ANGALIA LIVE NEWS
Monday, September 12, 2011
Waislamu sasa kuandamana kushinikiza Mahakama ya Kadhi
Aidan Mhando
JUMUIYA ya Taasisi za Kisilamu, imesema utatumia maandamano ya usiku na mchana, kushinikiza kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na kwamba hatua hiyo inakuja baada ya kushindikana kwa njia ya kidiplomasia, kuhusu kuanzishwa kwa mahakama hiyo.
Hayo yalibainishwa jana na Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Shehe Issa Ponda, alipokuwa akisoma tamko la msimamo wa Taasisi za Kisilamu kufuatia kauli ya Rais Kikwete katika Baraza la Idd el Fitri, lililofanyika Septembe mosi mwaka huu mjini Dodoma, kuhusu kuanzishwa kwa mahakama hiyo.
Shehe Ponda alizitaja taasisi zilizokutana na kuazimia kutoa tamko hilo kuwa ni pamoja na Baraza Kuu, Jopo la Mashehe, Baraza la Vijana wa Kiislamu na Basuta.
Alisema, baada ya kukutana wameamua kutoa tamko la kupinga hotuba ya Rais Kikwete na kwamba hatua hiyo imetokana na kutokubaliana na baadhi ya vipengele vilivyomo katika hotuba yake kuhusu kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.
“Moja ya vipengele vilikuwamo katika hotuba yake (Rais Kikwete) ni kwamba Serikali haitaanzisha Mahakama ya Kadhi na kwamba badala yake Waislamu wenyewe ndiyo waanzishe mahakama hiyo. Hii moja inonyesha kutokukubaliana juu ya kuanzishwa kwa mahakama hiyo,” alisema Shehe Ponda.
Alisema hakuna mahakama yoyote inayoweza kuanzishwa ikiwa nje ya dola na kwamba vinginevyo mahakama hiyo haitakuwa na nguvu katika kutekeleza majukumu yake.
“Lakini pia Jumuiya ya Taasisi za Kislamu, inapingana na kifungu cha pili na cha tatu cha hotuba kwamba Mahakama ya Kadhi haitowekwa ndani ya katiba, jambo linalomaanisha kwamba haitakuwa na nguvu kama ilivyo kwa mabaraza ya Kiisilamu ambayo yamesajiliwa kwa utaratibu wa kawaida lakini hayana uwezo wa kisheria,”alisema Shekhe.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya za Taasisi za Kiislamu, Ramadhani Sanze, alisema njia pekee ya kudai haki ya kutaka kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi hapa nchini ni kufanya maandamano ya usiku na mchana ili kilio cha Waislamu kiweze kusikilizwa.
“Wasilamu hawawezi kukubali kuona haki yao ya msingi ya kutaka kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi haipatiwi majibu sahihi, Kumekuwa na maneno mengi ya kuzungushwa kuhusu undwaji wa chombo hiki muhimu ambacho tunaamini kitasaidia kupunguza matatizo ya Waislamu,” alisema Shehe Sanze.
Alielezea kushangazwa kwake na kauli ya Rais Kikwete kwamba mahakama hiyo, itanzishwa na Wasilamu wenyewe.Alisisitiza kuwa waumini wa dini hiyo, wanaamini kuwa hakuna mahakama yoyote inayoweza kuwa na nguvu kama itakuwa nje ya dola.
“Kauli ya Rais Kikwete inaashiria kwamba hakuna uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, mahakama yoyote haiwezi kuwa nje ya chombo cha dola vinginevyo, haitakuwa na nguvu za kisheria,” alisema Sanze.
Mwanachi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment