Mshambuliaji wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga, Jerryson Tegete, ambaye tangu msimu wa ligi inayoendelea hajaifungia timu yake bao, amesema kuwa maamuzi ya kumsimamisha kwa mwezi mmoja yaliyotolewa na klabu dhidi yake ni ya kumuonea.
Uongozi wa Yanga kupitia mapendekezo yaliyotolewa na kamati ya ufundi ya klabu hiyo uliamua kumsimamisha nyota huyo baada ya kumkuta na hatia ya utovu wa nidhamu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Tegete ambaye baba yake ni kocha wa Toto African inayoshiriki ligi kuu pia, alisema kuwa amepokea barua ya kusimamishwa kwake kwa masikitiko makubwa na kuongea kwamba yeye amefanywa chambo tu, lakini kuna mambo mengi yanayojiri ndani ya klabu hiyo.
Tegete alikataa kueleza kwa undani zaidi, lakini aliongeza kwamba maamuzi yaliyofanywa dhidi yake si suluhisho la mgogoro wa ndani kwa ndani ulioko katika timu hiyo na kuwashauri viongozi wake wasichukue hatua kwa kusikiliza maneno ya 'watu wa pembeni' kwani baadhi yao ndio haohao wanaoiharibu timu.
"Siwaelewi hata kidogo, siwezi kusema zaidi ya hapo, barua wameshanikabidhi na wamenitaka nijieleze, kwa sasa nafikiria kwenda kwetu (Mwanza) kupumzika," alimaliza mshambuliaji huyo ambaye alikuwa tegemeo wakati timu ya taifa, Taifa Stars ilipokuwa chini ya Mbrazil, Marcio Maximo.
Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, aliliambia gazeti hili kuwa maamuzi ya kusimamishwa kwa mshambuliaji huyo yaliridhiwa pia na kocha Sam Timbe, ambaye naye alifikisha ripoti mbalimbali za wachezaji wake kwa uongozi ambapo Tegete huonekana kuzembea na kutofuatilia maagizo anayopewa.
Sendeu alisema vilevile kuwa huo ni mwanzo na uongozi umepanga kuwachukulia hatua kali wachezaji wote watakaokwenda kinyume na mikataba yao na kubwa ni kutii na kutekeleza maelekezo yanayotolewa na viongozi wa benchi la ufundi.
Habari zaidi zinasema kuwa sababu nyingine iliyomfanya Tegete asimamishwe, mbali na utovu wa nidhamu, ni kiwango chake kushuka katika mechi za hivi karibuni jambo linaloibua shaka.
Hali hiyo pia itafanyiwa kazi kwa kuwahoji wachezaji wengine ambao nao kiwango chao kimedaiwa kutiliwa shaka.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment