ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 12, 2012

Serikali yarejesha mchujo Kidato II

Wanafunzi wakifanya mitihani siku za hivi karibuni
ADA YA MTIHANI SH 10,000, KIDATO CHA NNE, SITA 35000 ANAYESHINDWA MARA MBILI KUFUKUZWA 
Fredy Azzah na Boniface Meena
 SERIKALI imerejesha mchujo kwenye mtihani wa kidato cha pili, ikisema kuanzia mwaka huu wanafunzi watakaopata wastani wa chini ya alama 30 katika masomo yote, watalazimika kurudia darasa.Katika uamuzi huo, ada ya mtihani wa kidato cha pili imerejeshwa na itaendelea kuwa Sh10,000 na ada kwa mitihani ya kidato cha nne na sita ni Sh35,000.
Tamko hilo la Serikali lilitolewa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo akisema Serikali imerudisha makali ya mtihani wa kidato cha pili baada ya  kuona ufaulu wa wanafunzi katika kidato cha nne unashuka kwa asilimia kubwa. “Matokeo ya mtihani wa kidato cha pili hupewa uzito mkubwa katika matokeo ya jumla ya mtihani wa kidato cha nne kama sehemu ya upimaji endelevu,” alisema na kuongeza: 


“Hivyo, kuanzia mwaka huu mwanafunzi atakayepata wastani wa chini ya asilimia 30 katika mtihani wa kidato cha pili hataruhusiwa kuendelea na kidato cha tatu.” “Mwanafunzi huyo atatakiwa kukariri (kurudia) kidato cha pili na fursa hii itatolewa mara moja tu. Atakayekariri kidato cha pili na kushindwa kufikia wastani wa asilimia 30 ataondolewa katika mfumo rasmi wa elimu.”

Waziri huyo alisema mtihani wa kidato cha pili ulianzishwa mwaka 1984 kwa madhumuni ya kutathmini maendeleo ya wanafunzi baada ya miaka miwili ya elimu ya sekondari. “Mtihani huu ni tathmini ya kati inayopima kiwango cha maarifa na ujuzi alioupata mwanafunzi kutokana na masomo aliyojifunza katika kidato cha kwanza na cha pili,” alisema na kuongeza:

“Mtihani wa kidato cha pili ni njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa wadau wote wakiwemo wanafunzi, walimu na wazazi wanawajibika ipasavyo katika utoaji wa elimu ambapo kwa kufanya hivyo, tutapata wanafunzi wazuri na kuweka misingi bora ya wanafunzi katika kujifunza.”

 Alisema  mwaka 2008 Serikali ilitamka kuwa wanafunzi ambao hawatapata alama 30 katika mtihani wa kidato cha pili hawatarudia  darasa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, badala yake ataendelea na masomo ya kidato cha tatu na atapatiwa mafunzo rekebishi.
“Hata hivyo, uchunguzi uliofanyika mwaka 2011, kuhusu ufaulu duni wa wanafunzi katika mtihani wa kidato cha nne, 2010 umebaini  moja ya sababu za wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani ya kumaliza kidato cha nne ni kutokana na kuwaruhusu wanafunzi kuendelea na masomo hata baada ya kushindwa kufikia alama ya ufaulu iliyowekwa katika mtihani wa kidato cha pili,” alisema.

Mulugo alisema takwimu zinaonyesha kuwa ufaulu wa mtihani wa kidato cha pili umekuwa ukishuka mwaka hadi mwaka kuanzia 2008 hadi 2010, jambo linaloashiria kuwa wanafunzi na walimu hawafanyi bidii katika kujifunza na kufundisha.

Gharama kama 1984 Mtihani wa taifa wa kidato cha pili pia umekuwa ukigharimiwa na Serikali tangu ulipoanzishwa mwaka 1984 hadi 1994 ulipositishwa na ulirejeshwa mwaka 1999 na wazazi walichangia gharama za uendeshaji hadi mwaka 2009, wakati Serikali ilipoamua kuugharimia kwa kusitisha ada ya mtihani kwa shule za Serikali. “Hata hivyo uendeshaji wa mtihani huu umekuwa mgumu kutokana na ongezeko la gharama za uendeshaji linalokwenda sambamba na ongezeko la idadi ya shule pamoja na wanafunzi mwaka hadi mwaka.

Ongezeko hilo linafanya gharama za uendeshaji kuwa kubwa,” alisema Malugo.  Alisema kutokana na ongezeko hilo la gharama za uendeshaji wa mtihani huo, wazazi na walezi watatakiwa kuchangia kuanzia mwaka huu kwa kiwango hicho cha Sh10,000 kwa kila mwanafunzi kwa shule zote, za Serikali na zisizo za serikali. 

Kidato cha nne Naibu Waziri huyo alisema pamoja na kuchangia mtihani wa taifa wa kidato cha pili, wazazi na walezi watapaswa kuchangia pia gharama za uendeshaji wa mitihani ya taifa ya kidato cha nne na sita kuanzia mwaka huu kwa kiwango hicho cha Sh35,000 kwa kila mwanafunzi kwa shule zote, za Serikali na zisizo za serikali.
“Ikumbukwe kuwa gharama hizi ni zile ambazo wazazi na walezi walikuwa wakichangia kati ya mwaka 1999 na 2009 kabla ya Serikali haijaamua kusitisha uchangiaji huo,” alisema Mulugo. Tangu kufutwa kwa utaratibu huo wa zamani kwa wanafunzi wa kidato cha pili, wadau mbalimbali wa elimu wamekuwa wakipiga kelele wakipinga wakisema uamuzi huo umekuwa ukichangia kuzorota kwa elimu nchini.

MWANANCHI

No comments: