Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya |
Siku chache baada ya Chama cha Madaktari nchini (MAT) kutangaza mgogoro na serikali na kuipa saa 72, serikali imetangaza kuwa ipo tayari kukaa nao meza moja na kuzungumzia masuala ya sekta ya afya.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya, alitoa kauli hiyo jana na kusema kuwa serikali ipo tayari kukaa na MAT kuzungumza kama watakuwa tayari.
Dk. Nkya alisema sakata la madaktari 1,994 waliokuwa katika mazoezi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili waliamua kutoendelea na ratiba zao za mazoezi kwa vitendo baada ya kucheleweshewa posho zao za kila mwezi.
Alisema baada ya kuchelewa kutolewa kwa fedha za posho, wizara ilifanya jitihada ya kuhakikisha fedha hizo zinapatikana haraka.
Alisema serikali ilikuwa ikitoa taarifa katika taasisi walizokuwa wakifanyia kazi kuhusiana na jitihada zinazofanywa ili kutatua tatizo hilo.
“Ieleweke kwamba wataalamu hawa huingia mikataba na hospitali husika na mkataba wanaoingia umeainisha hawatakiwi kugoma au kuanzisha mgomo,” alisema Dk. Nkya.
Dk. Nkya alisema pamoja na wizara kufanya jitihada hizo kuwa suala lao limefanyiwa ufumbuzi, lakini bado walishikilia msimamo wao wa kutorudi vituoni hadi wapokee fedha na kwamba jambo hilo halikuwa la kiungwana.
Alisema baada ya kuona hivyo, wizara ilipeleka wataalamu 51 waliokuwa wakisubiri kuanza mafunzo Januari mwaka huu ili kuchukua nafasi za wataalamu waliokataa kurejea katika hospitali hiyo kwa ajili ya kuzuia athari ambazo zingeweza kujitokeza kwa wagonjwa. Hata hivyo, alisema katika mgomo huo kuna wenzao 60 ambao hawakugoma.
“Baadhi ya wataalamu waliokuwa wakifanya mazoezi katika vituo kama vya Hospitali ya KCMC, Mount Meru, Bombo, Bugando na Manispaa za Dar es Salaam walitambua jitihada za wizara za kushughulikia tatizo hilo na waliendelea na ratiba yao ya mazoezi kwa vitendo,” alisema.
Alisema waliogoma uongozi wa Muhimbili uliwachukulia hatua na kuwaandikia barua kuwarudisha wizarani na kutaka wapatiwe wataalamu hao.
“Ili kuhakikisha wataalamu hao wanafikia malengo ya mazoezi ya vitendo wizara imeamua kuwapanga katika hospitali mbalimbali ikiwemo Muhimbili, Temeke, Mwananyamala, Aga khan, Amana na Lugalo kwa kuzingatia uwezo wa hospitali,” alisema.
Alisema Januari 16, mwaka huu wataalamu 194 walikuwa wamepewa barua na wameripoti katika vituo walivyopangiwa.
Alisa wizara yake imepata taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa MAT imewapa saa 72 iwarudishe madakatari hao katika hospitali ya Muhimbili pamoja na kutaka kuondolewa kwa baadhi ya viongozi wa wizara.
Hata hivyo, alisema tamko hilo halijawasilishwa rasmi wizarani na kusisitiza kuwa madakatari hao hawajafukuzwa kufanya mazoezi bali wamepangiwa vituo vingine.
Akizungumzia uamuzi wa MAT kumvua uanachama Mganga Mkuu wa Serikali, Deo Mtasiwa, Dk. Nkya alisema chama hicho hakiwezi kumchukulia hatua bali chombo chenye mamlaka ni Wizara.
Rais wa MAT, Dk. Namala Mkopi, alisema suala hilo watalizungumzia leo na kwamba tamko walilolitoa Jumamosi sio lazime lipelekwe wizarani ndio maana walitoa taarifa kupitia vyombo vya habari.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment