ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 4, 2012

Ndoa, mapenzi huundwa na katiba, isome ikusaidie

Na Luquman Maloto
Unajua katiba? Ni muundo wa sheria, kanuni zinazoainisha jinsi ambavyo nchi, chama au shirika vitakavyoendesha shughuli zao. Uhusiano wa kimapenzi upo katika mtindo wa kitaasisi lakini kwa bahati mbaya katiba yake haipo kwenye maandishi (non-written constitution).
Makala haya yataiweka katiba hiyo kwenye maandishi kwa ajili ya kukusaidia msomaji wangu kujua jinsi ya kuishi ndani ya uhusiano wako. Wengi wamekuwa wakipata tabu, wanapotoka na kuishi nje ya mistari inayofaa kwa sababu hawajaisoma au hawaijui.

Unahitaji muongozo wa kikatiba ili mapenzi yako yasitawaliwe na migogoro. Unatakiwa ujue jinsi ya kuishi kwa upendo na furaha. Amani itawale kwenye uhusiano, hali kadhalika tabia zako zikidhi mahitaji ya katiba ya mapenzi au ndoa yako.
Je, unatakiwa uyafanyie nini mapenzi yako au ndoa yako? Muonekano wako uweje mbele ya mwenzi wako? Ukiwa na hasira, ni kitu gani cha kufanya? Inapotokea mpenzi wako ameghadhabika, jambo lipi ufanye liweze kumrudisha kwenye mstari unaotakiwa?
Ndoa inahitaji nini? Kwa nini aliye kwenye ndoa hatakiwi kujiona ana uhuru wa kupitiliza kiasi cha kumuathiri mwenzi wake? Nini wajibu na haki za mtu kwenye mapenzi? Ni kwa namna gani mtindo wa maisha wa bachela, ukitekelezwa na mwanandoa ni sumu?
Hayo na mengine mengi, yanachambuliwa kinagaubaga kwenye katiba ya mapenzi. Mtu sahihi ni yule anayeishi kwa kujiamini, si ambaye anafanya kwa kujaribu, akisubiria matokeo au mapokeo ya mpenzi wake. Mapenzi ni rahisi mno endapo utaheshimu muongozo.
Katiba yenyewe inaundwa na vipengele vingi ambavyo nitavichambua katika wigo mpana ili uweze kuelewa ipasavyo. Inahitaji utulivu na umakini wakati wa kusoma, mwisho utakuwa ni mwenye mafanikio makubwa endapo yaliyomo kwenye maandishi yangu yatakita vilivyo ndani ya ubongo.

UPENDO
Hiki ni kipengele kikuu. Unaweza kukiita kifungu mama ndani ya katiba ya mapenzi. Huwezi kusema upo kwenye uhusiano makini kama upendo haupo katikati. Chukua hatua madhubuti endapo utabaini upendo haupo.
Mkatae mwenzi ambaye hakupendi, kinyume chake atakupa mateso mbele ya safari.
Muongozo wa kipengele cha upendo ni kwamba lazima wewe mwenyewe uanze kuwekeza upendo kisha naye akupende.
Ni maisha ya ubinafsi kutaraji kupendwa, wakati wewe mwenyewe huoneshi kwa mwenzako. Zingatia hili kila siku na wakati wote ili uweze kufaidi matunda mema kwenye uhusiano wako.
Kuna tabaka la watu ambao huishi kwa kusikilizia zaidi.
Haitakiwi kutegea, upendo unamaanisha pande mbili zinazovutana. Huyu anatekeleza hili kwa ajili ya mwenzake, hali kadhalika na mwingine anasimama imara kuhakikisha mpenzi wake anafaidi malisho mema ya mapenzi. Hakikisha mpenzi wako hakushindi upendo, onesha unampenda zaidi.
Upendo huyeyusha mengi. Ukiwekeza upendo kwa mwenzi wako, utamfanya nafsi yake iwe na woga. Ni rahisi kushinda vishawishi, kama atakuwa akikaa peke yake anakuwa anajiridhisha kuwa unampenda kwa moyo wako wote. Vinginevyo, anaweza kushawishika na kukusaliti kama tu akili yake itamtuma kuamini kwamba humpendi.
Hivyo basi, hakikisha upendo wako si wa wasiwasi. Mfanye awe na imani, ikibidi imani ya kupitiliza. Utafiti unaonesha kuwa mtu aliyeonesha upendo mkubwa kisha akasaliti kwa tamaa zake, anapobainika na kuachwa hujuta zaidi kuliko yule aliyeona hakukuwa na upendo kwa sababu haoni cha kupoteza.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpulishers.info

No comments: