ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 13, 2011

Dk. Mwakyembe afanyiwa uchunguzi kubaini maradhi yanayomsumbua


Madaktari bingwa wa Hospitali ya Indraprasta Apollo, iliyopo mjini Chinai, nchini India, wamechukua vipimo mbalimbali kwa lengo la kufahamu kinachomsumbua Mbunge wa Kyela, mkoani Mbeya, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye amelazwa katika hospitali hiyo.
Akizungumza na NIPASHE kwa simu, Katibu wa Mbunge huyo, Salum Nkambi, alisema hali ya Dk. Mwakyembe, ambaye alisafirishwa kupelekwa nchini India kwa ajili ya matibabu, inaendelea vizuri na madaktari wamekwishachukua vipimo ili waweze kubaini kinachosumbua mwili mwake.
‘’Hivi punde kama saa moja iliyopita, nimetoka kuongea na Dk. Mwakyembe. Kimsingi, hali yake inaendelea vizuri na madaktari wamemchukua vipimo kuanzia juzi (Jumanne). Jana (Jumatano) na Alhamisi (leo) watamchukua vipimo vingine ili kukamilisha utaratibu wao wa kuchunguza afya yake,”alisema Nkambi.

Awali, akizungumza na NIPASHE moja kwa moja kutoka nchini India katika hospitali hiyo, Dk.Mwakyembe alisema kwa kifupi kuwa anaendelea vizuri na kwamba, tangu afikishwe hospitalini hapo, amepata ushirikiano mzuri kutoka kwa madaktari.
Habari za uhakika, ambazo NIPASHE imezipata kutoka vyanzo mbalimbali serikalini, zinaeleza kuwa serikali inatarajia kutoa taarifa rasmi kuhusu ugonjwa unaomsumbua Dk. Mwakyembe siku yeyote kuanzia kesho mara baada ya madaktari kutoa majibu.
Inaelezwa kuwa serikali imeamua kuchukua hatua ya kuwaeleza Watanzania suala hilo kutokana na kuwapo kwa uvumi nchini, ambapo imefikia hatua baadhi ya watu wanadai kuwa amepewa sumu.
Tangu Dk. Mwakyembe apelekwe nchini humo mapema wiki hii kwa ajili ya matibabu, kumezuka mjadala kuhusu maradhi yanayomsumbua Dk. Mwakyembe hali iliyosababisha kila mtu kuzua jambo lake na hivyo kuwakanganya Watanzania.
CHANZO: NIPASHE

No comments: