Mkuu wa Idara ya Katiba na Sheria wa Chama cha NCCR - Mageuzi, Dk. Sengondo Mvungi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jana. (Na Mpigapicha Wetu).
CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimesema kitendo cha Mbunge wa Kigoma, Kusini David Kafulila na wenzake kuweka pingamizi la Mahakama, kuzuia hatua yoyote isichukuliwe kuhusu uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Chama kumsimamisha uanachama, ni sawa na kujimaliza mwenyewe.
Pia chama hicho kimesema kufuatia amri hiyo kimefungwa mikono hivyo kinasimamisha
hatua zozote kilichoanza kuchukua katika kutafuta suluhu ya suala hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Katiba na Sheria wa chama hicho, Dk. Sengondo Mvungi, alisema hata hivyo chama hicho kimeshangazwa na agizo hilo la Mahakama Kuu ambalo limesikiliza upande mmoja wa Kafulila pekee.
“Taarifa za agizo hilo tumezisikia kupitia watu wetu waliotupigia simu na wao habari hizo walizipata kwenye mtandao, sijui walimshawishi vipi Jaji, lakini sisi hili hatutashughulika nalo tena kwa kuwa amri hii imemuweka huyo Kafulila mwenyewe pabaya bila kujijua,” alisema Dk. Mvungi.
Akifafanua kuhusu hilo, alisema mara baada ya kikao cha Desemba 17, mwaka huu kumvua uanachama Kafulila na wenzake watatu, kuwavua wanachama wengine madaraka watatu na 17 kupewa onyo kali, siku hiyo hiyo, Kafulila aliandika barua kwa Mwenyekiti wa Taifa, James Mbatia akiomba uamuzi huo urejewe.
Alinukuu barua ya Kafulila iliyosema “kutokana na uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa kuniondoa uanachama kwa unyenyekevu mkubwa naomba niwasilishe ombi kwa Halmashauri kwa misingi kuwa nimejitetea vya kutosha, nimeomba radhi kwa niliyokosea chama, Mwenyekiti na Katibu Mkuu….”
Alisema kutokana na barua hiyo, chama hicho tayari kilishaanza maandalizi ya kuandaa Mkutano wa Halmashauri hiyo, lakini baada ya amri hiyo ya Mahakama, mkutano huo itabidi
usitishwe hadi hapo kesi ya msingi itakapomaliza kusikilizwa.
“Nawaambia kwa amri hii Kafulila amekula sumu, ilikuwa halmashauri ikutane na kurejea
tena uamuzi wetu dhidi yake na wenzake, lakini kwa amri hii ya Mahakama haiwezi kukutana
na sasa tumefungwa mikono, na tunaendelea na uamuzi wetu wa kumsimamisha hatutachukua
uamuzi mwingine hadi kesi ya msingi iishe,” alisema Mwanasheria huyo maarufu.
Alisema chama hicho kinasikitishwa na hatua hiyo kwa kuwa kinafahamu kuwa uamuzi huo wa Mahakama umembomolea nyumba yake mwenyewe Kafulila huku kukiwa na ‘shetani’ anayemshauri.
“Sisi tunasema aendelee kushauriwa tutafika tu,” alisema Dk. Mvungi.
Alisema anashangazwa na wale wanaoshangilia huku akivishutumu vyombo vya habari kushabikia amri hiyo ya Mahakama na kudai kuwa uamuzi wa chama hicho kumsimamisha Kafulila, haukuwa wa kukurupuka na wala chama hicho hakikuufurahia.
“Kwa masikitiko makubwa tumezuiliwa tusimsaidie Kafulila na wenzake na tunafurahi uamuzi wetu wa kumsimamisha uanachama haujatenguliwa na Mahakama kama inavyodaiwa, tunachosubiri ni kukutana mahakamani Januari 21, mwakani,” aliongeza.
Juzi Mahakama Kuu kupitia Jaji Alis Chingwile ilitoa amri ya kusitisha kutekelezwa kwa uamuzi wa Halmashauri Kuu ya NCCR wa kumsimamisha Kafulila hadi kesi aliyoifungua itakapomalizika.
Katika kesi hiyo, mbunge huyo anasimamiwa na Wakili Daniel Welwel.
Chanzo:Habari Leo
No comments:
Post a Comment