![]() |
| Mfanyabiashara maarufu Zanzibar, Mohammed Raza |
Ndoto ya Mfanyabiashara maarufu Zanzibar, Mohammed Raza, ya kuwa Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, imeanza kutoweka baada ya Kamati ya Maadili ya CCM kumtaka kuthibitishe uraia wake kabla ya Januari 12, mwaka huu.
Raza ametakiwa kuthibitisha kama ana uraia wa Canada kwa maadishi kabla ya Kamati Kuu ya (CC) ya CCM kukutana kuwajadili wagombea 14 wa nafasi hiyo leo.
Kamati hiyo ilikutana juzi na kutoka na mamuzi hayo baada ya kupitia na kuwajadili wagombea wote, akiwemo Raza aliwashinda katika kura za maoni.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho, Kamati hiyo ilimtaka Raza kuthibitisha kama ana uraia wa Canada kwa kuandika barua ubalozi wa Canada na kuwasilisha majibu kwa chama.
Mwenezi wa CCM Zanzibar, Issa Haji Gavu, alithibitisha kamati ya maadili kukutana Zanzibar, lakini hakuwa tayari kufafanua kama Raza alipewa maelekezo ya kuthibitisha uraia, badala yake alisema kuwa mambo yaliyojadiliwa na kuamuliwa ni siri ya kikao.
Aidha, alisema Kamati ya Maadili imekutana na kutekeleza wajibu wake na hatua iliyobakia ni matayarisho ya kikao cha CC kuteua jina moja la mgombea wa nafasi hiyo.
Raza alipoulizwa kama alitakiwa wa kuthibitisha uraia wake, alisema ni mapema kuzungumzia suala hilo.
Alisema kama kuna mtu au kiongozi mwenye wasiwasi na uraia, anayetakiwa kutoa ushahidi na vielelezo kwenye vikao badala ya yeye kutakiwa kufanya kazi hiyo.
Raza alisema kitendo hicho hakina tofauti na Mahakama kumtaka mshitakiwa kupeleka ushahidi wa kushitakiwa mahakamani badala ya kazi hiyo kufanywa na upande wa waendesha mashitaka.
Uchaguzi mdogo katika jimbo la Uzini unatarajia kufanyika mwezi ujao kufuatia kifo cha aliyekuwa mwakilishi wa jimbo hilo aliyefariki kwa ajali ya gari, Khamisi Mussa Silima, Oktoba mwaka jana.
CHANZO: NIPASHE
.jpg)
No comments:
Post a Comment