ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 13, 2012

Maalim Seif: Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni imara


MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni imara na ndiyo suluhisho la matatizo ya kisiasa Visiwani. 

Maalim Seif alisema hayo jana wakati alipofungua mkutano wa siku mbili unaojadili hali ya kisiasa ya Zanzibar mara baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa uliotayarishwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chini ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET). 

Alisema mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa unaonekana waziwazi umepokelewa vizuri na kukubalika na wananchi kuwa ndiyo suluhisho la kumaliza matatizo ya kisiasa yaliyoigubika Zanzibar kwa muda mrefu. Alisema hali ya maelewano ya wananchi wa pande mbili, yameimarishwa huku wananchi wakishiriki katika ujenzi wa taifa pamoja na huduma za jamii bila ya matatizo wala kubaguana. 

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), alisema elimu zaidi inahitajika katika kipindi hiki cha mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwani wapo watu na watendaji wa Serikali ambao hawaridhishwi na kufurahishwa na hali hiyo. 


“Najua wapo watu hawapendi maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa ambayo yameunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa....msilete fitina na kuvuruga maridhiano hayo kwani wananchi ndiyo muelekeo wanaoutaka kama kura za maoni zilivyoonesha,” alieleza Maalim Seif. 

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala alisema Redet imefurahishwa na kuwepo kwa utulivu mkubwa wa kisiasa tofauti na miaka ya nyuma. 

“Sisi Redet tulikuwa mashahidi wakubwa wa hali ya kisiasa Zanzibar ambapo tulikuwa tukishuhudia kwa muda mrefu.....Serikali ya Umoja wa Kitaifa inastahili pongezi kwa kudumisha maelewano na kuondosha siasa za chuki,” alisema Profesa Mukandala. 

Redet imekuwa ukiendesha elimu na mafunzo kwa makundi mbalimbali ya vijana Zanzibar kwa lengo la kujenga siasa za kuvumiliana na kuachana na chuki na uhasama.


HABARI LEO

No comments: