Advertisements

Saturday, October 1, 2011

jinsi ya kuyaweza mapenzi



Huko nyuma kupitia safu hii, nimewahi kuandika mada inayosema, “Mapenzi ni matamu lakini siyo rahisi”. Nilieleza kwa upana jinsi ya kukabili. Leo nimekuja na muongozo wa jinsi ya kufanya ili uyaweze mapenzi na kuushinda ugumu uliopo.


 Mada hii ina lengo la kukufanya uyaelewe mapenzi.
Si kukimbilia kuacha pale kunapotokea tofauti za hapa na pale na mwenzi wako wa maisha. Uvumilivu unahitajika, amini kwamba utamu wote unaoyazunguka ‘malavidavi’ kuna ugumu mkubwa.


Hapa tunazungumzia elimu zaidi inayoweza kukukomboa wewe kwa kuheshimu hisia za mwenzako na wakati huo huo ukawa unajali za kwako.
Kwa pamoja ndipo utaweza kufanikiwa kuwa na moyo tulivu katika nyakati zote.

Ukiheshimu hisia za mwenzi wako na ukawa unajali za kwako, itakusaidia kukufanya uwe na tumaini chanya wakati wote.
Wakati wa matatizo, hasa kipindi ambacho hampo kwenye maelewano mazuri, utabaki na imani kwamba yote yatakwisha.

Penda kuamini kuwa “hili nalo litapita” kwamba wakati ambao mwenzi wako amenuna, hataki kuzungumza na wewe, unachopaswa kufanya ni kuheshimu hisia zake na uamini kwamba mwisho atatulia na uhusiano wenu utaendelea kwa maelewano makubwa.

Ukitaka kulazimisha awe mchangamfu kwako kipindi ambacho amenuna, ni sawa na kukaribisha matatizo zaidi. Ni vema kuelewana, watu wengi wanakosea katika uhusiano wao kwa sababu hawatumii busara ili kuwaelewa wenzi wao pindi wanapoonesha hali tofauti.

Busara iendelee kuchukua nafasi.
Maneno “hili nalo litapita” liwe somo kwako.
Kwamba leo umerudi nyumbani, umetaka chakula cha faragha, mwenzako amekwambia hajisikii vizuri. Hutakiwi kupandisha mizuka na kusababisha nyumbani pasilalike kwa siku hiyo.

Badala yake unapaswa kuvumilia. Jiulize mmefanya tendo mara ngani katika uhusiano wenu, iweje siku hiyo akwambie hajisikii? Ukilazimisha ni sawa na kumfanyia mwenzako ubakaji.
Si ajabu akikuona unakuwa mkali, akakubali kukupa kwa shingo upande lakini si kwa ridhaa yake.

Mapenzi ni matamu lakini siyo rahisi kwa maana, nyakati nyingine utalazimika kuvumilia mambo ambayo pengine yatakuumiza.
Mko wawili na kujenga tafsiri ya mwili mmoja.
Pengine hata makundi yenu ya damu ni tofauti. Ilivyo maumbile yenu ni hasi na chanya ndiyo na damu zenu zilivyo.

Tofauti hiyo mnaielewa na kuikubali, iweje siku ukirudi nyumbani unamkuta amenuna na hataki kuzungumza na wewe ushindwe kuelewa? Hapo ndipo uvumilivu wako unahitajika.
Ni kipindi ambacho busara zako zinapaswa kufanya kazi kwa asilimia 100. Usilazimishe afanye upendavyo wakati mwili wake haupo tayari.

Unaingia faragha na mwenzi wako. Ameshindwa kukuridhisha kabisa.
Ni hekima zako kutambua kwamba siku hazilingani. Mbona siku nyingine alikupa mambo mazuri mpaka ukasema ‘poo’? Tatizo ni nini? Pengine nishati za mwili wake kwa siku hiyo hazipo sawasawa na hata yeye mwenyewe hajui.

Ukimkejeli kuwa hajiwezi ni sawa na kumchinjia baharini.
Siku zinazokuja atashindwa kabisa.
Si kwa sababu uwezo wake ni mdogo, la hasha! Maneno yako ya kejeli na dharau ndiyo yatakayoufanya moyo wake usinyae na kukuogopa ndani kwa ndani.
Fikra zake zitashambuliwa na ugonjwa hatari.

Si ugonjwa unaosababishwa na kirusi, hapana.
Ni gonjwa la maneno litakaloshambulia ubongo wake. Kila mara kabla ya kuingia kwenye mchezo atakuwa na maswali ya kujiuliza. “Sijui leo nitashindwa tena?” “Nikishindwa itakuwaje?” “Atanitukana tena?” “Hivi mimi ni mgonjwa?”

Mwisho wa maswali hayo atahitimisha kauli kwa kusema: “Inawezekana mimi ni mgonjwa kweli ndiyo maana nashindwa kazi.” Amini kuwa kauli hiyo ndiyo ugonjwa hatari ambao utashambulia hisia zake na kuusababisha mwili ushindwe kufanya kazi sawasawa.

Ukitaka kuendelea kufurahia mapenzi ni vizuri umpe moyo mwenzi wako pale inapoonekana ameshindwa kutekeleza kazi ya faragha inavyotakiwa.
Kaa naye vizuri na umueleze kwa lugha laini kwamba baadaye au siku inayofuata mtafanya tena kikamilifu na hakutakuwa na kushindwa.

Ikibidi msifie, mwambie kuwa yupo kamili kwa sababu kila siku mnapoingia kazini huwa unatosheka. Mueleze kuwa siku hiyo anasumbuliwa na uchovu au hajisikii vizuri.
Maneno hayo utayaona madogo lakini yatamjenga ipasavyo. Yatamrejeshea ari na afya, kwa hiyo siku nyingine hatakuogopa.

Mapenzi ni matamu lakini siyo rahisi.

Hii imesababisha watu wengi kushindwa kushirikiana vema na wenzi wao.
Jambo dogo la kumuelewesha mwenzake linakuwa tatizo mpaka uhusiano unageuka shubiri.
Wawili walioitana majina matamu na yenye kupendeza, wanageuka maadui.

Wanatangaziana sifa mbaya. “Yule muoneni hivyo hivyo kwa nje, hajiwezi kabisa kitandani.” Ni maneno ambayo si mageni.
Yanasababishwa na watu kutotambua thamani ya mapenzi, ugumu uliopo ili iwe rahisi kwao kupata alama A kwenye uhusiano wao.
Mapenzi ni magumu lakini ni rahisi sana.
Kanuni ni moja tu, kuwa mwelewa.
Unaona mwenzi wako anashindwa kukufikisha unapopataka, wewe una jukumu la kumwelewesha. Mfahamishe maeneo ambayo anatakiwa ayafanyie kazi ili ufurahie tendo.
Amini kuwa ukifanya hivyo, itakuwa rahisi kwako. Mapenzi ni matamu kama utayajua na kuyaweza.

Kuna maswali ya kujiuliza kuhusu mapenzi.Hayo ndiyo yatakuwezesha kutambua kama unatosha kuendelea na mwenzi wako au kinyume chake. Yatakusaidia kufurahia maisha yako ya kimapenzi.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info

No comments: