ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 14, 2011

Wananchi wavamia kituo cha polisi, wapiga gari mawe


Sakata la wananchi kuvamia shamba Karamodo wilayani Siha mkoani Kilimanjaro limechukua sura mpya baada ya wananchi hao kuamua kukishambulia kwa mawe gari na kituo kidogo cha polisi kilichopo katika kijiji cha Ngarenairobi wakishinikiza wenao kuachiliwa huru baada ya kukamatwa na polisi wakituhumiwa kuhusika na vurugu hizo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Obadia Jonas, alithibitisha kutokea vurugu hizo juzi jioni na kusema kuwa watu watatu wanashikiliwa na polisi na kwamba upelelezi utakapokamilika watapelekwa mahakamani kujibu mashitaka.


Alisema watu zaidi ya 100 walifunga njia kwa kutumia magogo huku wakiwashinikiza polisi kuwaachia wenzao na kwamba katika vurugu hizo, wananchi hao walipiga mawe gari la polisi aina ya Land Lover lenye namba za usajili PT 0781 na kuharibika upande wa kushoto.


Alisema wananchi hao walivamia kituo cha polisi katika kijiji hicho kwa lengo la kushinikiza kutolewa kwa wenzao waliokuwa wakishikiliwa kituoni hapo na kwamba tukio hilo lilitokea juzi usiku katika kijiji cha Ngarenairobi majira ya saa 2:00 usiku.

Juzi wananchi wa kijiji hicho walivamia shamba hilo na kugawana shamba lililokuwa likimilikiwa na
Shirika la Chakula na Kilimo (NAFCO) lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 2747 ambapo polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto.

Habari kutoka wilaya humo zimedai kuwa wananchi hao wameamua kuvamia shamba hilo kufuatia madai yao ya muda mrefu wakiomba serikali iwagawie ardhi hiyo kufuatia wao kukosa ardhi kwa ajili ya mashamba na kujenga makazi ya kudumu.

Baadhi ya watu waliozungumza na NIPASHE katika eneo la tukio na kuomba majina yao yasitajwe, walidai kuwa kwa muda mrefu serikali imekuwa na nia ya kutaka kulibinafsisha shamba hilo bila mafanikio huku wao wakiwa wamehamishwa kutoka kwenye makazi yao ya awali na kuhamishiwa kwenye ardhi ya muda ambayo haijapimwa na hawaruhusiwi kujenga makazi ya kudumu, jambo ambalo walidai linawakwamisha kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: