Kufanya hivyo ni sawa na kuingia kwenye moyo wa mwingine, kitu ambacho hakiwezekani hata kiduchu. Kaa ukijua kwamba nafsi ya kwanza itabaki kuwa ya kwanza na ya pili itaendelea kusimama katika uhalisia wake.
Maisha ni kama picha ambayo unaijenga kwenye fikra zako. Endapo utawaza mema na kutamani kumfanyia mwenzi wako vitu vizuri, ni rahisi kutekeleza. Utakosea mno, kama utakuwa unasumbuliwa na mawazo kwamba unachokitenda, mpenzi wako naye atakaa na kufikiria kisha akutendee kama unavyomfanyia.
Kwa miaka kadhaa, nimejifunza kujua tabia za watu kwenye mapenzi na kubwa ambalo nimebaini ni kwamba saikolojia ya ndani ndiyo ambayo inaleta utata. Uhusiano wa wengi unashindwa kudumu kwa sababu hiyo. Ukweli ni kwamba ndani ya mtu, kunakuwa na matarajio ambayo hayafikiriwi upande wa pili.
Hili ni tatizo lakini linaweza kuwa kinyume chake kama mhusika ataligundua hilo na kulitafutia ufumbuzi. Kwa nini uwaze peke yako? Iweje kichwa kiume kwa tamaa ya kutekelezewa jambo ambalo linaweza kuingizwa kwenye majadiliano? Mapenzi ni kitu kinachokutanisha nafsi mbili zenye hisia tofauti, kwa hiyo inabidi kuelewana ili muende sawa.
Acha kuwaza peke yako. Mshirikishe mwenzako jinsi ambavyo wewe ungefurahi kwa namna atakavyohusika kwenye mapenzi yenu. Muelekeze cha kufanya. Mshauri muonekano ambao wewe utakupa nguvu ya kujiamini kwamba upo kwenye uhusiano salama. Usipojadiliana naye, unadhani utasaidiwa na nani?
Kosa kubwa ambalo watu wengi huwa wanafanya ni kuwaacha wapenzi wao na kwenda kujadiliana na marafiki. Mtu anaweza kuketi na rafiki yake na kumwagia lawama chungu nzima jinsi asivyofurahishwa na mwenzi wake, wakati angezungumza na mhusika mafanikio yangeonekana kwa urahisi zaidi.
Achana na tabia ya kumsengenya mwenzi wako kwa marafiki zako. Unamponda kwa yale anayofanya kwa kuona hayapo sawa lakini mapenzi hayapo hivyo. Tambua kwamba wewe pekee ndiye mwenye nafasi ya kumfanya mpenzi wako abadilike kulingana na jinsi unavyotaka. Jijengee mawazo chanya kuanzia leo.
Binadamu walivyo katika jinsi mbili tofauti, ndivyo wanavyotofautishwa na namna ya kupenda pia jinsi ya kuhusika kwenye mapenzi. Wengi huishi na maumivu kwa kuona kwamba anachowaza, hakipo kwa mwenzi wake. Mathalan, unapenda mpenzi wako akununulie zawadi, hilo lirekebishe kwa kumuelekeza kwa upole.
Mwambie: “Mpenzi wangu, napenda sana ile simu.” Zungumza hivyo halafu ukae kimya. Naye akili inafanya kazi, kwa hiyo kama uwezo unaruhusu atakununulia. Jiepusha na tabia ya kuomba jamvi msibani. Pengine hana lakini wewe unalaumu kuwa hakujali ndiyo maana hajakununulia.
Kosa lingine kubwa ambalo wengi hulifanya ni kufananisha uhusiano wa watu wengine na kutaka kulazimisha uhusika wao ufanane na wenu. Mfano; mtu anaona jinsi rafiki yake anavyotendewa na mpenzi wake, kwa hiyo naye anatamani iwe hivyo. Ni binadamu wawili tofauti, ni ngumu kuwa na tabia za kufanana. Uvumilivu unahitajika.
KUKOSEA TAFSIRI
Binadamu kila mmoja kwa namna yake, anayo njia ya kuonesha ishara za mapenzi. Hata hivyo, ipo wazi kuwa wengi hufanana pale wanapochachawa kutokana na kuzidiwa na hisia za kupenda. Kila mmoja anaruhusiwa kupenda lakini pupa zikikuzidi, ni rahisi kuonekana mapepe. Haipendezi kuonekana hivyo.
Ieleweke kuwa ipo jamii ya watu ambao wanaweza kupenda lakini wasioonesha waziwazi hisia zao. Wakakomaa kisabuni, wewe ukadhani hawapendi kumbe wanaumia ndani ya nyoyo zao. Hili likae kichwani kwako, usije ukafanya kosa kubwa la kukosea tafsiri, matokeo yake uhusiano wako ukakaa tenge.
Tambua pia kuwa ipo jamii ambayo inaweza kuonesha waziwazi kwamba wanapenda kumbe hakuna lolote. Ni uchangamfu tu uliopo ndani yao. Anaweza akawa anakujali, ukiwa mbali anakupigia simu. Ukiwa na tatizo anajitoa kukusaidia lakini hiyo haina ishara kuwa anakuhitaji kimapenzi. Ni mambo ya urafiki tu hayo.
Hivyo basi, kabla hujaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi, hakikisha huchanganyi mambo. Usimtafsiri mtu kwa alama za juujuu. Fanyia kazi kile unachohisi. Usije ukachukia kwamba mtu unayempenda anakuchukia, wakati kumbe mwenzako ndiyo swaga zake. Lazima aweke madoido kidogo kwa kuhofia kuonekana mwepesi.
Wala usije ukadandia mti ambao siyo kwa kudhani unapendwa, wakati mwenzako ni geresha tu! Chukua hatua sahihi, kabidhi moyo wako kwa yule anayekupenda, si kwa sababu akikuona anakuchekea na kujishaua, la hasha! Kaa kwa yule ambaye amedhihirisha mapenzi ya kweli kwako. Ukikosea tafsiri, utaumia mbele ya safari.
Itaendelea Jumanne ijayo.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment