ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 18, 2012

Sitta aitabiria CCM hali ngumu


WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ametabiri kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, CCM itaendelea kupoteza majimbo ya ubunge, lakini akasisitiza kuwa bado itaongoza kwa idadi ya wabunge. 

Alisema hayo juzi katika kipindi cha Monday Agenda kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Capital na kufafanua kuwa ni suala la tabia ya asili ya baada ya kuanzisha mfumo wa vyama vingi, kwa chama tawala kupungukiwa wabunge. 

"Ukiangalia, tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza, wabunge wanapungua kidogo kidogo na ndivyo mfumo ulivyo, wanatumia udhaifu kidogo uliopo chama tawala kupata viti zaidi," alisema Sitta.
 

Hata hivyo, alibainisha kuwa CCM bado ina viongozi, wakiwamo wabunge wengi ambao wanaheshimika na hawana upinzani katika majimbo yao, ambao wataendelea kukipa chama hicho nguvu. 

"Kwa mfano, mimi katika Jimbo la Urambo Mashariki, nikiamua kugombea, waweke upinzani wasiweke nitashinda, kwa kuwa wananifahamu ni mtu wao na nimefanya mengi," alijinasibu na kuongeza kuwa viongozi wa aina yake wako wengi CCM na wataendelea kuipa nguvu. 

Kuhusu urais, Sitta alisema kama CCM itakosea kuteua mgombea urais mwaka 2015, litakuwa jambo la kusikitikia nchi. 

Alifafanua kuwa upo uwezekano wa kuwa na mtu ambaye ana nguvu ndani ya CCM, lakini nje anaonekana asiye na maadili na akikubalika kuwa mgombea wa chama hicho, nchi itapaswa kuonewa huruma. 

"Kama wataweza kununua mfumo wa chama wa kuteua mgombea urais, litakuwa jambo la kuionea huruma nchi," alisema Sitta. 

Kuhusu mvuto wa chama hicho tawala, Sitta ambaye pia ni Spika mstaafu wa Bunge, alisema umepotea kwa vijana, hasa kutokana na kukosekana kwa ajira; tatizo la kiuchumi ambalo kwa upande mmoja, halitokani na uongozi uliopo madarakani, bali hali ya kuyumba kwa uchumi wa dunia. 

Sababu ya pili ya kupotea mvuto wa CCM kwa mujibu wa Sitta, ni kukosekana kwa jitihada mpya za kuzalisha ajira na kuwapo watu wanaoishi maisha mazuri kutokana na ufisadi akitoa mfano uliosababishwa na “mikataba mibovu ya bahati mbaya”. 

Kuhusu umoja na mshikamano wa wana CCM, Sitta alisema haupo hasa kwa viongozi wa ngazi za juu na kuongeza kuwa ni jambo la kawaida katika vyama vya siasa. 

Kwa mujibu wa Sitta, sababu ni kuibuka kwa makundi mawili; la kwanza la viongozi wasiopenda mabadiliko, wanaoweka maslahi binafsi mbele na kuamini kuwa chama kinachotawala hakina tatizo. 

Kundi la pili alisema, ni la wanaoona kuwa chama kinapoteza mwelekeo, kimeacha kufuata falsafa za waasisi wa chama hicho akiwamo, Mwalimu Julius Nyerere. 

Alisema katika msuguano wa makundi hayo mawili, lazima kundi kubwa liwe la wanaotetea mwonekano mzuri wa chama kwa wananchi na kuonya; "kama chama hakitafanya yale kinachoyaamini basi kutakuwa na ombwe la kimaadili. 

Akizungumzia uhuru wa habari, Sitta alisema Tanzania ni kubwa, wanasiasa wanaweza kusema watakalo na katika mitandao ya intaneti hasa blogu, watu wanaweka chochote watakacho bila kuingiliwa na mtu. 

Hata hivyo, alisema kibaya ni matumizi mengine ya uhuru huo, ambapo watu wanasema uongo kwa makusudi na kuchafuliwa hasa viongozi aliosema ni rahisi kuchafuliwa na wao kukosa namna ya kujitetea. 

Kuhusu utaifa wa Watanzania, Sitta alitilia shaka kuwa unaweza kupotea na kutoa mfano wa Tanzania na Rwanda. 

"Wakati wa Mwalimu na hata wa Mzee Mwinyi, ilikuwa rahisi kuwataka wananchi wajitolee na wakafuata mwito wa kiongozi lakini hilo halipo leo. 

"Pale Rwanda, kuna siku iliamuliwa watu wote wajitokeze kufagia na kufanya usafi wa mazingira, lakini leo ukiwaambia Watanzania wafanye hivyo, watakucheka na kuhoji unasema nini," alisema Sitta na kuongeza kuwa kutofuatwa kwa mwito wa viongozi kutasababisha siku moja Taifa lipotee. 

Kuhusu maendeleo ya ushirikiano wa Afrika Mashariki, Sitta alisema unaendelea vizuri, lakini kwa sasa, hatua ya Umoja wa Sarafu wa kuufanya ushirikiano huo kutumia sarafu moja, umeanza kutiliwa shaka. 

Alifafanua kuwa shaka hiyo inatokana na mgogoro wa Umoja wa Ulaya (EU), uliotokana na nchi hizo kuwa katika hatua hiyo ya Umoja wa Sarafu. 

Kutokana na hali hiyo, Sitta alisema tayari baadhi ya wataalamu wameondoka kwenda Ulaya kujifunza changamoto inayokabili umoja huo katika hatua hiyo ya kutumia sarafu moja. 

Hata hivyo, alitabiri huenda umoja wa kisiasa kati ya nchi za Afrika Mashariki ukafikiwa mwaka 2020 baada ya majadiliano na utekelezaji wa kuingia katika hatua zijazo kutoka hatua ya soko la pamoja lililopo sasa. 

Sitta ni mmoja wa wabunge ambao wamekuwa wakijinasibu kupambana na ufisadi nchini na kuwa na kundi ambalo limekuwa kila likipata fursa, huzungumzia ufisadi na kutaka watuhumiwa wawajibishwe.


HABARI LEO

No comments: