ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, January 8, 2012

Seif amgeukia Tendwa

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad akiwahutubia mamia ya wafuasi wa chama hicho kwenye viwanja vya Bakhresa, Manzese Argentina, jijini Dar es Salaam. Katika mkutano huo, pamoja mambo mengine, Hamad ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alitetea uamuzi wa chama chake kuwatimua wanachama wake wanne, akiwamo Mbunge wa Jimbo la Wawi, Hamad Rashid Mohammed. (Picha na Mohammed Mambo).
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, sasa amemgeukia Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, na kumtaka aache mara moja kuingilia maamuzi yaliyofanywa na chama hicho.


Badala yake amemtaka afuate sheria na kanuni ya uendeshaji wa Taasisi yake na kwamba hadi anazungumza hajapokea amri yoyote ya mahakama.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kiwanja cha Manzese Bakhresa jijini Dar es Salaam jana, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema anashangazwa kuona Tendwa mwenye jukumu la kulinda Katiba za vyama vyote anakuwa mtetezi mkuu wa Mbunge wa Jimbo la Wawi, Hamad Rashid Mohamed, ambaye amefukuzwa uanachama kwa kufuata sheria na taratibu zote.
Mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wanachama wa chama hicho, ulikuwa maalum kutoa ufafanuzi wa hatua iliyochukuliwa na Baraza Kuu la Uongozi wa chama hicho wa kuwafukuza uanachama watu wanne akiwemo Hamad.
Alisema kwa ujumla anamheshimu sana Tendwa kutokana na majukumu yake ya kitaifa lakini kwa hatua yake anayoichukua ya kumtetea Hamad ni jambo linalomshangaza.
"Baada ya kuchukuliwa maamuzi yale, Msajili wa vyama vya siasa leo amejitokeza hadharani kumtetea Hamad, jambo hili linanishangaza sana, nilitegemea yeye angetuunga mkono kutokana na kutumia Katiba yetu vizuri," alisema.
Alhamisi iliyopita Tendwa, alisema tabia ya kufukuzana uanachama kwenye vyama vya siasa sio mzuri na unalisababishia hasara taifa na wananchi wanakosa haki yao ya msingi ya kuwakilishwa bungeni.
Maalim Seif alisema nia ya Msajili kutetea jambo hilo ni kuona chama hicho kinaendeshwa kihuni bila kufuata taratibu kitu ambacho kamwe hakitafanyika.
"Kweli Msajili anatetea kwa maana gani hasa, anataka kuona CUF ikiendeshwa kihuni? Kamwe haitawezekana kwani chama hiki hapendwi mtu," alisema huku akionekana kuchukizwa na jambo hilo.
Aidha amemtaka Msajili huyo pamoja na watu wengine waliojitokeza kusimama mstari wa mbele kupinga maamuzi hayo waache mara moja kwa sababu chama hicho sio mali ya mtu bali ni taasisi inayomilikiwa na Watanzania.
Akizungumzia mazingira ya kufukuzwa Hamad na wenzake watatu, Seif alisema kabla ya kuchukua maamuzi hayo kwanza walijaribu kuitisha vikao viwili vya kumuonya kuhusu mwenendo wake mbaya, lakini hakuonyesha kubadilisha mwenendo wake.
Alisema kikao kimoja kilifanyika Zanzibar na kikao cha pili kilifanyika jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha watu mashuhuri.
Alieleza kwa ujumla baada ya hali hiyo kushindikana waliamua kufuata taratibu za chama hicho ikiwemo kuwaita watu wote wanaotuhumiwa kukihujumu chama kwa ajili ya kujitetea na walifanya hivyo.
Alisema Baraza Kuu la uongozi wa chama hicho lilichukua maamuzi hayo kwa kuangalia haki ya mwanachama na sio ubunge wa mtu, kwani ndani ya chama hicho mtu yeyote hata akiwa kiongozi akionekana kwenda kinyume na taratibu anachukuliwa hatua.
Pamoja na hayo alisema CUF imefuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kumtaarifu Spika wa Bunge juu ya uamuzi huo na kama haikutekelezwa hayo chama chake hakitahusika.
"Hakuna atakayeweza kurudisha nyuma jambo hili, tumemwambia Spika kuwa huyu Hamad sio mwanachama wetu, akitaka kumlea hilo lake," aliongeza kusema.
Akizungumzia tishio la mahakama, Maalim Seif alisema kamwe hatishiki na jambo hilo kupelekwa mahakamani kwa sababu anatambua kila kitu kiliendeshwa kisheria na hakuna kitu kilichokiukwa.
Alisema watu kuwafukuza ndani ya chama hicho sio mara ya kwanza na wote walikimbilia mahakamni lakini baadae ukweli ulibaki palepale. Hata Mahakama ikimrudishia Hamad ubunge wake, watamtambua na ataendelea kuwa Mbunge wa mahakama.
Alisema amegundua kuna ajenda za siri zinazofanywa na baadhi ya watu waliochukizwa na muafaka wa Zanzibar ambapo sasa wanafanya kila juhudi kuwarudisha nyuma Wazanzibari walioanza kupata faida ya amani.
Alisema CUF itazidi kusimama imara kupinga njama zozote zitakazosababisha visiwa vya Zanzibar kukosa amani na kurudi katika hali ya siasa za huko nyuma.
Awali Naibu Katibu Mkuu wa chama hichoTanzania Bara, Julius Mtatiro, alisema zoezi la kuwasafisha viongozi wanaoaminika ni waasi litaendelea katika ngazi zote kuanzia Wilaya, Kata hadi Matawi ya chama hicho.
Alisema kuanzia sasa wanachama wote wawe makini kuwatambua watu wa aina hiyo na baadae wafanye utaratibu wa kuwafukuza kulingana na katiba na kanuni ya chama hicho.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: