Advertisements

Tuesday, January 31, 2012

Muhimbili ni maafa

  Maiti sasa zajazana wodini
  Madaktari waendelea kugoma
  Wauguzi nao waanza mgomo
Siku moja tu baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwataka madaktari kusitisha mgomo na kurejea kazini vinginevyo watajifukuzishwa kazi, hali imezidi kuwa mbaya katika hospitali ya Taifa Muhimbili na jana viliripotiwa vifo 10.

Mbali na hali ya vifo hivyo, madaktari wachache tu ndio walioripoti kazini jana, huku wengi wao wakiendelea na mgomo na
wengine wakiishia kusaini kitabu cha mahudhurio kazini bila kuhudumia wagonjwa.
Mwenyekiti Chama cha Wauguzi Muhimbili (Tanna), Paul Magesa, akizungumza na waandishi wa habari jana alisema wamseshuhudia maiti 10 ndani ya wodi mbalimbali ambazo hazijathitishwa vifo na madaktari hadi ilipotimia jana mchana.
Wakati hali ikiwa hivyo, wauguzi nao jana waliungana na madaktari kugoma kufanya kazi wakitaka Pinda afute kauli yake ya kutaka kuwafukuza madaktari, ambao wangeendelea na mgomo jana.
Kauli nyingine ya Pinda iliyopingwa na wauguzi ni ile ya kuitaka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupeleka madaktari wake katika hospitali za Mkoa wa Dar es Salaam ili kusaidia wagonjwa walioko hospitalini.
Hali hiyo ilishuhudiwa na timu ya waandishi wa NIPASHE jana, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam na hopitali nyingine za mikoa na wilaya.
Kutokana na hali hiyo, idadi ya wagonjwa wanaopelekwa katika hospitali ya Muhimbili ilishuhudiwa ikiwa imepungua kwa kiasi kikubwa kulinganisha na siku za nyuma, huku huduma kwa wagonjwa zikiwa zimezorota kwa kiwango cha kutisha.
Mbali na hayo, pia wagonjwa kadhaa waliofikishwa MNH kwa nyakati tofauti wakiwa ndani ya magari ya kubebea wagonjwa (ambulance), hawakupokelewa na watumishi wa hospitali hiyo.
Hali hiyo ilisababisha baadhi yao kupoteza maisha muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo na kukosa huduma za dharura.
Waandishi wa habari ambao walipata fursa ya kutembelea wodi za Sewahaji, Mwaisela na Kibasila, katika hospitali hiyo wakiongozwa na Ofisa wa Idara ya Uhusiano ya Hospitali hiyo, Jezza Waziri.
Walishuhudia katika wodi hizo vitanda vingi vya kulaza wagonjwa vikiwa vitupu baada ya ndugu kuwachukua wagonjwa wao na kulazimika kuwapeleka katika hospitali za binafsi na wengine kuwarudisha majumbani. 
Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa MNH, Aminiel Algaesha, alithibitisha madaktari wachache kuripoti kazini jana, wengi wao kuendelea na mgomo na wengine kuishia kusaini kitabu cha mahudhurio kazini bila kufanya kazi yoyote.
Miongoni mwa madaktari walioripoti kazini jana, ni Dk. Aziz Keto, ambaye alikutwa akiendelea na kazi katika wodi ya Mwaisela.
Akizungumza na waandishi wodini hapo, Dk. Keto alisema kilichomsukuma kurejea kazini jana, ni roho ya ubinadamu ya kujali wagonjwa wanaoendelea kuteseka kutokana na mvutano uliopo kati yao na serikali.
Hata hivyo, alisema kwa jumla hali katika hospitali hiyo ni mbaya kufuatia kauli ya Pinda dhidi ya madaktari juzi na kwa hiyo, akaitaka serikali kutofumbia macho madai ya madaktari. 
Naye Algaesha alisema wengi wa madaktari waliosaini mahudhurio, walikwenda hospitalini hapo wakiwa wamevaa kiraia.
Kutokana na hali hiyo, alisema huduma ilikuwa ikitolewa kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo peke yake.
Hata hivyo, alisema huduma za kujifungua kinamama ziliendelea kutolewa kama kawaida, lakini zile za kliniki hazikuwapo.
Alisema idadi ya mahudhurio kwa wagonjwa imeshuka. Kitengo cha Wagonjwa wa Dharura kabla ya mgomo wa madaktari kilikuwa kikipokea wagonjwa 60 hadi 70, lakini sasa wamepungua kufikia kati ya watano hadi 10.
WAUGUZI WAUNGANA NA MADAKTARI KUGOMA
Nao wauguzi jana walisitisha rasmi kutoa huduma kwa wagonjwa MNH, huku wakimtaka Pinda kufuta kauli yake ya kutangaza kuwafukuza kazi madaktari wote walio katika mgomo na kutangaza kuwapeleka madaktari wanajeshi, badala yake atafute njia nzuri ya kuzungumza nao ili wafikie muafaka.


Msimamo wa wauguzi wa kumtaka Pinda kutekeleza mambo hayo, ulitangazwa kupitia chama chao tawi la MNH (Tanna) jana.  


Akitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari jana, Mwenyekiti Magesa alisema wapo tayari kuendelea na kazi endapo serikali itafikia muafaka na madaktari.
Alisema endapo serikali haitafanya jitihada za dhati kushughulikia tatizo hilo, hali itakuwa mbaya zaidi mahospitalini.
“Tumeamua kusitisha kuendelea na kazi, kwa sababu sisi tumeingia kama kawaida kazini tumefanya kazi mpaka sasa 5, lakini hakuna madaktari, na kazi zetu huwa tunafanya kama teamwork (kwa umoja), hatuwezi peke yetu,” alisema Magesa.
Aliongeza: “Pia tumepokea kwa masikitiko makubwa sana kauli ya Waziri Mkuu ya kutangaza kuwafukuza kazi madaktari walio katika mgomo kwamba, atawaleta madaktari wanajeshi. Tunaomba aifute kauli hiyo na arudi tena katika meza ya mazungumzo na madaktari ili tatizo hili litatuliwe. Tunaamini anao uwezo mkubwa wa kutatua jambo hili. Asitumie jazba kutatua matatizo haya.”
“Pia tunawaomba madaktari nao wakubali kukaa katika mazungumzo”.
Alisema hawakubaliani na uamuzi wa serikali wa kutaka kuwapeleka madaktari wanajeshi kazini, kwani hawaamini utendaji wao wa kazi.
“Kwa kweli hatukubaliani na uamuzi wa serikali kuwaleta madaktari wanajeshi kazini. Tumewahi kushuhudia mwaka 2005. Utendaji wao sio mzuri. Vitu vingi hawajui. Kwa hiyo, mara nyingi walikuwa wanatuuliza sisi. Hivyo, kazi kubwa inakuwa inatuelemea sisi,” alisema Magesa.
Aliitaka serikali kutoa kauli juu ya uundwaji wa kurugenzi ya wauguzi ndani ya siku moja, ambayo itakuwa inashughulikia matatizo yao.
WATU 10 WAFA JANA
Mwenyekiti huyo wa Tanna, alisema miongoni mwa athari zilizotokea, ni pamoja na vifo vya watu 10 vilivyotokea hospitalini hapo jana.
Alisema hadi wakati anazungumza na waandishi wa habari maiti hizo zilikuwa hazijathibitishwa na daktari kwa maana hiyo zilikuwa wodini.
Kutokuthibitishwa kwa vifo hivyo kunatokana na mgomo wa madaktari ambao wameendelea na mgomo wao jana.
HOSPITALI YA OCEAN ROAD
NIPASHE ilitembelea Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kushuhudia madaktari wakiendelea na kazi kama kawaida, huku wagonjwa wakipatiwa huduma.
Mmoja wa maofisa waandamizi wa hospitali hiyo ambaye alikataa kutaja jina lake, alisema kimsingi hospitali hiyo haikuwahi kuwa na mgomo tangu mgomo wa madaktari katika hospitali nyingine uanze hivi karibuni.
Hata hivyo, alisema kilichoikumba hospitali hiyo ni ‘upepo’ wa mgomo huo, ambao uliitikisa kidogo baada ya madaktari wake kupatwa na kitu kama bumbuwazi. 
“Hata leo (jana) walikuja maofisa kutoka Wizara ya Afya, wakashuhudia madaktari wote wa hapa wakiwa wamesaini mahudhurio na kuendelea na kazi,” alisema.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dk. Twalib Ngoma, alipotafutwa na NIPASHE jana, hakupatikana na kwa mujibu wa Katibu Muhtasi wake, alikuwa akihudhuria kikao cha menejimenti.
HOSPITALI ZA MANISPAA
Katika Hospitali ya Mwananyamala, NIPASHE ilishuhudia madaktari walioajiriwa na serikali wakiendelea na kazi kama kawaida, lakini madaktari 18 wa mazoezi kwa vitendo hawakufika kazini.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Dk. Gunini Kamba, alithibitisha suala hilo.
Alisema mbali na hilo, karibu vitengo vyote vya huduma hospitalini hapo, ikiwamo maabara na tiba ya meno, viliendelea kutoa huduma kwa wagonjwa kama kawaida.
NIPASHE ilitembelea katika vyumba vya madaktari na kushuhudia wakiendelea na kazi kama kawaida.
Hospitali ya Temeke, karibu madaktari wote walioajiriwa na serikali waliendelea na kazi, isipokuwa watano walioko kwenye mazoezi ya vitendo.
Akizungumza na NIPASHE jana, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Margareth Nyalile, alisema madaktari hao walifanya kazi kama kawaida na hakuna aliyeripotiwa kusaini na kuondoka katika eneo la kazi. 
Katika Hospitali ya Amana, iliyoko Ilala, jijini Dar es Salaam, madaktari waliendelea na kazi kama kawaida.
Baadhi ya ndugu za wagonjwa walithibitisha kupatiwa huduma jana.
KCMC
Mkoani Kilimanjaro katika hospitali ya Rufaa KCMC, hali ya utoaji huduma si yakuridhisha kutokana na mgomo baridi unaoendelea, kwa madaktari walio kwenye mgomo kuorozesha majina kwenye daftari la mahudhurio na kisha kwenda nyumbani na wengine kuonekana wakirandaranda katika eneo la hospitali hiyo, bila kuwahudumia wagonjwa.
Wakati hali ikiwa hivyo, uongozi wa hospitali hiyo umesema kuwa hali ni shwari na hakuna mgomo, ambapo hadi ilipofika saa 5 asubuhi, madaktai wote walikuwa wamejiorozesha na hata walipofanya sensa kwenye maeneo yao ya kazi waliwakuta wakiwajibika kwa mujibu wa taratibu.
Aidha, baadhi ya wagonjwa waliozungumza na NIPASHE walisema wapo ambao wamefika hospitalini humo tangu saa 12 asubuhi, lakini hadi saa kumi jioni walikuwa hawajafanikiwa kumuona daktari huku wengine wakiamua kwenda nyumbani baada ya kukata tamaa ya kupata huduma.
Baadhi ya madaktari waliozungumza na NIPASHE wakiwa katika eneo la mgahawa mmoja hospitalini humo, walisema kuwa kauli za Waziri Mkuu Pinda si za kuridhisha bali zilizojaa ubabe bila kutaka kujua tatizo na madai ya msingi ya madaktari hao.
Alisema hawatafanya kazi inavyotakiwa bali wataandika majina na kuonekana wapo kazini, lakini hawatawaona wagonjwa.
“Serikali imejibu kwa ubabe haijataka kujua kiini cha madai yetu na jinsi ya kufikia kwenye mazungumzo bali inatumia ubabe na kututishia kutufukuza na kuleta madaktari wa Jeshi, nasi hatutafanyakazi bali tutatimiza wajibu wa kuandika majina kama tulivyofanya leo na sasa tupo majumbani, tuna wajibu wakuhudumia maisha ya mwanadamu lakini katika mazingira ya kutujali na si kutuburuza,” alisema daktari mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Nao baadhi ya wagonjwa waliokuwa katika eneo la mapokezi ya wagonjwa wa nje, walisema kuwa mgomo huo umewathiri na kusababisha baadhi ya watu kupoteza maisha kwa kukosa huduma za afya.
“Serikali kutowasikiliza madaktari ni sawa na kucheza na maisha ya Watanzania, tunaoumia ni sisi na si viongozi wa serikali maana wao wakiugua wanaenda kutibiwa Ulaya au India,” alisema mgonjwa mmoja.
Naye, Anna Thadei ambaye amejifungua, alisema alitakiwa awe ametoka hospitalini humo tangu juzi, lakini hakuna daktari kwa ajili ya kutoa ruhusa, hali inayomlazimu kubakia hospitalini kwa siku mbili zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dk. Moshi Ntabaye, alisema huduma zinaendelea vizuri na kwamba kati ya madaktari ambao wapo kwenye mafunzo ya vitendo 83, madaktari 53 na wanaochukua shahada ya uzamili watatu ndio walikuwa kwenye mgomo ila wawili wapo kazini.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwa mmoja wa watumishi wa hospitali hiyo zinaeleza kuwa hali ya utoaji huduma si ya kuridhisha kwani madaktari waliopo ni wachache ikilinganishwa na idadi ya siku zote.
DODOMA WAREJRA KAZINI
Mkoani Dodoma, watumishi wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, wamesalimu amri baada ya kusitisha mgomo wao uliodumu kwa takribani wiki moja na kuingia kazini.



Watumishi waliokuwa wamegoma ni madaktari, wauguzi, maabara, wafamasia na wa kada ya afya wakidai kuboreshewa mazingira ya kazi na afya.





Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Godfery Mtei, alisema tangu jana asubuhi  wamepokea wagonjwa wa nje zaidi ya 150 na akina mama wajawazito zaidi ya 30, baadhi wamejifungua kwa njia ya kawaida wengine kwa upasuaji.  



Naye, Muuguzi katika wodi ya wazazi namba 17, Asha Chambi, alisema hakuna tena mgomo hospitalini hapo na watumishi wanaendelea na kazi kama kawaida.



Hata hivyo, kiongozi wa kuratibu madai ya watumishi hao anashikiliwa na polisi kwa kosa la kushinikiza mgomo.
Hata hivyo, Mganga Mkuu hakutaka kulizungumzia hilo. 
NIPASHE ilipomtafuta mwenyekiti ambaye anashughulikia madai ya watumishi wa hospitalini hapo, Dk. Yahya Magaso simu yake ya mkononi iliita bila ya kupokelewa. 
MBEYA KWASUASUA
Mkoani Mbeya ni madaktari watano tu waliotii amri ya Serikali kati ya 75 waliokuwa wamegoma; katika Hospitali ya Rufaa Mbeya huku wengine wakindelea na mgomo.
Hata hivyo, waandishi wa habari walipotembelea Hospitali ya Rufaa Mbeya walishuhudia mgomo wa madaktari hao ukiendelea na madaktari watano tu ndio waliokuwa wamesitisha mgomo wao.
Wakizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo huku wakiwa wamekaa vibarazani, baadhi ya madaktari hao (majina tunayo), walisema kamwe hawawezi kurejea kazini hadi pale serikali itapotekeleza madai yao.
Mkurugenzi wa Hospitali hiyo ya Rufaa Mbeya, Eleuter Samky, alisema kuwa hadi majira ya saa saba mchana jana ni madakrtari watano tu kati ya 75 walikuwa katika mgomo huo ndio walikuwa wamekubali kurejea kazini.
“Kwa kweli hali bado ni mbaya kwa kuwa mgomo bado unaendelea, hapa kwetu ni madaktari watano tu kati ya 75 ambao wameweza kufika kazini kabla ya saa nne asubuhi, kwetu hili bado ni tatizo,”alisema Dk. Samky.
Alisema kuwa kutokana na mgomo huo hata huduma zinazoendelea kutolewa hospitalini hapo ni zile za dharura ambazo hutolewa na madaktari bingwa wakati zile za kawaida zimeendelea kusitishwa kutokana na kutokuwepo kwa madaktari wa kutosha.
TANGA HAKIJAELEWEKA 
Askari Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walionusurika kufa katika ajali iliyotokea kwenye msafara wa Makamu wa rais Dk. Mohamed Gharib Bilal  hawajatibiwa kwa kile kilichoelezwa kukosa Sh. 3,000 kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa picha X-Ray.



Kadhalika, wagonjwa waliyolazwa katika wodi mbalimbali za hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo wameondoka na kuacha vitanda vikiwa havina watu kwa kile kilichoelezwa mgomo baridi wa madaktari na hivyo kukosa huduma.
Askari hao PC Kaunguru Jastine, PC Nyamsagaria Bituro na PC Magesa Mnanka wamelazwa katika hospitali Bombo baada ya kuhamishwa kutoka hospitali ya Wilaya ya  Korogwe (Magunga) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi.
Wakizungumza kwa tabu katika wodi ya majeruhi, askari hao walidai kuwa baada ya kufikishwa hospitalini hapo hawajapata matibabu mpaka sasa licha ya mabosi wao kuhangaika ili kuhakikisha wanapata tiba.
Askari PC Jastine alieleza kuwa matibabu ya X-Ray ambayo alitakiwa kufanyiwa yamekwama baada ya kushindwa kulipia Sh. 3,000 za gharama ya huduma hiyo.
Uchunguzi uliyofanywa na NIPASHE hospitalini hapo umebaini kuwa hakuna wagonjwa waliyolazwa na hivyo vitanda vya wodi hizo kubaki vitupu jambo ambalo si kawaida.
Uchunguzi huo umebaini pia kuwa wagonjwa hao wameondoka ama kutoroshwa na ndugu na jamaa zao kwa kile kilichoelezwa kuwanusuru na kifo baada ua kukosa huduma kwa muda mrefu.
Ofisa muuguzi wa wodi ya wanawake, Fatuma Katala, alipotakiwa kueleza sababu za wodi hiyo kubaki na wagonjwa wanne tu na kwamba wamekimbia mgomo wa madaktari, alisema wengi wameruhusiwa baada ya afya zao kuimarika na wala si kwa ajili ya mgomo.
Wodi ya watoto ilikuwa na wagonjwa wawili tu huku nyingine zikionekana kuwa wazi na hivyo kuzifanya wodi hizo kuwa kama maghala yaliyohamwa na kutelekezwa.
Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Fred Mtatifikolo, alikataa kuzungumzia hali hiyo kwa maelezo kuwa kamati ya ulinzi na usalama inatembelea hospitalini hapo na hivyo yupi katika maandalizi ya kuipokea.



Chadema waonya
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemtaka serikali kuacha vitisho na matumizi makubwa ya vyombo vya dola kwa madaktari waliogoma.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, ilisema vitisho hivyo vimetakiwa kukomeshwa na serikali kwa makundi mengine katika jamii yanapotumia uhuru wa kikatiba.
Mnyika alisema kila mtu ama kundi lina uhuru wa kukusanyika, kujadiliana na kuhoji kuhusu uwajibikaji wa serikali na viongozi wake kwa kuzingatia ibara za 8, 18 na 20 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkurugenzi huyo alitoa mwito Tughe, MAT pamoja na kamati ya muda ya madaktari kutoa ushirikiano unaostahili kwa Chadema pamoja na kambi rasmi ya upinzani ili kuweza kuunganisha nguvu ya pamoja katika kushughulikia madai ya msingi ya madaktari.
MADAKTARI WANENA
Nao madaktari jana walisisitiza msimamo wao wa kuendelea na mgomo, huku wakipinga kauli ya Pinda.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka, alisema wanaendelea na mgomo kama kawaida.
Alisema kitendo cha Pinda kupiga marufuku mikutano ya madaktari hakina uhusiano na mgomo wao.
Dk. Ulimboka alisema wanaendelea na taratibu za kisheria kupinga tamko la Pinda la kuwazuia kukutana kujadili kuhusu maslahi yao.
Alisema Pinda hana mamlaka ya kuzuia mikutano ya ndani au ya nje kufanyika kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
Pia alisema hakuna sheria inayosema mtu akikosa kwenda kazini siku moja afukuzwe kazi. 
“Hapo ndipo tunapomtaka aanze kutufukuza,” alisema Dk. Ulimboka.





Aliongeza: “Nimemshaangaa Pinda. Yeye badala ya kutatua matatizo ya madaktari anabaki akitafuta CV (wasifu) yangu na badala yake kuwafanya wananchi wakiendelea kuteseka wakati alitakiwa kujibu hoja zao na madaktari kuendelea na kazi.”   


Alisema kwa sasa hawapo tayari kukaa meza moja na serikali kwa ajili ya mazungumzo mpaka hapo watakaporuhusiwa kuendesha vikao vyao kwani kwa sasa mawasiliano yao yamezuiwa.
Imeandaliwa na Beatrice Shayo, Elizabeth Zaya, Gwamaka Alipipi, Moshi Lusonzo na Muhibu Said, Dar; Salome Kiomari Moshi; Emmanuel Lengwa, Mbeya; Dege Masoli, Tanga na Jackline Massano, Dodoma.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Inashangaza viongozi hawaliangalii hili swala kwa ukaribu kama wafanyavyo when it's time to discus about their posho au kwa vile mgomo huu nini kwa hospital za walala hoi tu?!! Wawo bado wanapata huduma kama kawaida nje naye ndani yako nchi, nadhani wakati umefika kwa watanzania kuamka na kuwawajibisha hawa mafisadi