Mchuano wa vyama vya siasa katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga mkoani Tabora, umeingia doa baada ya kijana mmoja mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mussa Tesha (24), kuunguzwa usoni kwa kemikali aina ya tindikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathimini wa Jeshi la Polisi, Isaya Mungulu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Akielezea alisema tukio hilo limetokea saa 5:00 usiku Barabara ya Singida ambapo alipigwa na watu zaidi ya watano kabla ya kumwagiwa tindikali.
Alisema mara baada ya polisi kupata taarifa hiyo, walianza kufuatilia na kufanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa. Kuhusu tukio hilo kuhusishwa na mambo ya kisiasa, Mungulu alisema bado haijajulikana kama ni la kisiasa ama la.
Alisema bado wanaendelea na upelelezi zaidi, ili kubaini chanzo chake.
Hata hivyo, Mungulu hakumtaja mtuhumiwa huyo kwa kile alichoeleza uchunguzi unaendelea.
Kijana wa Green Guard, aliyemuokoa majeruhi huyo, Farahani Farahani, alidai kuwa alikutana na majeruhi huyo karibu na shule inayojulikana kama Jitegemee na kwamba wakati anarudi alikutana na wanaume wawili na majeruhi huyo akiwa katikati.
“Nikasema kwamba Katibu alinipigia simu kuwa kuna kijana anatafutwa ametekwa na watu wa Chadema , nikasema ngoja nirudi kama kutekwa na mimi nitekwe kwa sababu tayari nilishapata taarifa kuwa kuna kijana anatafutwa basi nageuza wale vijana wakanisimamisha samahani bwana huyu kijana hebu mpeleke kituo cha polisi,” alidai.
Alidai alipomchukua na kumfikisha katika ofisi za wilaya za CCM hatimaye polisi wakamchukua kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga. Akizungumzia tukio hilo juzi usiku, Katibu wa Fedha na Uchumi wa chama hicho, Mwigulu Nchemba, alisema Chadema wameainisha katika mpango wao kuwa watatumia nguvu kushinikiza kupata ushindi katika uchaguzi wa jimbo la Igunga.
“Ukizingatia kuwa ndio tu wametoka kuzindua inaelekea haya ndiyo maelezo yao ili kuweza kuwatishia wananchi sasa hiki si kitendo cha uungwana niseme waliofanya hiki kitendo na wote waliowatuma wote ni wanyama kabisa na niseme hata shetani sidhani kwamba anaweza akafanya kitendo hiki,”alisema.
Naye Mganga wa zamu, Godfrey Cyril, alisema majeruhi huyo anasadikiwa kujeruhiwa kwa kuunguzwa kwa kemikali aina ya tindikali.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Dk. Joseph Kisara, alisema majeruhi huyo alihamishiwa jana mchana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi. Aliondoka na ndege jana saa 7:00 kwenda katika hospitali hiyo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga (Chadema), Waitara Mwikabe, amesema hawajui lolote kuhusiana na tukio hilo. Alisema hakuna mwanachama wa Chadema ambaye anaweza kufanya tukio kama hilo.
“Siku zote hiyo ni biashara ya CCM, wanafanya matukio ili kutengeneza propaganda, “alisema na kuongeza kuwa wanachama wote wa chama hicho wanafanya kazi walizopangiwa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment