Mfanyabiashara maarufu katika sekta ya ujenzi, Indertit Sigh Jandu, amekamatwa na Idara ya Uhamiaji kwa tuhuma za kuwahifadhi na kuwatumikisha wahamiaji haramu 18.
Jandu na wahamiaji hao, wote wanashikiliwa mahabusi wakisubiri kufikishwa mahakamani.
Habari kutoka eneo la kampuni ya Jandu Construction & Plumbing, inayomilikiwa na mfanyabiashara huyo, zimeeleza Jandu alionyesha jeuri akidai kuwa na uhusiano na vigogo serikalini na wanasiasa.
Alizuiwa jana alipopeleka nyaraka za wahamiaji hao haramu.
Imeelezwa kwamba, maofisa wa Uhamiaji walivamia eneo la kampuni hiyo, Buguruni, jijini Dar es Salaam juzi usiku na kukuta kundi kubwa la watu wenye asili ya India na Pakistan nje ya eneo hilo kabla ya watu hao kukimbilia ndani na kujificha.
Kati ya wahamiaji hao, mmoja Kertik Patel, alikutwa akiwa na kibali kilichotolewa kupitia kampuni ya African Pride Textile Mills, akifanya kazi katika kampuni ya Jandu.
Chanzo cha habari ndani ya kampuni hiyo kinaeleza kwamba, maofisa wa Uhamiaji walipofika, walikuta wageni zaidi ya 30, ambao walikuwa wamejificha katika vyumba mbalimbali vya eneo hilo.
Baadhi walikutwa wakiwa wanapika chakula na wengine wakiwa wamelala.
“Baada ya ukaguzi wa chumba hadi chumba na baada ya kukagua nyaraka, tulikuta baadhi yao walikuwa na vibali halali, lakini 18 walikuwa hawako kihalali. Kati yao, 17 wakiwa raia wa India na mmoja raia wa Pakistan,” alisema mmoja wa maofisa wa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam.
Sehemu kubwa ya wahamiaji hao, waliingia nchini kwa kutumia viza ya matembezi, ambayo haiwaruhusu kufanya kazi nchini, baadhi zikiwa zimekwisha muda tokea mwaka juzi na wengine zikiwa zinaisha muda mwezi huu, kinaeleza chanzo ndani ya Uhamiaji.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Jandu alipoulizwa kuhusu wahamiaji hao, alikana kuwafahamu pamoja na kukutwa katika eneo lake la kazi, kabla ya kubanwa na kukiri kuwa ni wafanyakazi wake.
Hata hivyo, Jandu alipotakiwa kupeleka nyaraka za wahamiaji hao ofisi za Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, katikati ya jiji, aliamua kutafuta njia ya kuzima sakata hilo kwa ‘wakubwa’ kama alivyonukuliwa akitamba mbele ya wafanyakazi wake wengine.
Juhudi za Jandu kutaka kuzima sakata hilo, ziligonga mwamba baada ya kukwepa Uhamiaji Mkoa huo na kwenda Makao Makuu, Kurasini, Dar es Salaam, ambako nako alitakiwa kufuata taratibu kwa kuwasilisha nyaraka alikotakiwa kwa wakati.
“Alipofika mkoani, aliwekwa chini ya ulinzi na hadi sasa anashikiliwa wakati hatua nyingine zikiendelea kuchukuliwa,” kinaendelea kueleza chanzo chetu cha habari.
Habari zaidi zinaeleza kwamba, Jandu ni mmoja wa wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia wanaoingiza wahamiaji wengi na kuwatumikisha katika kampuni zao, baadhi wakiwa katika maandalizi ya kwenda kufanya kazi Afrika Kusini.
Imeelezwa kwamba, wahamiaji wanaoletwa nchini kwenda Afrika Kusini, hutozwa hadi Dola za Marekani 10,000, ambazo kwa ajili ya kupelekwa kufanya kazi nchini humo, biashara ambayo hufanywa na wafanyabiashara wengi nchini.
Hata hivyo, wageni ambao huwa hawana fedha za kulipia gharama hizo, hufanyishwa kazi kwa muda mrefu bila malipo ya kutosha.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment