ya msaada utakaohitaji tutoe.”
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: