ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 19, 2011

Lowassa kutoa ya moyoni leo



Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa
MILLYA ACHAFUA HALI YA HEWA CCM, ASEMA MAISHA YAKE YAKO HATARINI  
Waandishi Wetu
WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa leo anatarajiwa kuzungumza na vyombo vya habari katika mkutano ambao utazungumzia mambo makuu matatu likiwamo suala la Kampuni ya kufua umeme ya Richmond ambalo lilisababisha ajiuzulu wadhifa huo, Februari 2007.  Mkutano huo wa Lowassa unafanyika sikumoja tangu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Arusha, James Millya atoe matamshi makali akiwatuhumu aliowaita watoto wa vigogo kwamba wanavuruga umoja huo huku akilalamika kwamba: “Maisha yake yapo hatarini.”  Habari zilizopatikana jana kupitia kwa watu walio karibu na Lowassa zinasema, katika mkutano huo, Mbunge huyo wa Monduli (CCM), pia atazungumzia taarifa zinazomhusu ambazo zimekuwa zikichapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari nchini.


 Suala jingine ambalo linatarajiwa kuzungumzwa na kiongozi huyo ni kuhusu mgogoro ndani ya CCM mkoani Arusha, ambao unatokana na mgawanyiko miongoni mwa makada na viongozi wa chama hicho.  “Pia anasema kwamba ataanzia pale alipoishia, siku ile alipozungumza bungeni kuhusu Serikali kufanya uamuzi mgumu lakini hakutakuwa na kumshambulia mtu,” alisema mmoja wa watu hao na kuongeza:

 “Anasema (Lowassa) kwamba lazima aweke kumbukumbu sahihi kwa baadhi ya mambo ambayo yametamkwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa na viongozi wengine kwani amebaini kuwa uongo ukisemwa sana na kwa muda mrefu hugeuka kuwa ukweli.”
Hii ni mara ya kwanza kwa Lowassa kuitisha mkutano wa vyombo vya habari tangu alipojiuzulu kuzungumzia sakata la Richmond ambalo halikuwahi kupata hitimisho la kisiasa wala kisheria.

Lowassa pamoja na mawaziri wawili waliowahi kuwa na dhamana katika Wizara ya Nishati na Madini kwa vipindi tofauti, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha walijiuzulu nyadhifa zao kwa kuwajibika, baada ya matokeo ya uchunguzi wa Kamati Teule ya Bunge la Tisa, iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Ujenzi.

Uchunguzi huo ulihusu kampuni tata ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, ambayo ilishindwa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa mkataba baina yake na Tanesco, hivyo kuhamishia majukumu yake kwa kampuni Dowans.

Mkutano wa Millya
Mkutano wa Lowassa unafanyika katika kipindi ambacho CCM kinakabiliwa na misukosuko ambayo imedhihirisha kuwapo kwa mpasuko mkubwa huku kukiwa na tofauti za wazi miongoni mwa makada na viongozi wake ambao katika siku za karibuni wamekuwa wakirushiana maneno nje ya vikao rasmi vya chama.
 Jana, Millya naye aliingia katika malumbano hayo pale alipowaambia waandishi wa habari kwamba: “Watoto wa viongozi wa CCM na Serikali wamejitwika madaraka ya wazazi wao kinyume cha sheria za nchi.”

“Ninaomba kuwaonya watoto wa vigogo wenye tabia ya kuingilia mambo ya UVCCM na uendeshaji wa nchi kwamba hatutaruhusu na hatutavumilia watumie mamlaka tuliyowapa wazazi wao ili kutuvurugia jumuiya yetu,” alisema Millya na kuongeza:

 “Haki hufuatana na wajibu lakini amani huletwa na haki. Niwaombe viongozi wetu wasikubali kutumia mamlaka kunyima watu haki zao kwani kwa kufanya hivyo ni kuhatarisha amani na utulivu wa muda mrefu wa nchi yetu.” Millya alitoa kauli hizo akitokea polisi kuhojiwa kutokana na matamshi yake ya Oktoba 10, mwaka huu katika mkutano wa hadhara kwamba polisi walizuia maandamano ya UVCCM kutekeleza shinikizo la mtoto wa kigogo mmoja.
Akizungumzia kuhojiwa huko, Millya alisema: “Ni muhimu sana mfahamu kwamba sijayumba na sitayumba kwani tuna safari ndefu ya kujenga demokrasia ya kweli na Uhuru wa kweli wa mawazo na maoni.”

“Uhuru wa utashi wa kisiasa, Uhuru wa kusimamia misingi na kanuni za chama chetu, jumuiya yetu (UVCCM) bila woga, wala kuyumbishwa na mtu yeyote hata akijaribu kutumia vyombo vya dola au taasisi binafsi ili nitoke kwenye hoja ya msingi ya kuhakikisha Tanzania huru inawezekana.”
Alisema mkoa wa Arusha na Kanda ya Kaskazini wanahujumiwa na kikundi kidogo cha watu wenye uchu wa madaraka na wenye lengo la kulinda maslahi yao binafsi ya sasa na ya baadaye.

Alitoa mfano wa tamko lililotolewa na Baraza la UVCCM Mkoa wa Pwani kwamba Rais wa 2015, kamwe hawezi kutokea Kanda ya Kaskazini kuwa ni uthibitisho kwamba  vijana hao walitumiwa.

“Mbali na kwamba hili ni tusi kwa watu wa kaskazini wenye haki yao kikatiba kuwania nafasi ya uongozi wa juu wa nchi yetu, ni tusi pia kwa wapiga kura wa Tanzania wanaoamini katika demokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa,” alisema.
Alisema cha kushangaza mpake leo hakuna chombo chochote cha Serikali ambacho kimewahi kutoa tamko la kukanusha taarifa hiyo iliyounganishwa na taasisi moja ya juu serikalini.

Millya alisema kwa hali falsafa ya kujivua gamba yenye waasisi wake, ni mbinu madhubuti na endelevu za kuwapunguza nguvu baadhi ya watu wenye ushawishi mkubwa ndani ya CCM ili kuwazuia kugombea urais 2015.Alidai kuwa hivi sasa maisha yake yapo hatarini kutokana na kutumiwa ujumbe wa vitisho kupitia simu yake ya mkononi na kwamba ametoa taarifa polisi kuhusu suala hilo.

Kama walivyofanya, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangoro na Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Benno Malisa, Millya naye alimtuhumu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kwamba ndiye chanzo cha mitafaruku yote ndani ya CCM.

Hata hivyo, Nape alipoulizwa kwa simu Jumamosi iliyopita kuhusu shutuma nyingi kuelekezwa kwake alisema: “Sijui kwa nini haya mageuzi ya kujivua gamba yanapotajwa yanahusishwa na urais, hili si sahihi hata kidogo.”  Nape alikuwa akijibu tuhuma Ole Nangoro ambaye alimshambulia hadharani, akikosoa utekelezaji wa falsafa ya kujivua gamba inayosimamiwa na Sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu, Wilson Mukama.

Kujivua gamba Falsafa ya kujivua gamba ni moja ya maazimio 24 yaliyopitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ikiwataka watuhumiwa wa ufisadi kupima kisha kuachia nafasi zao za uongozi ndani ya chama.

Mmoja wa watuhumiwa hao, Rostam Aziz alishajivua nyadhifa zake ambazo ni ujumbe wa NEC na ubunge wa Igunga ambalo CCM ilifanikiwa kulirejesha kupitia kwa Dk Dalaly Kafumu katika uchaguzi mdogo uliomalizika hivi karibuni.

Habari kutoka ndani ya CCM zinasema taarifa ya utekelezaji wa maazimio 24 ya NEC likiwamo la kujivua gamba, inaandaliwa ili iwasilishwe kwenye kikao cha NEC ambacho kinaweza kufanyika mwishoni mwa mwezi huu au mapema mwezi ujao, kikitanguliwa na Kamati Kuu (CC).  Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Dar na Peter Saramba, Arusha


Mwananchi

1 comment:

Buckinghamshire said...

Hovyoooo! Unafiki, wizi na tamaa ndio vinaendesha siasa ya TZ. Upuuzi mtupu.