Baa nyingine mbili zimechomwa moto katika mtaa wa Mbweni katika Mkoa wa Mjini Mgharibi mjini Zanzibar.
Baa zilizochomwa moto usiku wa kuamkia jana ni Nyamachoma na Executive Park ambazo walioshuhudia walisema zilianza kuwaka moto kwa wakati moja saa 12:00 alfajiri.
Zaidi ya watu watano walinusurika kufa katika baa ya Executive ambayo upande mmoja ni nyumba ya kulala wageni.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo watu wenye silaha za kienyeji na bunduki walifyatua risasi hewani kuwatisha walinzi kabla ya kumwaga petroli katika majengo hayo na kuyalipua moto.
Baadhi ya wafanyakazi wa baa ya Executive walisema wakati wamelala walisikia watu wakipita nje na baadaye kidogo kuona jengo linawaka moto na kelele za kuwataka watoke nje.
“Tulipotoka nje, tayari moto ulikuwa umeshika jengo lakini watu walitupa taarifa ya kututaka kuamka nao tayari walikuwa wamekimbia,” alisema mfanyakazi mmoja wa baa hiyo.
Hata hivyo, alisema tukio hilo lilitokea baada ya watu wasiopungua wanne kumtishia mlinzi kwa bunduki na kufanikiwa kuchoma moto baa hiyo.
Meneja wa baa ya Nyamachoma, Muumini, alisema baa hiyo ilikuwa na walinzi wasiopungua wanne ambao ni vijana wa Kimasai.
Alisema wakati watu hao wanaivamia kila mmoja akiwa amevalia kanzu na koti, walinzi wa baa hiyo walikuwa wanaangalia televisheni ukumbini.
“Polisi wamefanikiwa kuokota mabaki ya baruti, inaonekana wahalifu wallikuwa na bunduki bandia iliyosababisha walinzi kusita kupambana nao,” alisema meneja huyo.
Akiwashukuru waliosaidia kuzima moto huo, meneja huyo alisema juhudi hiyo ilifanikishwa na majirani kwa ushirikiano mkubwa na Kikosi cha Zimamoto.
Aliungana na wamiliki wengine wa baa kulalamikia kitendo cha Serikali ya Zanzibar na ya Muungano kushindwa kuchukua hatua za kupambana na uhalifu huo, ambao tayari umesababisha baa 12 kuchomwa moto tangu Januari, mwaka huu.
Hakuna mtu aliyekamatwa kutokana na uhalifu huo, lakini Kamishana wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, katika mahojiano na NIPASHE mara kadhaa alisema matukio hayo ni hujuma na kusema uchunguzi unaendelea.
Si Serikali ya Zanzibar wala ya Muungano zilizotoa tamko lolote juu ya matukio hayo.
Viongozi wa Umoja wa Wamiliki wa Vileo Zanzibar wameomba msaada kupitia njia mbalibali.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment