ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 9, 2011

Miaka 50 tumeweza, tunasonga mbele

NI kweli tumethubutu, tumeweza na tunasonga mbele na kwa Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara pasi shaka nchi imepata mafanikio mengi kwenye afya, elimu, kilimo, miundombinu na sekta nyingine. 

Kwa nchi, miaka 50 ni kidogo sana japo kwa uhai wa binadamu anatakiwa kuwa mtu wa makamo mwenye maamuzi ya busara. 

Japo taifa hili limeshuhudia mabadiliko mengi ukilinganisha na wakati wa kupata uhuru, lipo tatizo katika ukuaji mdogo wa uchumi linalosababisha matatizo katika mzunguko wa fedha. 

Wakati tunapata uhuru, wito ulikuwa ni Uhuru na Kazi na wananchi pamoja na viongozi wao walijikita katika kilimo na viwanda vya mazao. 

Hivi sasa tuna Kilimo Kwanza ambapo wakulima sasa wanatumia zana za kisasa ingawa kwa kiasi kikubwa kikwazo kwao kimekuwa ni kushindwa kumudu bei za zana hizo. 

Kikubwa zaidi, kwa sasa ni wananchi kujipanga kuendeleza uchumi na kuachana na tabia ya kubeza kila kizuri kinachofanywa na Serikali kwa manufaa ya Watanzania wote. 

Watanzania tutumie vyema vyakula tunavyovipata badala ya kuuza nje chakula chote wakati wa mavuno na kusahau kujiwekea akiba, jambo ambalo muda wote limekuwa likiigharimu Serikali kununua vyakula kutoka nje yakiwamo mafuta ya kula, mchele, sukari na mazao mengine ya chakula. 

Inatupasa tufufue viwanda vyetu vya pamba, kwani tunalima pamba ya kutosha. Tuwatumie wataalamu ili wakulima walime pamba yenye viwango kwa ajili ya soko la kimataifa na la ndani. 

Tujifunze kuondokana na siasa za kubezana badala yake kila mmoja wetu achangie nini tufanye ili katika miaka 50 ijayo, uchumi wetu ukue kwa kasi na kujitosheleza kimsingi huku tukiuza bidhaa ambayo imesindikwa. 

Tunaweza kufanya yote hayo kama kila mmoja wetu atawajibika katika nafasi yake. 

Ni wazi ofisi zetu nyingi zinakabiliwa na uhafifu wa huduma na hii linakwamisha si tu maamuzi bali utekelezaji wa mambo anuai yaliyolenga kunyanyua taifa hili kutokuwa tegemezi hadi kujitegemea. 

Kuna vionjo vingi kama Watanzania tunavyotakiwa kufikiria wakati tunajiweka sawa kubadili Katiba na kuwa katika siasa za mashindano na wanachama wachache wa vyama vya siasa; ukweli huo unahitaji uongozi unaoangalia mbele kutakuwa na nini kisha kutwaa hatua za 
haraka. 

Kwa kuwa Rais Julius Nyerere alitutoa utumwani, Rais Ali Hassan Mwinyi akafungua milango ya biashara, Rais Benjamin Mkapa akakuza uchumi na kupunguza mfumuko wa bei basi ni kazi ya kizazi cha sasa kumsaidia Rais Jakaya Kikwete kulisukuma taifa mbele katika maelewano 
na masikilizano kwa ajili ya kujenga uchumi wa kati. 

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

No comments: