ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 6, 2011

Wiki muhimu kwa Dk. Mwakyembe


Madaktari wanaomtibu Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harisson Mwakyembe, wameanza kumfanyia tathmini ya mwisho ili kuamua kama aendelee na matibabu au arejee nchini.
Akizungumza na NIPASHE jana kutoka katika Hospitali ya Indraprasta Apollo nchini India alikolazwa, Dk. Mwakyembe, alisema madaktari hao walianza kumfanyia tathmini hiyo kuanzia jana na itakamilika leo.
Alisema baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo, madaktari wake watatoa taarifa kama amepona kabisa ili arejee nchini ama aendelee na matibabu.
Akizungumzia kuhusu maendeleo ya afya yake, Dk. Mwakyembe, alisema kuwa kimsingi inaendelea kuimarika na kwamba anachosubiri ni kupatiwa taarifa na madaktari wake kuhusu tathmini hiyo.
Aliongeza kuwa madaktari wanaomtibu wamekuwa karibu naye kwa kumpatia matibabu mazuri.

Kuondoka kwa Dk. Mwakyembe kwenda nje kupata matibabu kuliibua maswali mengi kwa wananchi, baada ya kuzuka kwa taarifa kuwa kuugua kwake kulitokana na kulishwa sumu, ambapo hadi sasa si serikali wala yeye aliyekanusha uvumi huo.
Dk. Mwakyembe alipelekwa India kupatiwa matibabu Oktoba 9, mwaka huu.
Akihojiwa na kipindi kinachorushwa na ITV cha Dakika 45, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alisema kuwa kuna uwezekano Dk. Mwakyembe amelishwa kitu kama sumu.
Sitta alisema alimwona Dk. Mwakyembe na hali aliyomkuta nayo kimsingi haikuwa nzuri kwani ngozi yake ilikuwa imeharibika na hata nywele zilikuwa zikipuputika.
KANDORO: WAOMBEENI VIONGOZI WANAOTIBIWA NJE
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, amewaomba wananchi wa mkoa huo na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuwaombea mawaziri, wabunge na viongozi wa kisiasa kutoka mkoani humo ambao ni wagonjwa na wanaoendelea na matibabu nje ya nchi ili wapone haraka na kurejea nchini kuendelea na majukumu yao ya kitaifa.
Kandoro alitoa ombi hilo wakati akifunga kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa Mbeya kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini hapa.
Alisema Profesa Mwandosya (Waziri wa Maji), Dk. Mwakyembe, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Nawab Mullah na Mbunge wa Viti Maalum mkoa (CCM), Hilda Ngoye, walistahili kuwepo katika kikao hicho, lakini bahati mbaya walikuwa wanaumwa na baadhi yao wapo nje ya nchi kwa matibabu.
Kandoro alisema kwa kuwa viongozi hao ni muhimu sana kwa maendeleo ya mkoa wa Mbeya na taifa kwa ujumla, wananchi wa ndani na nje ya mkoa kila mmoja kwa imani yake aendelee kuwaombea ili wapone haraka.
Hata hivyo, Profesa Mwandosya ambaye pia ni Mbunge wa Rungwe Mashariki, alirejea nchini Desemba Mosi, mwaka huu kutoka India alikokuwa akitibiwa ambako alikaa huko kwa takribani miezi mitano.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Mullah kwa takriban mwaka sasa amekuwa nje ya nchi kupatiwa matibabu kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo.
Mullah ambaye naye amerejea nchini Desemba 4, mwaka huu akizungumza na NIPASHE alisema alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya St Elizabert iliyopo Singapore.
Alisema kwa sasa yupo nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, ambako anapumuzika, kutokana na kuugua kwa muda mrefu, kazi za chama zimekuwa zikifanywa na Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Verena Shumbuko, ambaye pia katika vikao vya chama amekuwa akiviendesha kama Mwenyekiti wa CCM mkoa kulingana na kanuni na taratibu za CCM.
Kwaupande wake, Ngoye, akizungumza na NIPASHE kwa simu akiwa Dar es Salaam alisema anaendelea vizuri.
CHANZO: NIPASHE

No comments: