ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 24, 2012

Fifa yaipa Yanga siku 30 imlipe Njoroge


SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa) limeipa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam siku 30 iwe imemlipa beki wa zamani wa timu hiyo, John Njoroge, Sh 17, 159,800. 

Uamuzi huo uliotolewa na Fifa kupitia kitengo chake cha utatuzi wa migogoro (DRC) umeelezwa kuwa fedha hizo ni fidia kwa mchezaji huyo baada ya Yanga kuvunja mkataba wake kinyume cha taratibu.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa uamuzi huo wa DRC uliotolewa chini ya Jaji Theo van Seggelen ambaye ni raia wa Uholanzi ulifanywa Desemba 7 mwaka jana jijini Zurich, Uswisi na kutumwa TFF kwa njia ya DHL, Januari 17 mwaka huu. 

Njoroge ambaye ni raia wa Kenya aliwasilisha kesi yake Fifa kupinga Yanga kuvunja mkataba alioingia wa kuichezea timu yao kinyume na makubaliano. Mchezaji huyo hivi sasa anachezea timu ya Tusker ambayo ni mabingwa wa Kenya. 


“Yanga ina siku nne za kukata rufani kupinga uamuzi huo kuanzia tarehe iliyoupokea kama inataka kufanya hivyo. 

“Klabu hiyo inatakiwa iwe imeshamlipa Njoroge ndani ya siku 30 tangu ilipopokea uamuzi huo. Ikishindwa kulipa ndani ya muda huo, itatozwa riba ya asilimia 5 kwa mwaka ya fedha hizo. 

“Ikiwa Yanga itashindwa kulipa ndani ya muda huo vilevile suala hilo litafikishwa mbele ya Kamati ya Nidhamu ya Fifa kwa hatua zaidi,” alisema Wambura. 

Akizungumzia suala hilo jana, Ofisa Habari wa Yanga, Luios Sendeu alisema bado hawajapokea barua hiyo na kwamba watakapoipata watatoa tamko. 

“Tumesikia jambo hili, lakini tukishajulishwa rasmi, basi tutatoa taarifa yetu,” alisema Sendeu.

Habari Leo

No comments: