ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 24, 2012

Chamakh ashindwa kutamba, Gabon yapeta

Timu ya Taifa ya Gabon
MSHAMBULIAJI wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang alionesha kiwango cha juu kuiwezesha nchi yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Niger, juzi. 

Nyota wa Morocco, Marouane Chamakh alijikuta kwenye wakati mgumu, huku timu yake ikipokea kichapo ch mabao 2-1 kutoka kwa wapizani wao, Tunisia kwenye mchezo wa kundi C. Aubameyang, ambaye ananyoa kwa staili ya kumuiga nyota wa Brazil na Santos, Neymar, alifunga bao la kwanza kwa kichwa baada ya juhudi binafsi, kabla ya kusaidia la pili.
 

Kwenye mchezo huo ambao pia ulihudhuriwa na Rais wa Gabon, Ali Bongo, kikosi hicho kilichovalia jezi inayofanana na timu ya taifa ya Brazil, kilionyesha mchezo wa kuvutia na wa kasi huku safu ya ushambuliaji ya Niger, ikiwa butu kabisa. 

Aubameyang mwenye umri wa miaka 22, ambaye ni mtoto wa nahodha wa zamani wa Gabon, akiwa amelelewa na Klabu ya AC Milan na sasa anaichezea klabu ya Ligi Kuu ya Ufaransa, St Etienne, alikaribia kufunga bao la pili kwa kichwa, lakini golikipa wa Niger, Daouda Kassaly akautema na kumfikia Stephane Nguema aliyefunga kwa urahisi. 

Mara baada ya mchezo huo, kocha wa Gabon, Gernot Rohr ambaye ni raia wa Ujerumani alisema, “Presha ilikuwa kubwa, lakini tuliweza kucheza vizuri na kupata ushindi.” Katika mchezo mwingine juzi, Tunisia iliweza kuwanyamazisha wapinzani wake, Morocco kwa kuwachapa mabao 2-1, huku Chamakh akishindwa kutamba. 

Chamakh ambaye ni mshambuliaji wa Arsenal, msimu huu akiwa amepewa nafasi chache za kucheza, alipata nafasi nyingi za kufunga katika kipindi cha kwanza, lakini zote ziliokolewa na golikipa wa Tunisia, Aymen Mathlouthi. 

Tunisia ilipata mabao yake kupitia kwa Saber Khelifa aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Khaled Korbi dakika ya 34, kabla ya Youssef Msakni aliyetokea benchi kufunga la pili dakika ya 77, wakati lile la Morocco lilifungwa na nahodha wake, Houcine Kharjah.

No comments: