ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 14, 2011

Mwanafunzi ajiua kwa kukosa mtihani kwa sababu ya mimba


Mwanafunzi wa kidato nne, Tumaini Mussa (22), wa Shule ya Sekondari Matyazo, mkoani humu, amejiua kwa kujinyonga kwa kamba ya katani baada ya kutofanya mtihani wa Taifa kutokana na ujauzito.
Mwili wa mwanafunzi huyo ulikutwa ukining'nia  katika Kijiji cha Nyamnyusi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 11, mwaka huu saa 9:00 alasiri katika Kijiji cha Nyamnyusi Kata ya Nyamnyusi Tarafa ya Nyakitonto Wilaya ya Kasulu.

Kamanda Kashai alisema sababu za mwanafunzi huyo kujinyonga ni kuwa mjamzito na hivyo kushindwa kufanya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka huu.

Alisema wiki mbili kabla ya kuanza mtihani wa kidato cha nne, mwanafunzi huyo alijaribu kutoa mimba hiyo lakini ilishindikana, hali iliyosababisha alazwe katika hospitali ya Misheni ya Heri iliyopo wilayani Kasulu.


Alisema kulazwa huko kulimkosesha kufanya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne.

Wakati huo huo, watu wanne wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wakiwa na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG), wamevamia nyumba ya mganga wa kienyeji na kumuua mgonjwa aliyekuwa akitibiwa.

Majambazi hayo yalivamia nyumba ya  Baharaye  Jamal, ambaye ni mganga wa kienyeji  na kumuua kwa kumpiga risasi, Zawadi Obeid (22), mkazi wa Kijiji cha Kanyamahela.

Kamanda Kashai alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 6:00 usiku katika Kijiji cha Kigaga mkoani humu.

Alisema baada ya kumuua mgonjwa huyo, majambazi hayo yalimpora mganga huyo wa jadi Shilingi milioni nne.

Kamanda Kashai alisema hadi sasa hakuna anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo na polisi wanaendelea kuwasaka majambazi hayo yanayodaiwa kuwa yalitokea nchi jirani ya Burundi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: