ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 6, 2012

Majina ya walioteuliwa kushiriki kozi ya ngumi yatajwa

Kocha wa mchezo wa ngumi wa timu ya Ashanti na timu ya Mkoa wa Ilala Kimichezo, Rajabu Mhamila 'Super D',  pichani  aliyeteuliwa kushiriki kozi hiyo ya kimataifa.
SHIRIKISHO la Ngumi za ridhaa nchini (BFT) limepiga panga majina matano kati ya 30 ya makocha alioteuliwa kushiriki kozi ya kimataifa ya mchezo huo iliyopangwa kufanyika Januari 16 mwaka huu.
BFT imewakata washiriki hao baada ya Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kuwataka BFT kupunguza idadi hiyo kutokana na hasara iliyosababishwa na washiriki katika kozi ya awali iliyokuwa ifanyike tangu mwezi Novemba mwaka jana.

TOC ambayo huandaa kozi za michezo mbalimbali kutokana na ruzuku inayotolewa na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) ilikuwa iendeshe kozi hiyo tangu mwaka jana lakini haikufanyika kutokana na mkufunzi wa kozi hiyo kutoka nchini Algeria kuingia mitini.

TOC ililazimika kuwalipa nauli baadhi ya washiriki waliotoka nje ya Dar es Salaam kutoka katika fungu la pesa   za kuendeshea kozi hiyo hivyo kuwataka BFT kupunguza idadi hiyo hasa wale waliofanya utovu wa nidhamu katika kozi ya awali ili kiwango cha pesa kilichobaki kitosheleze mahitaji wa kozi itakayoendeshwa Januari 16 mwaka huu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga, alisema idadi ya makocha 25 waliowateua inaweza ikapungua tena kulingana na bajeti waliobaki nayo TOC ambapo, hata hivyo, hakuyataja majina matano ya washiriki walioachwa .

Aliwataja washiriki waliopenya kuhudhuria kozi hiyo kuwa ni mpiga picha wa Magazeti ya Business Times, Majira, Sports Starehe na Jarida la Maisha ambaye pia alikuwa bondia, Rajabu Mhamila 'Super D', Arnold Ngumbi, Moses Lema,  Anthony Mwang'onda na Edward Emmanuel (Dar es Salaam). Wengine ni Yahaya Mvuvi (Tabora), Joseph Mayanga na Zakaria Mwaseba (Morogoro), Omari Saady na Mussa Bakari (Mwanza), Ally Ndee (JKT Mbeya), Emilio Moyo na Gaudence Uyaga (Pwani) Juma Liso (Magereza Kigoma), Lyinda Kalinga (Dodoma) na Abdalah Bakari  (Tanga).

Wengine ni  Mohamed Hashim  (Polisi Dar es Salaam), David Yombayomba, Haji Abdalah, Said Omari (JWTZ),  Mazimbo Ally, Rogate Damian na Fatuma Milanzi (JKT), Musa Maisori na Hamisi Shaaban (Magereza Dar es
Salaam).

Kozi hiyo itaendeshwa na mkufunzi wa kimataifa, Josef Diouf, kutoka shirikisho la kimataifa la mchezo huo (AIBA) ambaye atashirikiana na makamu wa Rais wa BFT, Michael Changarawe. Kozi hiyo itafanyika  katika Shule ya Sekondari ya Filbert Bayi Kibaha Mkoani Pwani  na itafikia tamati  Januari 24 mwaka huu.

No comments: