ANGALIA LIVE NEWS
Friday, September 9, 2011
Dk Slaa, Mbowe wafunika Igunga
Boniface Meena, Igunga
KAMPENI za uchaguzi mdogo jimbo la Igunga, mkoani Tabora zimeanza rasmi huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiwarushia makombora wagombea wa CCM, Dk Dalaly Peter Kafumu na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
Wakati Chadema kilizindua kampeni hizo jana, CCM kinatarajiwa kuzindua kampeni zake huku Mkapa akitarajiwa kuongoza mashambulizi katika uzinduzi huo. Mkapa aliwasili Igunga jana kwa tambo za kuwasambaratisha wapinzani.
Tuhuma za Mkapa
Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Chadema, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibord Slaa alimtuhumu Mkapa kwamba alifanya biashara akiwa Ikulu kutokana na kuanzisha kampuni ya AnBen ambayo alidai kuwa imewaibia Watanzania chini ya mwamvuli wa Ikulu.
"Akija hapa mdaini pango kwa kuwa alifanya biashara akiwa Ikulu wakati ile ni mali ya wananchi,” alisema Dk Slaa.
Alifafanua kwamba, Mkapa akiwaeleza kuwa serikali imeleta maendeleo wana Igunga wamuulize kuhusu fedha ambazo zilitoka Ikulu kwa ajili ya biashara zake binafsi.
Hata hivyo, madai hayo dhidi ya rais mstaafu Mkapa si mapya kwani tayari Dk Slaa alikwishayaibua na kuyatangaza katika maeneo mbalimbali nchini.
Amgeukia Kafumu
Kuhusu Dk Kafumu, Dk Slaa alisema mgombea huyo wa CCM alipaswa ajiuzulu kutokana na kashfa za rushwa zilizoikumba wizara ya Nishati na Madini ambako alikuwa akifanya kazi.
Kabla ya kuteuliwa kugombea ubunge wa Igunga kupitia CCM, Dk Kafumu alikuwa Kamishana wa Madini.
“Kafumu akiongezwa kule kwenye halmashauri ni sawasawa na kuongeza panya kwa kuwa walioko huko ni mapanya na wanaotafuna fedha za wananchi,” alidai Dk Slaa.
Dk Slaa aliwataka wananchi waliokuwa wamefurika katika Uwanja wa Sokoine kumchagua mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye, ili aweze kulinda rasilimali za wana-Igunga katika halmashauri.
Alisema Dk Kafumu hawezi kuleta mabadiliko yoyote jimboni Igunga na taifa kwa ujumla, kutokana na mfumo mbovu wa CCM usioweza kusimamia maslahi ya wananchi.
Dk Slaa alisema nchi inahitaji kutetewa na makamanda ili iweze kufanikiwa kwa kuwa CCM imeshindwa kazi ya kuwasaidia wananchi.
Aliwaambia polisi wanaoagizwa kuwapiga mabomu wananchi wasifanye hivyo, kwa kuwa kazi ya Chadema ni kuwatetea polisi wadogo ambao wanapewa posho ndogo isiyokidhi mahitaji yao.
Mbowe na suti za JK
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema Serikali ya CCM imeshindwa kazi hivyo haifai kuwa madarakani wala kuongezewa wabunge kwa kuwa itazidi kuwadidimiza wananchi.
Alisema haiwezekani rais wa awamu ya nne apelekwe London kupimwa na kununuliwa suti halafu aweze kuwasimamia wananchi wenye matatizo mengi.
“Eti Msemaji wa Ikulu anakanusha ukweli..., hii ni aibu kwa taifa,” alidai Mbowe na kuongeza:
“Nchi inauzwa watu wanapewa suti hii ni mbaya, amekuwa akienda Marekani na akirudi anasema amekwenda huko kuwaona wakubwa watusaide neti..., wametuletea vyandarua hivyo tuvitumie kwa umakini…,” alibeza Mbowe.
Alisema hii ni aibu kubwa kwa nchi ya Tanzania kuomba mgawo wa neti, wakati rasilimali zilizopo nchini zinaweza kutatua tatizo hilo la malaria.
Kashindye ajifananisha na Nyerere
Mgombea Chadema, Kashindye, aliwaambia wananchi wa Igunga kuwa, wakiona mwalimu anaachia chaki na kwenda kwenye siasa, wajue hali ni mbaya na taifa linahitaji ukombozi.
“Hata mwalimu Nyerere aliachia chaki alipoona hali ni mbaya, akaamua kuingia kwenye siasa ili kuikomboa Tanzania tunayoishi leo,” alisema.
Alisema kuwa, CCM wanadhani watumishi wa Serikali ni mali yao kitu ambacho si kweli na kwamba, ameamua kuingia Chadema ili kuwatetea wananchi wa Igunga na taifa kwa ujumla.
“CCM ni chama kinachokufa, nisingeweza kuondoka na kuingia CCM kuwa mbunge wa kusinzia…,” alisema.
Alisema mfumo mbaya wa utawala wa CCM umesababisha fedha nyingi za ujenzi wa barabara wilayani humo kuliwa. Aliongeza kuwa hali hiyo imesababisha wananchi kuendelea kupata mateso.
“Nawaombeni mnitume niende huko bungeni nikawe spika ya Igunga ili nikaseme yote na tupate mafanikio,” alisema.
Mnyika, Heche wanguruma
Naye Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, aliwataka wananchi wa jimbo hilo kutokumchagua Dk Kafumu kwa kuwa ameliingiza taifa katika hasara kubwa kutokana na mikataba mibovu ya madini aliyoingia akiwa Kamishna wa Madini.
Mnyika alidai kuwa, haiwezekani mtu kama Dk Kafumu ambaye amekuwa dalali wa madini ya nchi awe mbunge wa Igunga, kwani atauza mali na almasi ya wana-Igunga.
“Sheria mbovu za madini Kafumu ndiye aliyeziruhusu na ufisadi mkubwa umefanyika katika sekta ya madini chini ya usimamizi wake, alifanya udalali wa kuliibia taifa na amelitia hasara ya Sh2,000 bilioni kwa kuingia katika mikataba mibovu ya madini,” alidai Mnyika na kuongeza:
“Mkapa akija mwambieni hatudanganyiki kwa kuwa wakati wa Serikali yake, ufisadi mkubwa ulifanyika akiwa pamoja na Dk Kafumu.”.
alisema Mnyika.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Heche, alimshambulia Dk Kafumu kuhusiana na mikataba mibovu ya madini ambayo imeliingiza taifa katika migogoro mikubwa na umasikini.
Alisema kuwa, Dk Kafumu hafai kuchaguliwa kwa kuwa yeye na chama chake wamekuwa wakifanya ufisadi ambao umewaweka wananchi katika maisha magumu wakati wao wakifurahia maisha mazuri ya kuwanyonya watanzania.
Heche aliwataka polisi kutojiingiza kwenye shughuli za kisiasa kwa kuwa watasababisha vurugu. Naye Mbunge wa Viti Maalumu wa Chadema, Susan Kiwanga, alisema ni lazima Igunga wahakikishe chama hicho kinashinda kwa kumchagua Kashindye ili aweze kuwatetea bungeni.
Mkapa atua, aanza tambo
Wakati akirushiwa makombora hayo, Mkapa jana alitua Igunga na kueleza kwamba, amefika kupigana na kumnadi mgombea wa CCM.
Rais huyo wa Awamu ya Tatu, alisema amejisikia faraja kusafiri katika barabara ya lami kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza ambayo ni matunda ya CCM.Akiwahutubia wananchi katika Kitongoji cha Makomero alisema ni muhimu wana Igunga wakavipuuza vyama vingine kwa kuwa CCM ikitoa ahadi inatimiza.
"Nimewasili Igunga, wana-Igunga kazi ni moja, ni ushindi tu,” alisema Mkapa wakati akiwasalimia wananchi waliofika kumpokea katika kijiji cha Makomero, kilichoko kilometa nane kutoka mjini Igunga.
"Nashukuru sana kuona kwamba, mara hii nimefika hapa Igunga kwa kupita barabara ya lami, mara ya mwisho nilipita ikiwa vumbi tu. Jamani, haya si maendeleo? alisema Mkapa huku akishangiliwa na wananchi.
Mkapa aliwataka wananchi wa Igunga kujitokeza kwa wingi Oktoba 2, mwaka huu kupiga kura na kuhakikisha wanampigia mgombea wa CCM Dk Dalaly Kafumu na kwamba kwa kufanya hivyo watakuwa wamechagua maendeleo."La msingi ni hilo mengine nitawaambia tutakapokutana katika mikutano ya kampeni," alisema Mkapa.
Mkapa alipokelewa na viongozi mbalimbali wa CCM, waliongozwa na Mratibu wa Kampeni za CCM jimboni humo, ambaye ni Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha, Mwigulu Nchemba, Katibu wa Oganaizesheni wa NEC, Asha Abdallah Juma na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora, Hassani Wakasuvi.
Baada ya kusalimia wananchi msafara wa Mkapa ulielekea Igunga mjini ukiwa na magari kadhaa, yaliyozungukwa na vijana waendesha pikipiki na baiskeli.Uchaguzi mdogo wa Igunga unatarajiwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Rostam Aziz aliyeliongoza jimbo hilo kwa miaka 18.
Hata hivyo, jana hakuna kiongozi wa Chadema aliyemgusa tofauti na miaka ya nyuma walipomtuhumu kwa ufisadi.
Mwanachi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment