ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 21, 2012

Mabadiliko makubwa yaja uchaguzi CCM

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC),Nape Nnauye
WABUNGE WAPIGWA ‘STOP’,TAKUKURU WATANGAZA VITA
Waandishi Wetu
MABADILIKO makubwa yanatarajiwa katika uchaguzi wa ngazi zote ndani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao mchakato wake umepangwa kuanza mwezi ujao.Miongoni mwa mabadiliko hayo ni pamoja na wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuzuiwa kugombea nafasi yoyote ndani ya chama, ikiwa ni hatua ya kufanya mageuzi yenye lengo la kuondoa tatizo la baadhi ya watu kujilimbikizia madaraka.

“Ikiwa mbunge au mjumbe wa Baraza la Wawakilishi anataka kugombea uongozi wa chama, basi lazima apate kibali cha Kamati Kuu ya CCM na si vinginevyo,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya chama hicho.

Habari ambazo Mwananchi lilizipata na kuthibitishwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Nape Nnauye zinasema uchaguzi ndani ya chama hicho tawala unatarajiwa kufanyika kwa kuzingatia marekebisho yanayofanywa katika katiba yake.

Nape alikiri jana kwamba kuna mchakato wa marekebisho ya katiba ya CCM. Hata hivyo, hakuwa tayari kuzungumzia kwa undani marekebisho hayo.

Jumatano wiki hii, CCM kilitangaza ratiba ya uchaguzi huo wa ndani ya chama pamoja na jumuiya zake, ambao uchukuaji  fomu utaanza Februari 4, mwaka huu kwa ngazi ya shina, tawi na kata.
 Ratiba iliyotolewa na Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba, Dar es Salaam inaonyesha kwamba katika uchaguzi wa ngazi ya wilaya, mkoa na taifa, fomu zitaanza kutolewa Juni 2, mwaka huu.  Uchaguzi huo unapewa umuhimu mkubwa na wachunguzi wa masuala kisiasa ambao wanauchukulia kama sehemu ya maandalizi ya chama hicho kutwaa tena dola katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Mchakato wote uchaguzi huo kwa ngazi zote, unatarajiwa kukamilika Novemba 11,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyotangazwa wiki hii na Radio Uhuru inayomilikiwa na CCM.

Mabadiliko ya Katiba
Katika mabadiliko ya katiba yanayofanywa na chama hicho, imeelezwa kwamba hatua ya kuwaengua wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika kinyang’anyiro cha nafasi za uongozi wa chama ni kuondoa tatizo la baadhi ya watu kujilimbikizia madaraka.
Kazi hiyo inafanywa na Kamati ya Marekebisho ya Katiba ya CCM chini ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Pius Msekwa na inatarajiwa kuwasilisha matokeo ya kazi yake katika vikao vya juu vya CCM vinavyotarajiwa kukutana Dodoma mwezi ujao.

Nape alikiri kwamba kuna mabadiliko yanayotarajiwa na kutaja moja tu kwamba ni lile la kufutwa kwa nafasi za wajumbe wa NEC wa mikoa na badala yake nafasi hizo kurejeshwa katika ngazi za wilaya.

Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi alisema pia wajumbe wa NEC kutoka katika jumuiya za chama wanapendekezwa kuchaguliwa na jumuiya husika badala kupigiwa kura na Mkutano Mkuu wa CCM kama ilivyo sasa.

Alipoulizwa kuhusu kupitishwa kwa mabadiliko hayo na vikao husika Nape alisema: “Najua  unachotaka kufahamu ni iwapo kuna mgogoro wa kikatiba, haupo kwani katiba yetu ina vipengele ambavyo vinaruhusu NEC kutekeleza jukumu hilo.”

“Kwa hiyo mapendekezo yatapelekwa kwenye kikao kijacho cha NEC na yakishapitishwa, basi yataanza kutumika isipokuwa tu kwa mujibu wa katiba lazima Mkutano Mkuu wetu uarifiwe kuhusu hatua hiyo.”

Juzi, Nape alinukuliwa akiwataka watu wanaoona kwamba anakivuruga na kukigawa chama hicho kutokana na kauli zake za kutilia mkazo miongozo na kanuni, watoke CCM na kuanzisha chama chao.  Alitoa kauli hiyo alipokuwa akihojiwa na Kituo cha Televisheni ya Taifa ya TBC1 juu ya maadhimisho ya miaka 35 ya CCM, uchaguzi ndani ya chama na matembezi ya mshikamano, mwaka huu. 
“...Mimi navuruga ulaji wa wachache, si kuvuruga chama, naamini nipo sahihi kwa sababu natetea wengi. Kama ninakigawa chama kwa kuvuruga ulaji wa wachache, basi nitaendelea kukigawa, wachafu waanzishe chama chao cha wachafu na wasafi wabaki upande wao (CCM).”  Alisema sasa ni wakati wa kukirejesha chama hicho katika misingi yake na siyo wachache kukitumia kujinufaisha. 
Ratiba ya uchaguzi
Ratiba inaonyesha kuwa uchaguzi huo umegawanyika katika sehemu kuu mbili; uchaguzi wa viongozi wa chama na ule wa Jumuiya zake.  Kwa mujibu wa ratiba hiyo, wanachama watakaowania uongozi kwenye jumuiya katika ngazi ya shina, wataanza kuchukua fomu kuanzia Februari 4 na uchaguzi utafanyika Februari 29, mwaka huu.
Kwa upande wa uongozi wa chama ngazi hiyo ya shina, uchukuaji fomu, utaanza Machi 23 na uchaguzi utafanyika Aprili 30.

Katika ngazi ya tawi, fomu kwa wagombea wa jumuiya zitaanza kutolewa Machi 3 na uchaguzi wake utafanyika Aprili 22, wakati fomu za kuwania uongozi wa chama zitaanza kutolewa Februari 20 na uchaguzi utafanyika Machi 31.

Katika ngazi ya kata, wagombea wa jumuiya wataanza kuchukua fomu Mei 4 na uchaguzi wake ni Juni 30, wakati kwa wagombea wa chama fomu zitaanza kutolewa Mei 13 na uchaguzi utafanyika Julai 4.  Ngazi nyingine
Visiwani Zanzibar, fomu kwa ajili ya uchaguzi wa majimbo zitaanza kutolewa Juni 2 na uchaguzi wake kufanyika Julai 26 kwenye jumuiya na Agosti 2 kwa wagombea wa uongozi wa chama.
Kwa upande wa wilaya, ratiba hiyo inaonyesha kwamba fomu za uchaguzi wa viongozi wa wilaya wa jumuiya Tanzania Bara, zitaanza kutolewa Juni 2 na uchaguzi wake kumalizika Agosti 22, huku fomu kwa ajili ya viongozi wa chama, zikipangwa kuanza kutolewa Juni  2 na uchaguzi kufanyika Septemba 26. 
Taarifa hiyo ilifafanua kwamba  katika ngazi ya mkoa, uchaguzi wa jumuiya utaanza Juni 2 na uchaguzi utafanyika Septemba 26 na fomu za uchaguzi wa viongozi wa chama, zitaanza kutolewa Juni 2 na uchaguzi wake kufanyika Oktoba Mosi mwaka huu. 
Ngazi ya taifa, fomu zitaanza kutolewa Juni 2 kwa wagombea wa jumuiya na uchaguzi wake utafanyika Oktoba 5 na fomu kwa ajili ya wagombea wa ngazi ya chama, zitaanza kutolewa Oktoba 25  na uchaguzi utafanyika Novemba 11.  Mkutano Mkuu wa taifa unatarajiwa kufanyika Oktoba 9 ili kukamilisha Uchaguzi Mkuu na kuunda Sekretarieti ya Taifa.
 Takukuru waonya  Wakati hayo yakiendelea, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imetangaza vita kwa  wote watakaotoa na kupokea rushwa ili kushinda katika nafasi mbalimbali za uchaguzi huo ndani ya CCM.

Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, ambako uchaguzi ngazi ya taifa unatarajiwa kufanyika, Sostenes Kibwengo amesema kuwa taasisi hiyo imejipanga kukabiliana na vitendo vya rushwa vitakavyojitokeza.
“Hatutamwonea haya mtu yeyote hata kama ni mkubwa kiasi gani, maana uchaguzi huo huwa unajaa vibweka ukizingatia mwaka huu wanapanga safu zao kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2015,’’alisema Kibwengo na kuongeza:   “Tusipokuwa makini na jambo hilo, CCM kitaingiza viongozi wabovu na wazembe ambao mwisho wa siku, wataifanya Serikali yote kuwa ni ya wala rushwa.’’
Kauli hiyo imeungwa mkono na Takukuru Taifa. Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwan alisema kimsingi suala hilo limo ndani ya taasisi hiyo mkoani Dodoma hasa kwa kuzingatia kuwa mkutano huo unafanyika kwenye eneo lake.

Habari hii imeandaliwa na Exuper Kachenje, Keneth Goliama na Habel Chidwali, Dodoma

Mwananchi

No comments: