WIKI iliyopita tulianza kujadili mada ya kuyafanya mapenzi yachanue kwa kuishi ndani ya mwenzi wako. Leo tunaendelea na mada yetu kuanzia pale tulipoishia. Twende pamoja.
Kusema ukweli, hao marafiki wamenikosha kiasi ambacho naona thamani yao ni kubwa kuliko Jamie.
Kusema ukweli, hao marafiki wamenikosha kiasi ambacho naona thamani yao ni kubwa kuliko Jamie.
“Vile vilio vya kimahaba, sauti za kubembeleza na pongezi baada ya kazi ni kitu kikubwa kwangu. Hata kama ni sifa za uongo lakini mimi zinanipeleka pale ninapotaka. Sijisikii kwenda faragha na mtu ambaye najitahidi kumfurahisha na kumridhisha lakini yeye ananitolea macho utadhani hana hisia. Najisikia kumchoka!”
Inawezekana mwenzi wako hakwambii lakini ukweli usimame kwenye kipimo chake kwamba anahitaji manjonjo yako ili afurahie penzi tatizo unabana. Kauli ya Justin kama nilivyomnukuu kwenye makala haya toleo lililopita, inaweza kuwa fundisho kwako kwa sababu wengi wamejikuta wakipoteza mvuto wao, kisa ni vitu vidogo.
Hii ndiyo sababu ya kumtaka kila mmoja kuzingatia yale ambayo mwenzi wake atakuwa anapenda na kutekeleza kwa kiwango bora ili kumridhisha. Sanaa ya mapenzi kama ambavyo nimekuwa nikipigania kuisambaza siku zote, inamtaka mtu kuishi ndani ya mwenzake. Kuugua kwa maumivu, kuhuzunika katika majonzi na kufurahia palipo na sherehe.
Ni kituko mwenzi wako anaumia wewe unacheka. Yupo kwenye maumivu makali, wakati huo kwa upande wako ni chereko kwa kwenda mbele. Aina hii ya maisha haiwezi kuwa sawa na haikubaliki. Unapaswa kumjali mpenzi wako hata kama haikugusi lakini machoni muoneshe kuwa upo pamoja naye, vinginevyo ni mateso kwako.
Katika mapenzi, ogopa wewe na mwenzi wako kutofautiana kihisia. Falsafa ya mapenzi haifundishi ugumu wala haielekezi ubinafsi, inatoa muongozo katika wawili kuwa kitu kimoja. Hii inamaana kuwa unapolazimisha kwenda kinyume na mwenzako, unakuwa unaonesha kiwango cha chini cha ufahamu katika mambo ya ‘malavi davi’.
ANGALIA USIPITWE NA WAKATI
Kwa kawaida, mtu ambaye ni mjanja wa mapenzi anabaki kuwa namba moja katika kuhakikisha hapitwi na wakati. Ikiwa hujali hisia za mwenzi wako, wewe utaonekana wale wale. Badilika leo na uzichange karata zako vizuri, mwenzi wako anakuhitaji, anataka ukweli wako, kujali kwako, huruma yako na anapenda kusikia sifa njema zinatamkwa na kinywa chako.
Mwanasaikolojia Born Lewis wa Marekani katika makala yake “Your Sentimental and True Love” anasema: “Inakuhitaji uwe muelewa zaidi wa hisia za mwenzako ili uweze kudumu. Mfano; Msome na ujue kwamba anahitaji kusifiwa halafu umsifie. Akienda kupewa sifa na mtu wa pembeni atajua humkubali. Hilo ni kosa kubwa katika mapenzi.”
Lewis anafafanua: “Ni kosa kubwa kwenda kumpongeza mfanyakazi mwenzako kwa muonekano wake, wakati hujafanya hivyo kwa mpenzi wako nyumbani. Ukitaka kujua kwamba inauma, fikiria mwenzio amekuona ulivyovaa na hakukwambia kitu lakini unapata taarifa kuwa amemsifia jirani yenu. Itakuuma, itakupunguza imani yako kwa mwenzi wako.”
Sherry na Mosses ni wapenzi lakini hata siku moja Sherry hajawahi kuonesha kwamba anamkubali Mosses ingawa penzi lao linazidi kuvuta miaka. Ilivyo ni kwamba mara nyingi ni Mosses ndiye huonesha hisia zake kwa Sherry na hata marafiki zao hufikia kusema kwamba jamaa ndiye anayesababisha uhusiano wao uendelee kuwepo, vinginevyo wangekuwa wamekwishapigana mwereka.
Sherry anapoambiwa amependeza anajibu asante halafu imetoka. Akiambiwa yeye ni mwanamke mzuri jibu ni ‘thank you’. Hathubu kumwambia Mosses kuwa amependeza au ni mwanaume anayemvutia kuliko wote, ila akiwa kazini kwake, pongezi huzimwaga huko. “James umependeza!” Sherry anamwambia mfanyakazi mwenzake.
Wakati mwingine Sherry anakosa hekima, anamueleza Mosses: “Unajua sisi pale kazini kwetu kuna vijana wazuri. Unajua Jamal ana sura nzuri sana? Halafu Sam anajua kupigilia mavazi ukimuona hadi raha.” Inawezekana Sherry anazungumza kweli lakini kichwani kwake kuna kelele za ndani (internal noise) zinazomsababishia umapepe, hivyo kukosa busara ya kuchagua maneno mbele ya mpenzi wake.
Ukitaka kujua mkuki kwa nguruwe, siku moja Sherry alikutana na Zawadi ambaye ni mfanyakazi mwenzake Mosses. Zawadi akaamua kuwa mkweli: “Mosses nimemuacha ofisini ila kanifurahisha, amenisifia huyo. Anasema nimependeza sana leo.” Ilikuwa ni kama Zawadi kamroga Mosses kwani Sherry alikasirika mno siku hiyo.
Walipokutana nyumbani, Sherry alitaka maelezo ni kwa nini alimsifia Zawadi kwamba amependeza badala ya sifa hizo kuzielekeza kwake. Mosses akaona mpenzi wake anampanda kichwani, akamjibu: “Mbona wewe huwa unawasifia wanaume wa kazini kwako mimi sisemi, tena mbele yangu.” Sherry ikamgonga kichwani, akapata pointi!
Itaendelea wiki ijayo.
www.global.publishers.info
No comments:
Post a Comment