Advertisements

Tuesday, January 31, 2012

Mkwasa aihofia Ethiopia

Kocha wa timu ya taifa ya soka ya wanawake
(Twiga Stars), Charles Boniface Mkwasa



Kocha wa timu ya taifa ya soka ya wanawake (Twiga Stars), Charles Boniface Mkwasa, amesema kuwa watalazimika kufanya maandalizi makali zaidi kabla ya kuwavaa Ethiopia katika mechi ijayo ya kuwania kufuzu fainali za wanawake za Kombe la Mataifa ya Afrika kwani ushindi wao wa mabao 6-4 dhidi ya Misri unaonyesha kuwa sasa wameimarika kuliko ilivyokuwa hapo kabla.
Akizungumza na NIPASHE jana, Mkwasa alisema kuwa hofu waliyo nayo, na ambayo itamlazimu yeye na kikosi chake kufanya maandalizi makali zaidi kabla ya kucheza raundi inayofuta, ni matokeo ya kusisimua ya ushindi wa mabao 4-0 walioupata Ethiopia katika mechi yao ya marudiano dhidi ya Misri juzi jijini Addis Ababa, ikiwa ni wiki mbili tu baada ya timu hiyo ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kulala ugenini Misri kwa mabao 4-2 na kuonekana awali kuwa ni kama wameshatolewa.

Mkwasa ambaye kikosi chake kilifuzu kwa hatua ijayo baada ya kushinda kwa jumla ya mabao 7-2 dhidi ya Namibia, alisema kuwa Ethiopia si ngeni kwao kwani wameshawahi kucheza dhidi yao na mara zote Twiga walionekana wazuri zaidi na kupata matokeo ya jumla ya ushindi.
Hata hivyo, Mkwasa aliongeza kuwa ufahamu wake wa awali kuhusiana na Ethiopia ni kwamba hawatishi sana na wenghi waliamini kuwa wasingeweza kubadili matokeo ya awali ya kuwa nyuma kwa mabao 4-2 na kisha kushinda 4-0 dhidi ya timu kali ya Misri.
“Matokeo haya yanaonyesha kwamba Ethipia wamebadilika sana… kiwango chao kitakuwa kimeimarika zaidi na sio sawa na kile tunachokifahamu sisi. Hilo ndilo linalonifanya mimi na wenzangu kuchukua tahadhari mapema kwani tunajua kuwa mechi hiyo haitakuwa rahisi,” alisema Mkwasa.
Mkwasa alisema kuwa kabla ya kuwavaa Ethiopia, watalazimika kuanza maandalizi yao mapema na akawataka Watanzania waendelee kuwaunga mkono kama walivyofanya juzi uwanjani wakati walipoishangilia timu hiyo kuanzia mwanzo wa mechi hadi mwisho.
“Kitakachotusaidia kuvuka raundi inayofuata ni maandalizi makini tu… tunatakiwa kuanza maandalizi mapema. Tunawashukuru sana wananchi na tunaomba waendelee kuiunga mkono timu yao ili vijana waendelee kuwapa raha,” alisema Mkwasa.
Mechi ya kwanza ya Twiga dhidi ya Ethipia kuwania kufuzu fainali za Afrika zitakazofanyika Novemba nchini Equatorial Guinea itachezwa Mei jijini Addis Ababa, Ethiopia na marudiano yatafanyika wiki mbili baadaye jijini Dar es Salaam.
KOMBE LA DUNIA
Katika hatua nyingine, Mkwasa alisema kuwa endapo serikali na wadau wote wa soka watashiriki kikamilifu kuwekeza katika soka la wanawake, anaamini kwamba kuna siku,  kikosi cha Twiga kitaandika historia mpya nchini kwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkwasa alisema kuwa umefika wakati serikali ambayo ndiyo msimamizi wa kila jambo, kuitazama Twiga kwa karibu zaidi na ikiwezekana, iache utaratibu wa sasa wa kujitokeza siku za mwisho za maandalizi kwa sababu hali hiyo huenda ikawarudisha nyuma wachezaji ambao wanatumia muda mwingi kuitumikia nchi.
Mkwasa alisema kuwa Twiga Stars ina njia fupi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia tofauti na mechi za wanaume ambazo huwa ni nyingi na ushindani wake ni mkubwa zaidi kwani timu nyingi za upinzani huundwa na nyota wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya.
"Bado misaada inahitajika katika timu ya Twiga, uwekezaji ndio utakaofanikisha ndoto za Watanzania kutimia kwa sababu kucheza mashindano ya Dunia kwa wanawake ni jambo linalowezekana kama misingi itakuwepo," alisema kocha huyo ambaye pia anaifundisha klabu inayoshiriki ligi kuu Bara ya Ruvu Shooting.
"Wachezaji wako imara, wanajituma na kama watapewa heshima inayolingana na kazi wanayoifanya, nina uhakika Watanzania watazidi kufurahi… nafurahi kuona wote wana nidhamu na hiyo ndio moja ya siri ya mafanikio yetu," aliongeza.
Wakati huohuo, Mbunge wa Jimbo la Ilala jijini Dar es Salaam, Mussa Zungu, aliungana na Mkwasa kwa kusema kwamba serikali ndiyo yenye wajibu wa kusimamia maandalizi ya timu za taifa na mafanikio ambayo yanaonyeshwa na wachezaji wa Twiga yanawafanya waone aibu.
Zungu alisema kwamba hakuna timu ya taifa iliyofanikiwa bila ya mchango wa serikali hivyo akaitaka iweke fungu maalumu la maandalizi ya timu za taifa na si kusubiri kuungana pale mafanikio yanapopatikana.
Wachezaji wa timu hiyo walivunja kambi jana na kesho wamepata mwaliko maalum wa kutembelea kituo cha televisheni cha ITV ambacho mara kwa mara kimekuwa kikiendesha kampeni kali za kuhamasisha wananchi kuichangia kwa hali na mali katika wakati wa maandalizi ili ifanye vizuri.
CHANZO: NIPASHE

No comments: