Waamriwa kuripoti wizarani
Wao wasema hawataondoka
Dodoma waendelea kugoma
Wao wasema hawataondoka
Dodoma waendelea kugoma.jpg)
Kutokana na kitendo hicho, uongozi wa hospitali hiyo umewaamuru warudi Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili wakapangiwe vituo vingine vya kazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Dk. Marina Njelekela katika taarifa yake kwa madaktari hao, aliwataka kuhakikisha wanarudisha vifaa ambavyo walipatiwa na hospitali hiyo ikiwemo funguo za vyumba, vitambulisho na kuripoti katika Wizara hiyo mara moja.
Awali madaktari hao walikuwa wakiidai serikali Shilingi milioni 176 ambazo ni posho kwa ajili ya kujikimu na kucheleweshwa kuzipata na kuwafanya waishi katika mazingira magumu.
Madaktari hao ambao tangu juzi jioni walianza kuingia wodini na kuanza kutoa huduma kwa wagonjwa, baada ya kupatiwa posho zao, lakini ilipofika jana majira saa 11:00 alfajiri wakiwa wanabadilishana zamu walijulishwa kuwa wanatakiwa waende jengo la utawala kupewa maelekezo.
Baada ya kufika katika jengo hilo kila mmoja alikuwa anapatiwa barua yake ambayo ilimjulisha kuwa anatakiwa kurudi katika Wizara hiyo kutokana na kukiuka makubaliano ya mafunzo kwa vitendo.
NIPASHE ilifanikiwa kuipata barua hiyo iliyosainiwa na Dk. Njelekela, ikieleza kuwa uamuzi huo ulifanywa na makubaliano ya uongozi wa hospitali hiyo.
Moja ya vipengelea cha barua hiyo ilisomeka kuwa: “Uamuzi huu umechukuliwa baada ya wewe kukiuka makubaliano ya mafunzo kwa vitendo baina yako na hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kifungu namba 1 (b), (d), (f) na (g) kama ilivyoelekezwa na Katibu Mkuu katika barua yake ya kukupangia mafunzo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.”
MADAKTARI: HATUONDOKI
Kwa upande wake kiongozi wa madaktari hao, Dk. Deogratus Mally, alisema kuwa tayari fedha zao zimeingia tangu juzi jioni majira ya saa 11:00 na kwamba baadhi yao waliingia wodini jioni.
Alisema jambo la kuvunjwa kwa mkataba sio la kweli kwani ilikuwa ni halali yao kudai haki yao ya msingi kwa kuwa walikuwa wanaishi katika mazingira magumu na wengine kukosa hata nauli ya kwenda kazini.
“Wao wametuvunjia mkataba wetu kwa kutucheleweshea fedha kwani makubaliano ni kwamba kila mwisho wa mwezi tunapatiwa posho zetu na hawakutujulisha kama fedha zetu zitachelewa, halafu leo hii wanajifanya kutubadilishia kibao kuwa sisi tumevunja mkataba, hivyo basi hatupo tayari kuripoti wizarani,” alisema Dk. Mally.
Dk. Mally alikanusha madaktari hao kugoma kama walivyoambiwa, lakini alisema wanachojua walimwandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kumjulisha kuwa wameshindwa kwenda kazini kutokana na kutokuwa na fedha za usafiri pamoja na matatizo mengine.
Dk. Mally alisema waliowacheleweshea fedha zao ndio waliovunja mkataba na kwamba makubaliano katika mkataba wao ni kila mwisho wa mwezi kupatiwa posho zao ili waweze kujikimu, lakini haikufanyika hivyo.
“Sisi hatujafanya mgomo kama inavyodaiwa ila tunachokijua ni kwamba hatujaingia kazini kutokana na hali zetu kutokuwa nzuri katika masuala ya kifedha na ndio maana wengine iliwawia vigumu kuendelea na kazi mpaka hapo watakapopatiwa posho zao. Tulipopatiwa fedha zetu juzi jioni tulianza kazi, tunashangaa kupatiwa barua za kufukuzwa,” alisema Dk. Mally.
Kuhusiana na madai kuwa wamevunja mkataba, alisema watatafuta mwanasheria ili kulijadili jambo hilo na kusisitiza kuwa hawapo tayari kwenda kuripoti wizarani.
Alisema kwa sasa wanajiandaa kumuandikia barua Mkurugenzi wa hospitali kumjulisha kuwa hawajavunja mkataba kama alivyodai.
“Mamlaka ya kutuambia kuwa twende wizarani kwa ajili ya kupangiwa vituo vingine vya kazi sio jukumu lake kwani sisi tumewekwa pale kwa ajili ya wizara, tulitegemea kuona wizara ndio inatuambia tukapangiwe vituo vingine,” alisema Dk. Mally.
Alisema kwa sasa wanasubiri majibu kutoka Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kwa kuwa walikuwa na kikao wizarani jana kabla ya kutoa tamko lao.
Hata hivyo, alisema ameshindwa kuelewa sababu ambazo zimewapelekea kunyimwa kutoa huduma kwa wagonjwa wakati hali sio nzuri katika wodi.
Alisema mpaka jana, huduma zikikuwa zimezorota kutokana na kuwepo kwa madaktari wachache ambao wanajikuta wakifanya kazi nyingi, hali ambayo inaweza ikaleta madhara.
MGOMO WAENDELEA DODOMA
Hali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma imeendelea kuwa tete, baada ya mgomo wa madaktari kuendelea.
Mgomo huo wa madaktari huo ulianza juzi, umesababisha kudorora kwa huduma.
Zaidi ya madaktari 33 ambao wanaidai wizara hiyo fedha kuanzia Novemba na Desemba, mwaka jana.
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Nassoro Mzee, alisema hadi jana madaktari walikuwa wanaendelea na mgomo, ingawa fedha ipo kwenye utaratibu wa kulipwa.
Alisema fedha hizo zilishawasili hazina ndogo ya Dodoma na kinachosubiriwa ni kuwalipa.
Kutokana kwa kuzorota kwa huduma, hospitali hiyo ililazimika kuazima madaktari kutoka hospitali ya Manispaa ya Makole, Udom na hospitali ya Ifakara ili kuweza kuongeza nguvu katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
“Fedha zimeshafika na zipo kwenye utaratibu hadi Jumatatu nina imani madaktari wote watakuwa wamelipwa,” alisema.
Naye, Katibu wa hospitali hiyo, Isaack Kaneno alisema madaktari hao wamekataa kuingia kazini kwa madai kuwa hadi wapate fedha mkononi.
Kaneno alisema licha ya kuelezwa kuwa fedha zipo hazina na zinashughulikiwa, bado wamekosa imani.
Alisema ingawa wanasisitiza kuwa wanadai miezi miwili, ukweli ni kuwa ni za mwezi mmoja.
“Inasikitisha, wenyewe wanadai mwezi mmoja na hapo hapo kuna watumishi wengine wa serikali wadai miezi mingi, mbona hawajagoma kwa nini wao?” alihoji.
MADAKTARI WA TEMEKE WALIPWA
Hatimaye madaktari wanaofanya kazi kwa vitendo katika Hospitali ya Temeke, mkoani Dar es Salaam, jana walilipwa posho zao. Zoezi kuwalipa lilifanyika kuanzia majira ya saa 4:00 asubuhi na hadi mchana madaktari wote 30 wanaofanyakazi katika hospitali hiyo walikuwa wamelipwa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Magreth Nyalile, alisema zoezi la ulipaji lilifanyika katika hali ya utulivu na hakuna daktari aliyekosa malipo.
Alisema kutokana na umuhimu wao katika utoaji huduma za matibabu, waliamua ulipaji ufanyike kwenye eneo la hospitali badala ya ofisi za Manispaa ili kuepuka usumbufu.
“Zoezi la ulipaji lilianza kufanyika tangu saa nne asubuhi ya leo (jana), nafurahi kuona hakuna malalamiko ya mtu kukosa pesa,” alisema Nyalile.
Aidha, alieleza kuwa wameamua kuwalipia dirishani ili kuokoa muda, lakini katika miezi iliyobakia madaktari hao wataingiziwa malipo yao kwenye akaunti zao za benki kama inavyofanyika kwa watumishi wengine.
Imeandikwa na Beatrice Shayo, Moshi Lusonzo, Dar na Jacqueline Massano, Dodoma.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
Aibu Tanzania.
Post a Comment