ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 23, 2011

Hakimu akataa kutoa hati kukamatwa Mbowe, Lissu



Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha amekataa ombi lilililotolewa na wakili wa Serikali, Haruna Matagane, la kutaka Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, wakamatwe kutokana na kutofika mahakamani jana.
Hakimu Devotha Msofe alikataa ombi hilo jana kutokana na taarifa aliyoitoa Wakili wa utetezi, Method Kimomogolo, kuwa Mbowe na Lissu wameshindwa kuhudhuria mahakamani hapo kutokana na ndege yao kubadilishwa ratiba ghafla, lakini walikuwa njiani kwenda Arusha kusikiliza kesi hiyo na pia walikuwa na mkutano wa chama hicho ambao uliisha usiku wa manane.

Kimomogolo alimweleza Hakimu Msofe kuwa: “Washtakiwa hao wameshindwa kufika mahakamani kutokana na ndege yao kubadilishwa ratiba, hivyo kama Wakili wa serikali anataka tuwasubiri hadi hapo watakapofika mahakamani muda si mrefu, tupatie ruhusa yako ili tuweze kuwasubiri.”
Baada ya kutoa taarifa hiyo, Wakili wa serikali Haruna Matagane, alidai kuwa haiwezekani Lissu na Mbowe wamedharau mahakama, hivyo alisisitiza kuwa mahakama itoe hati kwa washtakiwa hao kukamatwa kwa sababu ya dharau zao.
Matagane pia alidai kuwa upelelezi umeshakamilika na anaomba usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo ufanyike.
“Mheshimiwa Hakimu, naomba mahakama hii itoe hati ya kukamatwa kwa washtakiwa hawa wawili, kwani wanadharau mahakama kwa sababu kama kikao cha chama wangefanya siku mbili kabla ya kesi, ila kufanya jana huku wakijua kuna kesi kesho yake ni dharau za makusudi, pia upande wa Jamuhuri tunaomba tarehe ya usikilizwaji wa kesi hii, kwa sababu upelelezi wa kesi hii tayari umeshakamilika,” alidai.
“Pia kama huyu wakili Kimomogolo ameona kuwa washitakiwa wamechelewa ndege, ameshindwa kutupa hata kielelezo chochote kuonyesha kama anayosema yana ukweli,” alidai.
Baada ya Hakimu Msofe kusikiliza hoja za pande zote, alisema hawezi kutoa amri ya kukamatwa kwa Lissu na Mbowe, kwani yeye jukumu lake lilikuwa la kuahirisha kesi hiyo na angekuwepo
Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Judith Kamuzora, tangu awali angetoa uamuzi wa kukamatwa kwa washtakiwa hao kama angeona inafaa.
“Mimi siwezi kutoa hati ya kukamatwa kwa sababu Wakili Kimomogolo ambaye anawawakilisha washitakiwa ametoa sababu ya kutofika kwao, hivyo hakuna haja ya kufanya hivyo, pia mimi kazi yangu kubwa leo (jana) ni kuahirisha kesi na itakuja tena kwa kutajwa Desemba 20, mwaka huu,” alisema.
Katika kesi hiyo, washitakiwa 26 walikuwepo mahakamani hapo, pamoja na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa.
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na mashtaka matatu.
Katika shitaka la kwanza ilidaiwa kuwa, Novemba 7 na 8, mwaka huu, Dk. Slaa, Lissu na wafuasi wao 26 walifanya mkusanyiko usio halali katika eneo la NMC saa 11:00 alfajiri.
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa washitakiwa hao walikaidi amri ya polisi ya kuwataka watawanyike.
Katika shitaka la tatu, Dk. Slaa anadaiwa kutoa matamshi ya uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete na OCD wa Arusha, Zuberi Mwombeji.
Katika shitaka la nne, inadaiwa kuwa Mbowe alifanya mkusanyiko usio halali kwenye viwanja vya NMC na alidaiwa kukimbia wakati wenzake walipokamatwa. Hata hivyo, baadaye Mbowe aliunganishwa kwenye kesi hiyo.
Washitakiwa wote wanadaiwa kufanya mkusanyiko huo kwa ajili ya kushinikiza kutolewa mahabusu kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ambaye awali alikataa dhamama na kwenda mahabusu ya gereza la Kisongo kabla ya Mbowe kumsihi akubali dhamana, lakini Hakimu aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo alikataa kutoa hati ya Lema kutoka mahabusu akitaka asubiri hadi siku iliyokuwa imepangwa awali ya kutajwa kwa kesi hiyo ambayo ilikuwa ni Novemba 14, mwaka huu. Lema alikaa mahabusu kwa wiki mbili.
CHANZO: NIPASHE

No comments: