ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 14, 2011

Umeshindwa kabisa kuacha kujichua? – 3

MAMBO rafiki? Upo poa? Najua utakuwa mzima na pilika zinaendelea kama kawaida. Karibu kwenye uwanja wetu wa kujifunza. Bila shaka una shauku ya kutaka kujua nini kinaendelea katika ukurasa huu.
Naam! Tunaendelea na somo letu, ni mada pana ambayo kama nilivyosema awali inahitaji lugha ya kirafiki zaidi ili tuweze kwenda sawa, ujumbe ufike bila kuchafua ‘hali ya hewa’. Bila shaka tumekwenda vizuri.

Leo tunaendelea kuangalia athari zinazoweza kumpata mtu anayeendekeza mchezo huu, mwisho kabisa tutahitimisha na namna ambavyo tatizo linaweza kuisha bila dawa za hospitalini au kienyeji. Karibu darasani rafiki yangu.

MFADHAIKO
Mtu ambaye anaendekeza kazi hii, hupata mfadhaiko. Anayepata mfadhaiko, huwa mwepesi sana wa kuwa na matamanio kwa jinsia ya upande wa pili.

Si ajabu mtu mwenye mchezo huo, kutembelea akimwangalia mwanamke kuanzia Magomeni hadi Manzese! Amefadhaika. Ameshazoea kumaliza kazi nzima akiwa peke yake, kwa hiyo raha yake inabaki kuwa katika picha tu na si kitu halisi.

Macho yanakuwa juju juu, si kwa kupenda, ni kwa sababu tayari ameshaathiriwa na tatizo hilo. akitoka hapo, ujue moja kwa moja faragha, anaanza mambo yake. Kelele nyingi, kumbe yupo peke yake!

Mfadhaiko hauishii hapo, hata akiwa kwenye vyombo vya usafiri au mkusanyiko wa watu, mwathirika huweza kumaliza ‘kazi’ kwa macho tu, tena wakati mwingine bila kuwa na taarifa. Anakuja kugungua baadaye sana, kwamba kumbe kila kitu kilishafanyika bila hiyari yake.

KUSHINDWA TENDO LA KAWAIDA
Mwenye mchezo huo, pamoja na uhodari wake wa kujifurahisha akiwa peke yake, anapokutana na mwenzi wake faragha, kazi inakuwa si ya kiwango cha kuridhisha. Kuna athari nyingi ambazo hujitokeza.

Kwanza, anakosa ujasiri, hayupo tayari kuandaliwa, kumuandaa mwenzake. Kishazoea kufanya kila kitu haraka haraka, tena kwa kutumia hisia zaidi kuliko uhalisia wa tukio lenyewe.

Anakuwa goigoi, anachelewa kuwa tayari, hata akiwa tayari anafika safarini mapema zaidi. Mbaya zaidi, akifika hawezi kuanza safari nyingine. Hata kama akianza, kuna uwezekano mkubwa wa kuishia njiani.

Baadhi yao, hubaki wakiwa baada ya wahusika wao kuwagomea katikati ya safari. Zipo athari nyingi zaidi ya hizo, kutegemea na namna tatizo lilivyokomaa na aina ya jinsia.

KUFEDHEHEKA
Baada ya hayo hapo juu kujitokeza kwenye ndoa/uhusiano wa mwathirika, kinachofuata sasa inakuwa ni kufedheheka. Kwa bahati mbaya sana, unaweza kufanya siri mchezo wako, lakini athari zikawa wazi kwa mwenzako.

Hata kama hatagundua chanzo cha tatizo, lakini atagundua kwamba huna msisimko, huwezi kazi au vyovyote vile. Wengi husema kwa hisia, humaanisha kwamba hakuna wanachopata kutoka kwa wenzao, lakini mambo yakizidi kuwa hovyo, wanafunguka: “Mwenzangu kila siku unaniacha na kiu, una tatizo gani?”

Kauli hiyo rafiki yangu, inatosha kabisa kukufanya ushindwe kazi moja kwa moja. Unajua nini? Utaanza kuwaza: “Kumbe siwezi kitu...halafu mwenzangu ameshagundua. Nitafanyaje mimi? Mbona nahadhirika?”

Ndugu yangu, ikifikia hapo utakuwa unamkimbia mwenzako na kwenda chemba kumaliza biashara zako mwenyewe. Furaha ya moyo itatokea wapi? Kama ndiyo mnaishi kinyumba au mpo ndani ya ndoa ndiyo kabisaaa!
Umeona kazi hiyo?

UNATAKA KUACHA?
Hakuwa dawa kubwa sana ya kuacha mchezo huu. Najua wengi walikuwa na hamu ya kutaka kusikia, wataachaje huu mchezo. Ndugu zangu, NI RAHISI SANA, lakini usitegemee Shaluwa atakuwa na mambo mapya sana ya kukufanya uache.

Usitarajie kwamba nitakuja kuingia kwenye nafsi yako na kukuambia ACHA KUJICHUA! Ndugu zangu, nitawapa dondoo chache sana, lakini kubwa ni kwamba ATHARI nilizotaja hapo juu zinatosha kabisa kukubadilisha!

Hebu nikuulize, utakuwa na hamu ya kuendelea na haya mambo kama ndoa yako itakuwa hatarini? Nani atakubali kufedheheka? Nani atakubali kupoteza heshima yake? Bila shaka hakuna. Pitia dondoo zifuatazo;

(i) Badilisha utaratibu wa kulala, lala kifudifudi, badala ya chali (rejea maelezo yangu ya awali kuhusu chanzo cha tatizo)
(ii) Acha kuangalia mikanda ya kikubwa ukiwa peke yako.
(iii) Kaa mbali na simulizi zinazohamasisha mapenzi, mazungumzo ya aina hiyo na kampani za watu wanaopenda kusimulia mambo ya faragha.

(iv) Acha mazoea ya kujishika sehemu zako za siri.
(v) Fanya mazoezi ya viungo angalau robo saa tu kwa siku.
(vi) Juu ya yote haya, FUTA kabisa mawazo ya jambo hilo. AMUA kwa dhati ya moyo wako, tambua na ogopa athari ambazo unaweza kuzipata, kisha ACHA KABISA mchezo huo ili kulinda heshima yako na kujipa furaha ya maisha.

Kama nilivyosema, si rahisi kuandika kila kitu hapa, hivyo kama kuna kipengele hujaelewa vyema, tuwasiliane kwa mazungumzo zaidi.
Wiki ijayo nitakuja na mada nyingine, nitazungumza na wale ambao tayari wameathiriwa na tatizo hili, wameamua kuacha lakini uwezo wao faragha ni mdogo. Wiki ijayo tutaona namna ambavyo unaweza kurejesha heshima yako, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya Let’s Talk About Love na True Love vilivyopo mitaani.


No comments: