KATIKA sehemu ya pili wiki iliyopita, nilieleza kuwa ni kawaida kwa watu wengi kufanya mambo kadha wa kadha kwa lengo la kuteka hisia za mtu anayemtaka. Lengo lao ni kurusha roho tu ili kumfanya mhusika avutwe naye. Hujaona mtu anaazima gari kwa lengo la kutongozea? Watu wa aina hiyo wapo na wanaendelea kuwepo.
Usimshangae huyo, mwingine huazima hata
nguo pindi anapokwenda kukutana na mtu anayemtega kuwa wake. Jambo la kutambua ni kuwa hilo ni moja kati ya makosa makubwa ambayo watu huyafanya katika uhusiano wa kimapenzi. Usimshangae huyo, mwingine huazima hata
Katika kosa la maigizo, wengine huamini mpaka nguvu za giza. Kwamba mtu anabadilisha waganga ili kuteka hisia za mtu. Muhimu ni kutambua kuwa hakuna mganga wala mchawi anayewezesha kuufanya uhusiano wako uwe na afya.
Kitendo cha kujipa tabia au muonekano wa bandia ni ishara kuwa hujikubali. Sasa kama wewe mwenyewe unashindwa kukubali ulivyo, unataka nani akukubali? Kadhalika, hiyo ni dalili kwamba hujiamini. Je, kama wewe hujiamini, unataka nani akuamini?
Achana na maigizo, jiamini na uache mguso wako wa asili ndiyo umvute. Wengi wanaoendeshwa na kujivika uhusika ambao hawana ni washamba wa mapenzi. Hata kama baadhi hufanikiwa kutimiza matarajio yao mwanzoni lakini mwisho hubaki na aibu.
KUZIDIWA NA HISIA MAPEMA
Jambo lingine ambalo ni hatari kubwa ni kuzidiwa na hisia mapema. Hakuna anayeweza kupinga ukweli kuwa mapenzi ni mchezo wa hisia, kwa hiyo siyo kosa kuzionesha kwa mtu ambaye umempenda. Tatizo ni wakati wa kuzionesha. Haifai kuzidiwa mwanzoni mwa uhusiano.
Ikae akilini kwako kuwa maisha ya sasa, mpaka unakuja kukutana na mwenzi wako, utakuwa umeshapita kwa wengine, naye ni hivyohivyo, kwa hiyo kila mmoja anajua matarajio ya mapenzi. Kitendo cha kuzidiwa na hisia huamsha hali fulani ya usumbufu kwa mwingine.
Nitoe msisitizo kuwa watu wazuri kwenye mapenzi ni wachache lakini wanatolewa macho na wengi. Kwa kulitambua hilo, unapaswa kuishi kwa akili ili usigeuke kero. Endapo atakuona msumbufu, hatasita kumkaribisha yule ambaye anamuona atampa furaha badala ya karaha.
Lazima atakuwa na uzoefu wa kimapenzi, bila shaka anaujua utulivu katika uhusiano. Kama ndivyo, unadhani atakubali kupoteza muda kwako, wakati kila siku unachemsha kichwa chake kwa maswali au vitendo ambavyo chanzo chake ni kuzidiwa na hisia za mapenzi juu yake.
Ieleweke kuwa hisia hutokana na ukweli wa mapenzi. Yaani, unapozidiwa na hisia, maana yake moyo wako haudanganyi. Unapenda kupitiliza, kwa hiyo unakuwa unahitaji na mwenzako naye akutendee haki. Ni hapo ndipo usumbufu huibuka. Upendo kugeuka kero kwa anayependwa.
Mapenzi siyo maneno, vitendo ndiyo hutafsiri upendo. Vema ukatia akilini kuwa kama kweli unampenda, utamsaidia pia kupata utulivu. Wewe ndiye utamfanya awe na utulivu, endapo hutampa usumbufu wa hapa na pale. Inahitaji busara kidogo kulitambua hilo, kwani wengi wamefeli.
Mara nyingi mtu anayezidiwa na hisia, hushindwa kujidhibiti. Mwenzi wake akichelewa kujibu SMS, hugeuka tatizo kubwa linalohitaji suluhu ya mtu wa tatu. Akimpigia simu, ikaita mara saba bila kupokelewa, akipokea tu shari. Kabla ya salamu ni swali: “Mbona hupokei simu?”
Katikati ya mazungumzo, kama upande wa pili utaonekana kuna utulivu, shari inaanza: “Mbona upo sehemu iliyotulia hivyo? Upo wapi?” Kwa akili ya haraka, inamtuma mwenzi wake yupo nyumba ya kulala wageni, hoteli au sehemu yoyote akishiriki tendo la faragha na mtu mwingine.
Hisia mara nyingi hudanganya, kwani huzalisha mawazo mabaya na matokeo yake ni karaha ndani ya uhusiano. Hakuna anayeweza kuvumilia tuhuma za kila mara. Mapenzi maana yake ni amani na furaha, wewe hiyo amani humpi, furaha ndiyo hana kabisa. Lazima atakukimbia au atakuumiza zaidi kwa sababu anaweza kutafuta mlango wa kutokea wakati hujajiandaa kuachwa.
KUSHINDWA KUSOMA ALAMA
Zipo alama muhimu ambazo ni vema kuzijua na uzibaini kwa mwenzi wako kabla hujazama kwenye dimbwi la mapenzi. Bahati mbaya wengi hutawaliwa na papara, matokeo yake hushindwa kubaini vitu ambavyo vinaweza kumfanya apate uelekeo wa uhusiano wake.
Katika pointi hii, nashauri watu kwenda kwa mwendo wa kinyonga badala ya kupiga mbizi bila kujua kina cha maji. Kusoma alama muhimu kwa mwenzi wako mapema ni sawa na kutegua kitendawili. Itakusaidia kujua kama kweli uliyenaye ana mapenzi ya kweli au anaweza kuwa laghai.
Wengi wanapoingia kwenye uhusiano wa kimapenzi hueleza kuwa wanapenda, tena huweka wazi kuwa hisia zimeanguka kwa wale wanaowapenda. Hata hivyo, huacha mambo mengi ndani ya uvungu wa nyoyo zao. Wewe utakuwa mshindi, endapo utaweza kumsoma mwenzi wako na kumuelewa kinagaubaga.
Pointi hapa ni kuwa mwanzo kabisa wa uhusiano, yapo mambo mengi ambayo kila mmoja hujitahidi kuyazungumza. Hiyo huita kujiweka wazi lakini imethibitika kitaalam kwamba maelezo ambayo hutolewa ni asilimia 40 tu, zilizobaki hufichwa. Asilimia 60 zilizobaki utazifichua kwa kusoma alama muhimu.
Nyongeza ni kwamba mara nyingi wengi hujitahidi kusema uongo mwanzoni mwa uhusiano. Hata kama mtu anapenda lakini hudanganya hili na lile pengine kwa hofu, tahadhari au kama pointi ya kushinda penzi. Mantiki hapa ni kukutaka uwe makini na umsome mwenzako kwa undani kabisa.
No comments:
Post a Comment