Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kijiji cha Nyakaduha Wilaya ya Geita mkoani Mwanza, Aaron Yegela, ametiwa mbaroni kwa tuhuma za wizi wa dawa za binadamu zenye thamani ya Shilingi milioni mbili.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa na kuhojiwa kwa saa kadhaa na Jeshi la Polisi na baadaye kuachiwa kwa dhamana.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kuiba dawa zilizopelekwa kituoni kwake kutoka Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa.
Kwa mujibu wa Polisi wilayani Geita, mtuhumiwa huyo amefunguliwa jalada la uchunguzi namba GE/223/RB/12 na baada ya kukamilika atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.
Imedaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alifikishwa polisi na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Omary Dihenga kufuatia ukaguzi uliofanywa na Mfamasia wa Wilaya, Ramadhan Msuya kwa kushirikiana na Katibu wa Afya wa Hospitali ya Wilaya ya Geita.
Uchunguzi huo uligundua upotevu wa dawa mbalimbali zikiwemo Quenine, Amoxilin, Aspirin, Panadol na chupa za maji (drips) ambazo katika uchunguzi huo, iligundulika orodha ya mgao wa dawa zilizokutwa kwenye Zahanati ya Nyakaduha zilikuwa tofauti katika uwiano wake, hivyo kulazimika kufanyika ukaguzi wa kushtukiza Desemba 21, mwaka jana.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment