Sasa wapora shehena ya shaba
Jeshi la Polisi Mkoa wa Temeke, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, inawashikilia watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, kwa tuhuma za kuteka lori lililobeba shehena ya madini aina ya shaba mkaoani Morogoro na kuja kuyauza Dar es Salaam.
Watu hao ambao hawajafahamika, wanatuhumiwa kuteka lori hilo aina ya Scania, baada ya kumfunga kamba dereva na utingo wake na kisha kuwatupa porini eneo la Mikumi mkoani Morogoro.
Kamanda wa Polisi Mkoa huo, David Misime, alithibitisha kushikiliwa kwa watu hao kwa tuhuma hizo.
Kwa mujibu wa Kamanda Misime, lori hilo lenye namba za usajili T818 AML lenye tela namba T862 AWR, lilikuwa likitokea nchini Zambia kwenda bandari ya Dar es Salaam.
Alisema lilitekwa juzi eneo la Mikumi, Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.
Kamanda Misime alisema taarifa za tukio hilo walizipata siku hiyo kutoka mkoani Morogoro na ndipo walipoanza jitihada za kufuatilia.
Alisema jitihada zao zilizaa matunda baada ya jana kulikuta lori hilo likiwa limeegeshwa katika Barabara ya Mbozi, eneo la Chang’ombe, wilayani humo, nje ya kiwanda cha kutengeneza nyaya cha MCL na kuwatia mbaroni watu hao.
Habari zinasema kuwa watu hao walitaka kuingiza shehena hiyo ya shaba kwenye kiwanda hicho kwa ajili ya kuiuza.
Hata hivyo, Kamanda Misime alisema wanaendelea na uchunguzi, ikiwa ni pamoja na kuwatafuta watu wengine zaidi wanaotuhumiwa kuhusika na utekaji huo.
“Tunasubiri wenzetu (polisi) wa Morogoro, kwa sababu dereva aliyetekwa kesi ilifunguliwa Morogoro,” alisema Kamanda Misime.
Lori hilo, ambalo mmiliki wake bado hajafahamika, linashikiliwa katika kituo cha Polisi Chang’ombe, jijini Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment