ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 19, 2011

KESI ZA UCHAGUZI MKUU:CUF wabwagwa, Chadema, CCM wakwama

Abdallah Bakari, Mtwara na
Frederick Katulanda, Mwanza
WANAODAIWA kuwa wafuasi wa CUF wamefanya vurugu mahakamani, kuvamia maduka na kuiba mali na kutaka kuichoma moto nyumba ya Mwenyekiti CCM Mkoa wa Mtwara, kwa kile kilichoelezwa kuwa kutoridhishwa na hukumu ya Mahakama Kuu iliyompa ushindi Mbunge wa CCM, Asnain Murji, dhidi ya mpinzani wake, Hassan Uledi wa CUF.

Uledi alifungua kesi mahakamani hapo kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana Jimbo la Mtwara Mjini, yaliyompa ushindi Murji wa CCM. Baada ya kusikilizwa kwa takriban mwaka mmoja, kesi hiyo jana ilitolewa hukumu na kumhalalisha Murji.Muda mfupi baada ya kutolewa hukumu hiyo jana, wafuasi wanaodaiwa kuwa wa CUF walijikusanya kuelekea ofisi ya chama hicho wakiwa njiani, inadaiwa waliishambulia nyumba ya kada huyo wa CCM iliyopo karibu na ofisi hiyo kwa kurusha mawe.



Tukio hilo lilifuatia na kitendo cha wafuasi hao kwenda dukani kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara, Dadi Mbullu, ambako walipora mali na kumwaga dizeli kwenye kuta za nyumba hiyo kwa lengo la kuichoma moto.
Hata hivyo, wafuasi hao hawakufanikiwa kuchoma moto nyumba hiyo baada ya polisi kuwasili dakika chache baadaye na kuwatawanya kwa risasi za mpira.



Mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo ambaye hakutaka kutajwa, alisema wafuasi hao wa CUF, walianza kwa kurusha mawe dukani humo jambo ambalo lilimfanya muuzaji kukimbia, hali iliyotoa upenyo wa kuingia ndani na kupora mali.
“Walianza kwa kurusha mawe, muuzaji akakimbia ndipo walipoingia dukani na kupora bidhaa mbalimbali. Wengine walikuwa na madumu ya mafuta… polisi ndiyo waliowatawanya kwa kupiga risasi hewani,” alisema.

Vurugu hizo zilisababisha maduka yaliyopo karibu na eneo hilo likiwamo duka la Murji kufungwa kwa hofu ya kuporwa. Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya magari ya polisi waliobeba silaha za moto, yalikuwa  yakizunguka na kusababisha hofu kwa wananchi.
Wakati tukio hilo linatokea, Mbullu hakuwapo nyumbani kwake na taarifa zinasema alikuwa safarini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.
Jithada za kuwapata viongozi wa CUF wa Mtwara mjini kuzungumzia tukio hilo hazikuzaa matunda, baada ya simu zao kutopatikana na hata mwandishi wa habari hizi alipofika ofisini kwao zilikuwa zimefungwa.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara, Masoud Mbengula, alieleza kusikitishwa kwake na tukio hilo na kutupa lawama kwa polisi kwa kutozifanyia kazi kwa umakini taarifa ambazo chama hicho kiliripoti mapema.

“Nawalaumu polisi katika hili, sisi (CCM) tuliripoti juu ya kuwapo kwa vurugu iwapo wangeshindwa kesi hii siku mbili kabla…walikuwa wakihamasishana kwenda kwa wingi mahakamani na kuwa tayari kwa lolote iwapo watashindwa,” alisema Mbengule na kuongeza:
“Hizi si siasa, huu ni uhalifu ambao unapaswa kupingwa kama uhalifu mwingine …wameiba mali za dukani, wamemwagia mafuta ukuta kwa lengo la kuchoma moto unawezaje kuita hizo ni siasa?"

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuki, alisema asingeweza kuzungumzia tukio hilo kwa sababu alikuwa safarini Dar es Salaam.Awali, akisoma hukumu hiyo iliyochukua saa moja na nusu, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Seleman Kihiyo, alisema mlalamikaji ameshindwa kuthibitisha madai yake, hivyo ameamua kutupilia mbali ombi lake la kutaka kutengua matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 31, mwaka jana na kumpatia ushindi Murji.

Miongoni mwa hoja ambazo mlalamikaji aliwasilisha Mahakamani hapo ni madai kuwa, walinyimwa haki ya kuhesabu kura, kucheleweshwa kutangazwa kwa matokeo na baadhi ya fomu za matokeo kutosomeka vizuri.

Jaji Kihiyo alisema madai hayo yote yameshindwa kuthibitika mbele ya mahakama, hivyo ameamua kulitupilia mbali shauri hilo na kuamuru mlalamikaji kumlipa mlalamikiwa gharama zote za uendeshaji kesi na kwamba, anaweza kukata rufaa iwapo hajaridhishwa na uamuzi huo.

Umati wa watu ulihudhuria mahakamani hapo, kusikiliza kesi hiyo yenye mashahidi watatu, wawili wakiwa wa upande wa mlalamikaji na mmoja upande wa mlalamikiwa. Hata hivyo, hawakupata fursa nzuri ya kusikiliza hukumu hiyo kutokana na kukatika kwa mawasiliano ya vipaza sauti vilivyofungwa nje.
Wakati hayo yakiendelea mkoani Mtwara, kesi namba 12/2010 ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa Jimbo la Ilemela jana ilishindwa kuanza kusikilizwa baada ya mashahidi wawili kushindwa kufika mahakamani.

Wakili wa Mbunge Highness Kiwia (Chadema), Tundu Lisu, alisema jana baada ya kuahirishwa kesi hiyo kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na kukosekana kwa mashahidi wa upande wa walalamikaji.

Alisema kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Oktoba 21, mwaka huu.
Msajili wa Mahakama Isaya Arufani, alieleza kuwa kesi hiyo imeahirishwa hadi Ijumaa itakapoanza kusikilizwa na Jaji Gadi Mjemas.Katika kesi hiyo, walalamikaji wanaopinga matokeo ya uchaguzi ni wakazi watatu wa Ilemela, Yusuf  Lupilya, Nuru Nsubugu na Beatus Madenge.

Washitakiwa ni Kiwia, Msimamizi wa Uchaguzi ambaye ni Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Willson Kabwe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).Katika matokeo hayo yanayopingwa mahakamani, Kiwia alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 31,269 dhidi ya mpinzani wake, Anthony Diallo wa CCM aliyepata kura 26,270.


Mwananchi

No comments: