ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 31, 2012

Nahodha: Sitta lete ushahidi wa Mwakyembe

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha amemtaka Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta kuwasilisha ushahidi wa madai aliyoyatoa juzi kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe alilishwa sumu. 
Juzi akiwa na kundi la makada wenzake wa CCM wanaojipambanua kuwa wapambanaji wa ufisadi, katika uzinduzi wa Programu ya Neno la Hekima kutoka kwa Kiongozi iliyoanzishwa na Kanisa la Ufufuo na Uzima, Sitta alirejea kauli yake ya awali kuwa Dk Mwakyembe ambaye pia Mbunge wa Kyela, alilishwa sumu
.
“Nasema Dk Mwakyembe kapewa sumu. Kama vyombo vya uchunguzi vinasema siyo, basi watueleze ukweli, tena haraka,” alisema Sitta na kushangiliwa na maelfu ya waumini wa kanisa hilo na kuongeza:

“Vipi uone binadamu ambaye ukimshika katika ngozi unga unamwagika chini, mhudumu anakuja kuufagia lakini baada ya saa moja unarudi tena, kitu hicho siyo cha kawaida. Wamejaribu, wameshindwa kwa kuwa Dk Mwakyembe analindwa kwa jina la Yesu ambalo ni kubwa kuliko yote.

Kwa hiyo nuksi, kurogwa kuwekewa sumu ni kama maji katika mgongo wa bata, yanatiririka tu na kwenda zake.”  Alisema mafisadi wapo kwa ajili ya kuangamiza taifa na kuwaangamiza viongozi wanaotetea maslahi ya wananchi akidai kwamba sasa siku zao zina hesabika. Akizungumza jana, Vuai alisema ushahidi ukija suala hilo linaweza kuchunguzwa huku akihoji:

“Ulimwuliza Sitta kama ana uhakika.”  Hata hivyo, Vuai alisema masuala yote yanayohusu uchunguzi hayawezi kuzungumzwa katika vyombo vya habari na kwamba ni mambo ambayo hufanyika kwa umakini mkubwa... “Labda  nikueleze kitu... hilo suala unalolisema mimi sijalisikia ila kama amezungumza hivyo basi alete ushahidi.”

“Kwanza hilo jambo la Sitta kusema Mwakyembe kalishwa sumu unaniuliza mimi? Kwa nini usimtafute huyo Sitta ili akueleze vizuri ili ujiridhishe?”  Alisema suala kama hilo linapotokea na mhusika akawa na ushahidi anatakiwa kuuwasilisha sehemu husika na kwamba kuzungumza kitu bila kuwa na ushahidi haisaidii huku akisisitiza kuwa  mpaka sasa hakuna mtu yoyote aliyejitokeza kutoa madai hayo.

Dk Mwakyembe aliondoka nchini Desemba 9, mwaka jana kwenda katika Hospitali ya Appolo, India kwa matibabu baada ya kuugua maradhi yaliyosababisha ngozi yake kuharibika na tangu arejee nchini juzi ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kuonekana katika hadhara ya watu.

Wengine waliohudhuria uzinduzi huo ni Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Kahama, James Lembeli, Mbunge wa Viti Maalumu Mbeya, Hilda Ngoye, aliyekuwa Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro na Mjumbe wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Mkoa wa Kilimanjaro , Paul Makonda.   Mbali ya kuapa kuendeleza mapambano dhidi ya mafisadi, Dk Mwakyembe pia alisema:

“Nilifika hospitalini Oktoba 10 (mwaka jana), na tangu wakati huo sikuweza kuvaa viatu lakini leo hii naweza kuvaa viatu, kwa hiyo shetani ameshindwa.”  Alisema atatumia siku za Jumapili kuzunguka katika makanisa mbalimbali kwa lengo kumkemea shetani.

Mwananchi

No comments: