Wasusa kikao, watoka nje
Waeleza hawataki kuburuzwa
Waeleza hawataki kuburuzwa
Wabunge hao ni Joseph Mbilinyi maarufukwa jina la Mr. II Sugu ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), kupitia Mkoa wa Mbeya, Naomi Kaihula, ambao kwa mujibu wa sheria ni madiwani wa halmashauri hiyo.
Kabla ya kuzuka kwa sakata hilo, madiwani wawili waliochaguliwa hivi karibuni, David Mwashilindi wa Kata ya Nzovwe (Chadema) na Samweli Mwamboma wa Kata ya Majengo (CCM), waliapishwa na kuungana na madiwani wenzao katika kikao hicho.
Hata hivyo, wakati Meya wa Jiji, Athanas Kapunga, akianza kuendesha kikao hicho, Mwenyekiti wa Madiwani wa Chadema, Boid Mwambulange ambaye ni Diwani wa Kata ya Forest, alisimama na kudai kuwa baadhi ya hoja ambazo kambi ya upinzani inaziona kuwa ni muhimu hazikuingizwa kwenye ajenda.
Baada ya Mwabulange kutoa malalamiko hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ambaye ndiye Katibu wa Baraza hilo, Juma Rashid Idd, alisimama na kutoa maelekezo ya kanuni zinazopaswa kufuatwa wakati wa kuandaa ajenda za vikao vya Baraza hilo.
Baada ya maelekezo ya Mkurugenzi, Mwabulange alisimama tena kutaka kutoa maelezo zaidi na ndipo Meya Kapunga, alipolazimika kuingilia kati kwa kumuamuru kukaa chini na kufuata kanuni za uwasilishaji wa ajenda.
Hata hivyo, Mwabulange alikaidi amri ya Meya ya kumtaka kukaa chini na ndipo yalipoibuka mabishano kwa dakika kadhaa huku diwani huyo akiendelea kusimama huku akiungwa mkono na madiwani hao wa Chadema ambao walikuwa wakizungumza kwa sauti za juu.
Kufuatia hali hiyo, Meya Kapunga aliamua kuwahoji madiwani wanaotaka kikao hicho kiahirishwe na wale wanaokubali kiendelee. Madiwani wa CCM ambao ni wengi ndani ya Baraza hilo walitaka kikao hicho kiendelee, huku madiwani wa vyama vya upinzani wakitaka kiahirishwe.
Baraza hilo linaundwa na madiwani 22 wa CCM, Chadema (18) na NCCR-Mageuzi (2).
Baada ya kura hiyo iliyopigwa kwa staili ya madiwani kusimama, ilionekana madiwani wa Chadema wameshindwa kutokana na idadi yao kuwa ndogo na ndipo Mbilinyi alipowaongoza wenzake kuinuka na kutoka nje ya ukumbi wa mkutano.
Wakizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi huo, madiwani hao walisema wameamua kutoka nje ya ukumbi kwa kuwa hata wakibaki ndani hawataweza kuwatetea wananchi bali watakuwa wanaburuzwa na wingi wa wabunge wa CCM.
Mbilinyi alisema uamuzi waliouchukua ni sahihi kwa kuwa kwa kufanya hivyo wanakuwa wamepaza sauti yao inayopinga kuburuzwa na wingi wa madiwani wa CCM ambao hawajali nguvu ya hoja na badala yake wanatumia nguvu ya idadi yao kuamua mambo yasiyo na maslahi kwa wakazi wa Jiji la Mbeya.
“Nikiwa mmoja wa madiwani tulioungana kutoka nje ya kikao, naamini kuwa tumefanya kitu sahihi kwa kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kupaza sauti zetu kupinga Meya Kapunga anavyopotoka kuliendesha Baraza hilo,” alisema Sugu.
Alisema wao wamechaguliwa na waliowataka wawatetee hivyo haiwezekani wakakubaliana na hoja zinazoletwa kwenye vikao huku zikiwa zimepitwa na wakati, ilhali kuna hoja za msingi zinazopaswa kujadiliwa.
Mwenyekiti wa wabunge hao, Mwambulange, alizitaja hoja zilizopaswa kujadiliwa katika kikao cha jana kuwa ni pamoja na kuteketea kwa soko la Mwanjelwa lililopo eneo la Sido pamoja na kamati zilizoundwa na meya kinyume cha sheria kufanya uchunguzi wa tuhuma zisizo na ukweli zinazowakabili baadhi ya madiwani wa Chadema akiwemo yeye.
“Meya aliteua tume hizo pasipo idhini ya kikao chochote cha baraza la madiwani. Tume hizo zimetumia fedha nyingi za halmashauri kinyume cha utaratibu. Sasa hatuwezi kukubali kuacha hoja hizo zipite hivi hivi kwa kuendekeza ubabe wa Meya Kapunga,” alisema Mwambulange.
Baada ya wabunge wa Chadema kususa, kikao hicho kiliendelea kwa muda kwa kujadili sababu za wabunge hao kususa na baadaye kuahirishwa huku Meya Kapunga akisema kitendo kilichofanywa na madiwani hao ni cha aibu kwa kuwa walitaka kushinikiza kikao kujadili mambo ya kuwapotosha wananchi.
“Binafsi niliona kama watu waliotoka kwa mapumziko mafupi ya kwenda msalani au kupunga upepo. Ninawashukuru wengi mliopiga kura ya kuendelea, ” alisema Kapunga.
Naye Mkurugenzi Idd akizungumza na waandishi wa habari, alisema walichokifanya madiwani wa Chadema ni jambo la kidemokrasia kwa kuwa mtu ana uwezo wa kuamua kutoka au kubaki ndani ya kikao kulinaga na anavyoona uzito wa hoja inayojadiliwa.
Akizungumza na NIPASHE juu ya uamuzi wa madiwani hao kutoka nje ya ukumbi wa mkutano, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija, alisema hawakukubaliana na uamuzi wa Meya Kapunga ambaye alikataa kujadili hoja za msingi na kuleta hoja ambazo wao wanaona hazina maslahi kwa wananchi.
Mwambigija alisema madiwani wa Chadema walitaka kwanza ijadiliwe hoja ya kuungua kwa soko la Mwanjelwa ili kutafuta njia ya kuzuia matukio kama hayo yasitokee tena.
Alisema madiwani hao hawakukubaliana na uamuzi wa Meya kukataa kujadiliwa kwa hoja ya msingi kama hiyo na kutaka kujadili hoja za mambo ya Februari, ambazo wao wanaona kuwa hazina umuhimu kwa sasa.
Naye Mbunge Kaihula alisema tatizo kubwa ni unyanyasaji wa Meya Kapunga kwa madiwani wa Chadema kwa kutaka kuendesha kikao hicho kidikteta bila ya kujali kanuni za vikao.
Alisema hoja zilizoandaliwa zilikuwa zimepitwa na wakati na ndipo walipoamua kutoka nje na kupeleka hoja zao kwa wananchi ambao ni nguvu ya umma itakayowahukumu viongozi wa CCM kama Kapunga kwa kutojadili hoja zenye maslahi ya wananchi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment