ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 31, 2012

Zec yatupa pingamizi la CUF, Chadema dhidi ya Raza



Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetupiliambali pingamizi lililokuwa limefunguliwa na mgombea wa CUF dhidi ya mgombea wa (CCM), Mohammed Raza, katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Uzini mkoa wa Kusini Unguja. 
Uchaguzi huo mdogo unatarajia kufanyika Febuari 12, mwaka huu kufuatia kifo cha aliyekuwa mwakilishi wa jimbo hilo khamis Mussa Silima aliyefariki kwa ajali ya gari oktoba mwaka jana huko mkoani Dodoma. 
Akizungumza na NIPASHE msimamizi wa uchaguzi huo, Mussa Ali alisema baada ya ZEC kukutana na kujadili rufaa ya mgombea wa CUF, wamekubaliana na maamuzi ya awali yaliyokuwa yametolewa na ZEC Wilaya kuwa pingamizi lililokuwa limefunguliwa limekosa mashiko ya kisheria. 
“Tayari nimepokea maamuzi ya ZEC kuwa Raza ni mgombea halali katika uchaguzi mdogo wa uzini,” alisema. 

Alisema baada ya uamuzi huo wa Raza na chama chake sasa wanaruhusiwa kuendelea na kampeni. 
Chama cha Mapinduzi kilisitisha kampeni zake kimya kimya Januari 28 baada ya wagombea wa CUF na Chadema kukata rufaa ZEC wakipinga maamuzi ya tume hiyo ngazi ya Wilaya Zanzibar. 
Alisema ZEC baada ya kupitia rufaa ya mgombea wa CUF na Chadema, imebaini hazikuwa na nguvu za kisheria kwa mujibu wa sheria ya tume ya uchaguzi ya Zanzibar. 
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya maamuzi hayo ya ZEC, Mkuu wa kitengo cha Idara ya Itikadi na uenezi CCM visiwani hapa, Ali Mwinyi Msuko, alisema chama hicho kinatarajia kuzindua kampeni zake kesho. 
Alisema kampeni hizo zinatarajiwa kuzinduliwa na Makamu Mwenyekiti wake Amani Abeid Karume katika uwanja wa Ghana katika Jimbo la Uzini. 
Awali wagombea wa CUF Salma Hussen Zarali na wa Chadema, Ali mbarouk Mshimba, walifungua pingamizi ngazi ya Wilaya, kabla ya kutupiliwa mbali na kuamua kukata rufaa. 
Katika madai yao wagombea hao walisema kiapo cha Mgombea Raza kilifanyika kinyume na sheria ya uchaguzi ya namba 11 ya Mwaka 1984 na marekebisho yake kifungu cha 46(3)(a) cha sheria ya uchaguzi ya Zanzibar. 
Walisema Raza alitakiwa aape mbele ya hakimu kwa mujibu wa kifungu cha sheria hiyo badala yake alikula kiapo kwa Jaji wa Mahakama Kuu pamoja na kutoambatanisha stakabadhi ya gharama za kiapo chake alizotumia Mahakamani. 
CHANZO: NIPASHE

No comments: