ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, September 11, 2011

Yanga ni `full` kuboronga

Ikicheza bila wachezaji wa kigeni wa kulipwa, timu ya Ruvu Shooting jana iliipelekesha puta Yanga na kutoka nayo sare ya bao 1-1 katika mechi ya ligi kuu ya Bara, kwenye tambarare ya Uwanja wa Taifa jijini.
Kwa matokeo hayo Yanga imefikisha pointi tatu kutokana na mechi nne, pengine mwanzo wake mbaya zadi katika historia ya ligi ya hadhi ya juu zaidi nchini. Imetoka sare tatu na kufungwa mara moja.

Kocha wa Yanga Sam Timbe ambaye alilalamikia ubovu wa sehemu ya kuchezea ya Uwanja wa Jamhuri wa Morogoro baada ya sare nyingine katikati ya wiki, jana alimtaja muamuzi wa mchezo kama sababu ya kutoshinda.
Bao la kuongoza la Ruvu Shooting lilifungwa na Paul Ndauka katika dakika ya 71 baada ya kuunganisha krosi ya Raphael Keyala.
Lakini Keneth Asamoah aliyeingia kutoka benchini wakati wa mapumziko aliisawazishia Yanga kwa shuti kutoka ndani ya eneo la hatari nusu saa tangu kuanza kwa kipindi cha pili, alipounganisha pasi ya Godfrey Taita.
Yanga ilicheza nusu saa ya mwisho ikiwa na wachezaji 10 uwanjani baada ya kiungo wa kimataifa wa Rwanda Haruna Niyonzima kutolewa nje na muamuzi Alex Mahagi kwa kosa la pili la kadi ya njano, la kujiangusha kwenye eneo la hatari.
Awali alikuwa ameonyeshwa kadi yan jano katika kipindi cha kwanza kwa mchezo mbaya.
Muamuzi huyo aliondoka uwanjani chini ya ulinzi mkali wa polisi kutokana na kuwepo kwa hofu ya kufanyiwa fujo mashabiki wa Yanga. Shooting ipo nafasi moja juu ya Yanga, ikiwa na pointi tatu pia baada ya mechi nne.
Timu zote zilifanya mashambulizi ya kutafuta pointi zote tatu lakini kwa mechi ya nne mfululizo, safari hii kwenye uwanja mzuri, Yanga ilishindwa kuibuka na ushindi.
Timbe alisema baada ya mchezo huo kuwa timu yake ilipoteza nafasi nyingi, lakini pia "maamuzi ya muamuzi yametuuma."
Shooting: Benjamin Hengu, Michael Pius, Paul Ngalema, George Michael, Shaban Suzan, Jumanne JUma, Ayoub Kitala, Hassan Dilunga, Abdallah Juma, Kassim Linde, Raphael Keyala.
Yanga:Yaw Berko, Oscar Joshua, Godfrey Taifa, Mohammed Mbegu, Chacha Marwa, Nurdin Bakari, Julius Mrope/Kenneth Asamoah, Haruna Niyonzima, Dennis Mwape, Jerry Tegete/Juma Seif, Rashid Gumbo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: