ANGALIA LIVE NEWS
Wednesday, October 19, 2011
Profesa Mahalu: Serikali inanihujumu
James Magai
BALOZI wa zamani wa Tanzania Italia, Profesa Dk Costa Mahalu amedai kuwa shahidi wa tano wa upande wa mashtaka, alichomoa viambatanisho katika barua yake.Profesa Mahalu alitoa kauli hiyo jana wakati akijitetea kuhusiana na kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili pamoja na aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Barua hiyo ni ile aliyomwandikia Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kuhusu mchakato wa ununuzi wa jengo la ubalozi huo, Rome.
Barua hiyo ya Februari 20, 2002 ilitolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka kupitia kwa shahidi wake wa tano ili iwe kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo.
Akiongozwa na wakili wake, Mabere Marando jana, Profesa Mahalu alidai kuwa katika barua hiyo aliambatanisha taarifa tatu za uthamini wa jengo hilo kila taarifa ikionyesha thamani yake.
Alidai kwamba kwa mujibu wa taarifa hizo, ya kwake iliyokuwa kwa niaba ya ubalozi huo ndiyo iliyoonyesha gharama ya chini kuliko taarifa ya Wizara ya Ujenzi na ya mmiliki wa jengo hilo, Fernando Morelli.
Taarifa ya uthamini uliofanywa na Ofisa wa Wizara ya Ujenzi, Thomas Kimweri na ya mmiliki wa jengo hilo zilionyesha kuwa jengo hilo lina thamani ya zaidi ya Dola za Marekani 3milioni.
Hata hivyo, Profesa Mahalu katika taarifa yake ya uthamini alionyesha kuwa jengo hilo lina thamani ya Dola za Marekani 2.78milioni na bei hiyo ndiyo ambayo hata mmiliki wa jengo alikubali kuuuzia ubalozi huo wa Tanzania.
Profesa Mahalu jana aliiambia mahakama kuwa barua hiyo iliyokuwapo, haijakamilika kwa kuwa wakati alipoiandika, aliiambatanisha na vielelezo hivyo, lakini ilipowasilishwa mahakamani hapo na shahidi huyo wa upande wa mashtaka, haikuwa na vielelezo hivyo.
Alidai kuwa alijaribu kuomba nakala halisi za vielelezo hivyo kutoka serikalini lakini alinyimwa huku akidai kuwa ni kutokana na chuki binafsi dhidi yake kwa kuwa ni mshtakiwa.
Kutokanana kitendo hicho cha upande wa mashtaka kumnyima nakala hizo halisi za vielelezo, aliiomba mahakama imruhusu awasilishe vivuli vyake.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Ponsiano Lukosi aliiomba Mahakama iwape muda kuvipitia vielelezo hivyo kwa umakini ili kujiridhisha na mahakama ilikubali ombi hilo na kuamuru nakala hizo ziwasilishwe leo kama hakutakuwa na pingamizi.
Katika barua hiyo, Profesa Mahalu alieleza kuwa malipo ya jengo hilo ni Dola za Marekani 2,788,862.24 sawa na Sh2,534,770,448.80 kwa wakati huo na kwamba matayarisho yote yanayohusiana na ununuzi wa jengo hilo yameshakamilika.
Alieleza kuwa ikiwa malipo yatakamilia, ubalozi ungeweza kuhamia mara moja kwa kuwa jengo hilo lilikuwa halihitaji matengenezo yoyote ya msingi.
Hivyo aliiomba Wizara ya Fedha iipatie Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa sehemu ya fedha zilizokuwa zimesalia kwa utaratibu wa kuomba bajeti ya nyongeza bungeni Aprili, 2002.
Alisema fedha hizo pia zilikuwa ni kwa ajili ya kuwalipa mawakili na wathamini waliohusika katika mchakato mzima wa ununuzi huo.
Pia aliomba apewe kibali na hati maalumu ya Kisheria (Power of Attorney) ili kumruhusu kutia saini mikataba husika ya ununuzi na umilikaji wa jengo hilo kwa niaba ya Serikali, kama sheria inavyotaka.
Nakala za barua hiyo pia zilipelekwa kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu Kiongozi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Kamishna wa Bajeti.
Katika kesi hiyo, Profesa Mahalu na mwenzake Martin wanadaiwa kuhujumu uchumi kwa kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60, kupitia mchakato wa ununuzi wa jengo la ubalozi huo, wakati wakiwa utumishi wa umma.
Wanadaiwa kula njama na kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti na katika maeneo tofauti huko nchini Italia, likiwamo la kumpotosha mwajiri wao katika hati ya matumizi.
Wanadaiwa kuwa Septemba 23, 2002 jijini Rome, washtakiwa wakiwa waajiriwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walisaini vocha yenye namba D2/9/23/9/02 ikionyesha kuwa bei ya ununuzi wa jengo la ubalozi ni Euro 3,098,741.58.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, maelezo hayo yalikuwa ni ya uongo na yenye nia ya kumdanganya mwajiri wao.Mbali na utetezi wao watuhumiwa hao, pia mashahidi kadhaa wanatarajiwa kutoa utetezi dhidi yao akiwamo Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa ambaye ununuzi wa jengo hilo ulifanyika wakati wa utawala wake.
Mkapa ameridhia kutoa ushahidi huo na tayari ameshawasilisha hati yake ya kiapo itakayotumika kama ushahidi huku akieleza katika hati yake ya kiapo kuwa yuko tayari hata kufika mahakamani kutoa ushahidi.
Katika hati hiyo ya kiapo Mkapa anakiri kuwa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo ulifanyika wakati wa uongozi wake na kwamba alikuwa akijua kila kilichokuwa kikiendelea kuhusiana na ununuzi huo na kwamba ulifanyika kwa mujibu wa sheria.
Aliongeza kuwa Serikali yake ilimpa Profesa Mahalu mamlaka yote ya kusimamia na kutekeleza mchakato wa ununuzi wa jengo hilo kupitia nguvu ya kisheria aliyopewa na Serikali yake.
Mkapa alisisitiza kuwa kupitia utaratibu wa Serikali alikuwa akijua kuwa taarifa ya uthamini wa jengo hilo iliyofanywa na Wizara ya Ujenzi ilikuwa ni Dola za Marekani 3.0 milioni wakati Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ilikadiriwa Euro 5.5 milioni.
Pia Mkapa alisisitiza kuwa alikuwa bado anatambua taarifa ya Serikali bungeni ya Agosti 3, 2004 iliyoeleza na kuthibitisha kuwa taratibu zote za ununuzi wa jengo hilo zilifuatwa kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali na kwamba dalali alilipwa kikamilifu.
“Kwa kipindi chote ambacho nimefanya kazi na Balozi Mahalu katika nafasi mbalimbali za utumishi wa Serikali, ameonyesha tabia thabiti na za dhati, uaminifu, utiifu, uchapakazi na ubora,” alisema Mkapa.
Alisema kuwa sifa hizo zilimfanya atunukiwe na Rais wa Italia, Tuzo ya Heshima ya Juu wakati wa kuadhimisha siku ya taifa hilo, muda mrefu baada ya kuwa ameondoka nchini humo.
Mashahidi wengine wanaotarajiwa ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Hata hivyo, Rais Kikwete bado hajatoa ukubali wake kutoa kama Mkapa.
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment