ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 27, 2012

Kinana: Wanaotaka urais 2015 wamvuruga Kikwete



ASEMA WANAVURUGA UTENDAJI WA SERIKALI KUTEKELEZA AHADI ZAKE
Leon  Bahati
ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Kampeni za Rais Jakaya Kikwete wakati akigombea urais kwa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Abdulrahman Kinana, amesema vigogo wa chama hicho walioanza kampeni za urais sasa wanavuruga utendaji wa serikali.Akizungumza jana katika ziara yake ya kutembelea matawi ya CCM mkoa wa Dar es Salaam,  Kinana alisema vigogo hao ni wabinafsi, wanaivuruga nchi na hawana lolote wanalolifanya kwa maslahi ya chama hicho tawala.
“Sasa hivi Rais Kikwete ana miaka mingine minne mbele kabla ya kumaliza uongozi wake na CCM ina kero nyingi za kushughulikia ili kutekeleza ilani yake, halafu wengine wanazungumzia urais sasa," alisema Kinana
Kinana alizitaja kero hizo kuwa ni elimu, afya, maji, barabara, mazingira, maisha magumu yanayosababishwa na mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani shilingi.


Kauli hiyo ya Kinana ambaye ni mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, imekuja katika kipindi ambacho baadhi vigogo wa CCM wamekuwa wakipigana vikumbo kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi, huku wakitumia majukwaa mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, makanisa na misikiti kujipigia kampeni.

Akizungumzia harakati za vigogo hao kugombea Urais ndani ya CCM Kinana alisema; “Wote wanaozungumza kwenye vyombo vya habari, hawasemi kwa manufaa  ya wananchi wala maslahi ya wanachama bali  kwa maslahi yao binafsi.”
Alifafanua kwamba, masuala ya kuutaka urais siyo ya kuzungumzia sasa kwani bado Rais Kikwete ana miaka minne ya kuwa madarakani huku akikabiliwa na kazi kubwa ya kutatua matatizo ya wananchi katika kipindi hiki ambacho taifa linakabiliwa na hali mbaya kiuchumi.

 “Je, huu kweli ni wakati wa kuyazungumzia hayo? (masuala ya kuwania urais)," alihoji Kinana.
Kinana alitahadharisha kuwa mazingira wanayoyajenga vigogo hao yatawafanya wanachama na wananchi kwa ujumla, wawachukie utakapowadia wakati wa uchaguzi mwingine.

Alisema anasikitishwa na hali hiyo hasa ikizingatiwa kuwa wanaoanza kupiga kampeni za urais ni watu wazito ndani ya nchi na ni wajumbe wa vikao vikuu ndani ya CCM, lakini wanaona kusema kupitia vyombo vya habari watasikika nchi nzima.

“Hao mnaowasikia wakisema kwenye vyombo vya habari ni wajumbe wa vikao tena vikubwa na hakuna anayewazuia. Wanaona wakisema kwenye vikao, wananchi hawatasikia,” alifafanua.

Kinana alisema hayo akijibu swali aliloulizwa na mmoja wa wanachama wa CCM tawi la Buguruni, aliyetaka kujua kwa nini vigogo wa chama hawaonyeshi mshikamano kwa kutotumia vikao vya chama kujali masuala mazito kama hayo, badala yake wanakwenda kwenye vyombo vya habari?

“Viongozi wa juu muwe na mshikamano, nendeni kwenye vikao, mna vikao vya kusemea, acheni kusema kwenye vyombo vya habari,” alionya Kinana

Kinana aliwahakikishia wana CCM mkoa wa Dar es Salaam kwamba, suala hilo atalifikisha kwenye chama ili lifanyiwe kazi kulingana na taratibu zake.
Katiba mpya
Kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba, Kinana alisema Rais Kikwete amekuwa akifanya kazi yake vizuri ikiwemo kuwashirikisha wadau mbalimbali kuhusu jambo hilo na amekuwa akikutana nao Ikulu ili  kujenga amani na utulivu nchini.

Aliwataja wadau hao kuwa ni pamoja viongozi wa vyama vya upinzani.
Alisema Rais ni kiongozi wa nchi na anatumia nafasi hiyo kupata maoni kutoka kwa watu mbalimbali ili kuwa na katiba mpya iliyo bora.

Kwa mujibu wa Kinana, Rais Kikwete amekutana na viongozi wa vyama vya upinzani na tayari amepata maoni ya CCM, kupitia Kamati yake Kuu (CC).Hivyo, alisema Rais anakutana na makundi yote ya watu bila upendeleo ili kujenga mshikamano katika kuandika katiba mpya.

Alifafanua kwamba, kinachofanyika sasa ni kuunda mchakato wa namna maoni ya katiba hiyo yatakavyochukuliwa kutoka kwa wadau mbalimbali.

Hata hivyo, alisema kwa sasa Rais anasubiri wabunge wafanyie marekebisho baadhi ya vipengele vya Sheria ya Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.Kinana alisema baada ya marekebisho hayo, Rais ataunda tume ya kukusanya maoni itakayojumuisha watu wa kada zote bila kujali itikadi za vyama vyao vya siasa.

Akerwa na 'uheshimiwa'
Katika hatua nyingine Kinana alisema  amekuwa akikerwa na tabia ambayo katika siku za karibuni imeshika kasi, kwa viongozi ndani ya chama kuitwa “waheshimiwa.”

Alisema hata kwenye mikutano yake na wanachama jijini Dar es Salaam amekuwa akiitwa “mheshimiwa” ambalo hakubaliani nalo na kushauri neno kuwa sahihi linalopaswa kutumika ni “ndugu.”

Rushwa ndani ya CCM
Kinana alisema kuwapo kwa vitendo vya rushwa ndani ya chama ni tatizo linachangia kwa kiasi kikubwa kupata viongozi wasiofaa ndani ya chama, hivyo kusisitiza kuwa safari hii, wameamua kulivalia njuga.
Alisema wanaotaka uongozi kwa rushwa hawafai kwa sababu hawana malengo mazuri ya chama bali binafsi.
Kinana alionya kwamba, kuna baadhi ya wanachama ambao huwashawishi wagombea ili wawape fedha kwa ajili ya kuwapigia kampeni na kuhakikisha kuwa wanashinda.
Alisema mwanachama anayetaka fedha ili amchague kiongozi hana malengo mazuri na chama hicho, hivyo naye anapaswa kuchukuliwa hatua kwa vile kufanya hivyo ni kukisaliti chama.

CCM kufuta unafiki
Katika hatua nyingine, CCM mkoa wa Dar es Salaam umesema katika uchaguzi ndani ya chama na jumuia zake unaotarajia kufanyika mwezi ujao, wamepania kuondoa aina zote za unafiki.

Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salam, Said Mihewa alisema katika kuchuja wagombea, watahakikisha haki inatendeka na kipaumbele kitatolewa kwa wanachama kufanya uamuzi.

Alisema iwapo vikao vya chini, tawi na kata vitamwelezea mwanachama yeyote kwamba hafai kuwa kiongozi, watawaita na kuwakutanisha ana kwa ana na wanayemtuhumu ili wafafanue jinsi asivyofaa.
“Tutawaita na kuwakutanisha na mnayesema hafai, mseme mbele yake kuwa hafai! Na yeye ajieleze kwa nini anasema anafaa?” alisema Mihewa.

Mchakato wa uchaguzi wa ndani wa CCM unatarajiwa kuanza mwezi ujao na kumalizika Oktoba mwaka huu.

Mwananchi

No comments: