ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, September 11, 2011

Mkapa ashambulia wapinzani safari za JK



Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, amewashambulia wapinzani wanaobeza safari za nje za Rais Jakaya Kikwete wakati wao wanaenda huko kuomba ruzuku kwa ajili ya kuendesha shughuli za vyama vyao.
Mkapa alirusha makombora hayo jana katika viwanja vya Sokoine mjini Igunga, wakati wa uzinduzi wa uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga mkoani Tabora.
Akihutubia umati wa watu uliofurika katika viwanja hivyo, Rais Mkapa, alisema kuwa wamekuwa wakimshtaki Rais Kikwete nje ya nchi kwamba amekuwa akisafiri sana safari za anasa.

“Kwani wao hawaendi, mimi nasafiri nje ya nchi kwenye kazi zangu za kimataifa huko nje nakutana nao (wapinzani) kwenye ndege ndio kusema wanakwenda kwenye anasa? Alihoji.
Alisema kuwa safari za Kikwete ni kwa ajili ya kwenda kuimarisha uhusiano ambao ulishaanzwa zamani lakini wao wamekuwa wakienda kuomba ruzuku kwa ajili yao.
Aidha, alisema kuwa watu wamekuwa wakimsakama kuwa amebinafsisha mashirika ya umma mengi ambayo yamekuwa na mafanikio mazuri.
Alitoa mfano wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambayo ilikuwa ikienda Hazina kuomba ruzuku lakini baada ya kubinafsisha na kugawanya kuwa NMB na NBC zikifanya vizuri.
Aidha, alimsifia Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kuwa ni mpambanaji kweli kweli aliwezesha ujenzi wa barabara katika kiwango cha lami kutoka Nzega hadi Singida.
Alisema amemhakikishia kuwa daraja la Mbutu wilayani hapa ambalo limekuwa likipoteza maisha ya watu wakati wa mvua, limetengewa bajeti kwa ajili ya ujenzi wake.
Katika mkutano huo, Mbunge aliyejiuzulu Rostam Aziz, alipokelewa kwa shangwe na wafuasi wa CCM, ambapo aliusalimia umati wa watu uliokuwa umeshiriki katika uzinduzi huo.
Huku akishangiliwa kwa nderemo na vifijo, Rostam alisema amekuja kushiriki katika uzinduzi wa kampeni hizo kama Mbunge mstaafu, mwana Igunga na mwanachama wa CCM pamoja na kumuombea kura Mgombea ubunge wa jimbo hilo Dk. Peter Kafumu.
‘’Nimekuja kama mwanachama wa CCM, kama mwana Igunga na mbunge mstaafu wa Chama cha Mapinduzi, naombeni mmpatie ushirikiano na kumpatia kura za ndio Dk. Peter Kafumu’’alisema Rostam.
Kwa upande wake, mgombea wa uchaguzi huo, Dk. Kafumu, alimsifia Rostam kwa kazi nzuri aliyoifanya wakati wa uongozi wake.
“Natoa shukrani zangu kwa mbunge aliyetangulia amefanya kazi nzuri na mimi naahidi kuwa nitaiendeleza na namuomba tushirikiane kila atakapopata nafasi,”alisema.
Aidha, aliwaomba wananchi wa jimbo hilo kumchagua ili waweze kushirikiana naye katika kutatua matatizo mbalimbali ya jimbo hilo yaliyobakia.
Kwa upande wake, Katibu wa Uchumi na Fedha Taifa (CCM), Mwigulu Nchemba, ambye ni mratibu wa kampeni hizo za jimboni hapa alisema kuwa CCM katika uchaguzi huu mdogo kina mikasa mingi hasa wa ajali ya mtoto Peter Zakaria aliyegongwa na gari aina ya Fuso wakati wakiandaa mapokezi ya kumpokea Dk. Kafumu.
Alieleza pia tukio jingine la kumwagiwa tindi kali mfuasi wa chama hicho, Mussa Tesha aliyekuwa akibandika mabango katika miti iliyopo mjini hapa.
Alivitaka vyama vya siasa vilivyowania kiti hicho kufanya siasa za kistaarabu na za kujenga tofauti na hivi mambo yanayojitokeza ya kuhatarisha maisha ya wanachama kwa mambo hayo.
Aidha, alisema matatizo yanayo jitokeza katika Serikali ya Awamu ya Nne ni ya kawaida kwani huwezi kuyarekebisha kwa wakati mmoja.
‘’Hata Roma haikujengwa mara mmoja walikaa muda mrefu na wakamaliza hivyo matatizo hayawezi kuisha kwa wakati mfupi tu yanaisha kwa muda muafaka nawaombeni wananchi tuwe pamoja tuijenge CCM yetu na mbunge wetu tupeni kura za ndiyo,’’ alisema.
Mkutano huo uliwashirikisha viongozi wakuu wa chama hicho wakiwemo, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, Katibu Mkuu, Willson Mukama na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, (Mahusiano na Uratibu) na baadhi ya wabunge.
Uzinduzi huo uliopambwa na wasanii mbalimbali kikiwemo kikundi cha vichekecho cha Comedy, ToT na wengine.
Pia wanachama wanasadikika kuwa wa vyama vya upinzani idadi kwenye mabano Chama cha Chadema (180), CUF (17) na SAU (15), walirejesha kadi zao katika mkutano huo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: